Isaya 24:1-23
Isaya 24:1-23 BHN
Sasa Mwenyezi-Mungu anaiharibu dunia na kuifanya tupu. Atausokota uso wa dunia na kuwatawanya wakazi wake. Kila mtu atapatwa na mambo yaleyale: Mtu wa kawaida na kuhani; mtumwa na bwana wake; mjakazi na bibi yake; mnunuzi na mwuzaji; mkopeshaji na mkopaji; mdai na mdaiwa. Dunia itaharibiwa kabisa na kuangamizwa; Mwenyezi-Mungu ametamka hayo. Dunia inakauka na kunyauka; ulimwengu unafadhaika na kunyauka; mbingu zinafadhaika pamoja na dunia. Watu wameitia najisi dunia maana wamezivunja sheria za Mungu, wamezikiuka kanuni zake, wamelivunja agano lake la milele. Kwa sababu hiyo laana inaitokomeza dunia, wakazi wake wanateseka kwa makosa yao. Wakazi wa dunia wamepungua, ni watu wachache tu waliosalia. Mizabibu inanyauka, divai inakosekana. Wote waliokuwa wenye furaha sasa wanasononeka kwa huzuni. Mdundo wa vigoma umekoma, nderemo na vifijo vimetoweka; midundo ya vinubi imekomeshwa. Hakuna tena kunywa divai na kuimba; mvinyo umekuwa mchungu kwa wanywaji. Mji uliohamwa umejaa uharibifu; kila nyumba imefungwa asiingie mtu. Kuna kilio barabarani kwa kukosa divai; shangwe yote imekoma, furaha imetoweka duniani. Mji ni magofu matupu; malango yake yamevunjwavunjwa. Kama vile zeituni chache tu juu ya mzeituni au tini chache tu juu ya mtini baada ya kumaliza mavuno, ndivyo itakavyokuwa katika nchi zote: Watu wachache watabakia hai. Watakaosalia watapaza sauti, wataimba kwa shangwe. Kutoka magharibi watatangaza ukuu wa Mwenyezi-Mungu, nao wakazi wa mashariki watamsifu. Watu wa mbali watalisifu jina la Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli. Tunasikia nyimbo za sifa kutoka miisho ya dunia, nyimbo za kumsifu Mungu aliye mwadilifu. Lakini mimi ninanyongonyea, naam, ninanyongonyea. Ole wangu mimi! Wasaliti wanaendelea kuwa wasaliti, usaliti wao unazidi kuwa mbaya zaidi. Hofu, mashimo na mitego, hivi ndivyo vinavyowangojeni enyi wakazi wa dunia. Atakayeikimbia hofu atatumbukia shimoni; atakayetoka shimoni atanaswa mtegoni. Madirisha ya mbinguni yamefunguliwa, misingi ya dunia inatikisika. Dunia inavunjikavunjika, inapasuka na kutikiswatikiswa. Inapepesuka kama mlevi, inayumbayumba kama kibanda. Imelemewa na mzigo wa dhambi zake nayo itaanguka wala haitainuka tena. Siku ile Mwenyezi-Mungu ataliadhibu jeshi la angani kadhalika na wafalme wa duniani. Wote watakusanywa kama wafungwa shimoni; watafungwa gerezani pamoja kwa miaka mingi, na baada ya muda huo atawaadhibu. Kisha mwezi utaaibishwa, nalo jua litaona aibu kuangaza, kwa kuwa Mwenyezi-Mungu wa majeshi atatawala huko Yerusalemu katika mlima Siyoni; ataonesha wazee wa watu wake utukufu wake.