Isaya 11:1-10
Isaya 11:1-10 Biblia Habari Njema (BHN)
Kutatokea chipukizi katika kisiki cha Yese, tawi litachipua mizizini mwake. Roho ya Mwenyezi-Mungu itakaa kwake, roho ya hekima na maarifa, roho ya shauri jema na nguvu, roho ya ujuzi na ya kumcha Mwenyezi-Mungu. Atafurahia kumcha Mwenyezi-Mungu. Hatahukumu kadiri ya mambo ya njenje, wala kuamua kufuatana na yale anayosikia. Atawapatia haki watu maskini, atawaamulia sawasawa wanyonge nchini. Kwa neno lake ataiadhibu dunia, kwa tamko lake atawaua waovu. Haki itakuwa kama mkanda wa kujifunga, uaminifu utakaa naye kama mkanda kiunoni. Mbwamwitu ataishi pamoja na mwanakondoo, chui watapumzika pamoja na mwanambuzi. Ndama na wanasimba watakula pamoja, na mtoto mdogo atawaongoza. Ngombe na dubu watakula pamoja, ndama wao watapumzika pamoja; na simba atakula majani kama ng'ombe. Mtoto mchanga atacheza kwenye shimo la nyoka mtoto ataweza kutia mkono shimoni mwa nyoka wa sumu. Katika mlima mtakatifu wa Mungu hakutakuwa na madhara wala uharibifu. Maana kumjua Mwenyezi-Mungu kutaenea pote nchini, kama vile maji yajaavyo baharini. Siku ile chipukizi wa Yese atakuwa ishara kwa mataifa; mataifa yatamtafuta na makazi yake yatatukuka.
Isaya 11:1-10 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Basi litatoka chipukizi katika shina la Yese, na tawi litakalotoka katika mizizi yake litazaa matunda. Na Roho ya BWANA itakaa juu yake, roho ya hekima na ufahamu, roho ya shauri na uweza, roho ya maarifa na ya kumcha BWANA; na furaha yake itakuwa katika kumcha BWANA; wala hatahukumu kwa kuyafuata ayaonayo kwa macho yake, wala hataonya kwa kuyafuata ayasikiayo kwa masikio yake; bali kwa haki atawahukumu maskini, naye atawaonya wanyenyekevu wa dunia kwa adili; naye ataipiga dunia kwa fimbo ya kinywa chake, na kwa pumzi ya midomo yake atawaua wabaya. Na haki itakuwa mshipi wa viuno vyake, na uaminifu mshipi wa kujifungia. Mbwamwitu atakaa pamoja na mwana-kondoo, na chui atalala pamoja na mwana-mbuzi; ndama na mwanasimba na ng'ombe wanono watakuwa pamoja, na mtoto mdogo atawaongoza. Ng'ombe na dubu watalisha pamoja; watoto wao watalala pamoja; na simba atakula majani kama ng'ombe. Na mtoto anyonyaye atacheza penye tundu la nyoka, na mtoto aliyeachishwa kunyonya atatia mkono wake katika pango la fira. Hawatadhuru wala hawataharibu katika mlima wangu wote mtakatifu; maana dunia itajawa na kumjua BWANA, kama vile maji yanavyoifunika bahari. Na itakuwa katika siku hiyo, shina la Yese lisimamalo kuwa ishara kwa makabila ya watu, yeye ndiye ambaye mataifa watamtafuta; na mahali pake pa kupumzikia patakuwa na utukufu.
Isaya 11:1-10 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Basi litatoka chipukizi katika shina la Yese, na tawi litakalotoka katika mizizi yake litazaa matunda. Na roho ya BWANA atakaa juu yake, roho ya hekima na ufahamu, roho ya shauri na uweza, roho ya maarifa na ya kumcha BWANA; na furaha yake itakuwa katika kumcha BWANA; wala hatahukumu kwa kuyafuata ayaonayo kwa macho yake, wala hataonya kwa kuyafuata ayasikiayo kwa masikio yake; bali kwa haki atawahukumu maskini, naye atawaonya wanyenyekevu wa dunia kwa adili; naye ataipiga dunia kwa fimbo ya kinywa chake, na kwa pumzi ya midomo yake atawaua wabaya. Na haki itakuwa mshipi wa viuno vyake, na uaminifu mshipi wa kujifungia. Mbwa-mwitu atakaa pamoja na mwana-kondoo, na chui atalala pamoja na mwana-mbuzi; ndama na mwana-simba na kinono watakuwa pamoja, na mtoto mdogo atawaongoza. Ng’ombe na dubu watalisha pamoja; watoto wao watalala pamoja; na simba atakula majani kama ng’ombe. Na mtoto anyonyaye atacheza penye tundu la nyoka, na mtoto aliyeachishwa atatia mkono wake katika pango la fira. Hawatadhuru wala hawataharibu katika mlima wangu wote mtakatifu; maana dunia itajawa na kumjua BWANA, kama vile maji yanavyoifunika bahari. Na itakuwa katika siku hiyo, shina la Yese lisimamalo kuwa ishara kwa kabila za watu, yeye ndiye ambaye mataifa watamtafuta; na mahali pake pa kupumzikia patakuwa na utukufu.
Isaya 11:1-10 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Chipukizi litatokea kutoka shina la Yese, kutoka mizizi yake Tawi litazaa tunda. Roho wa BWANA atakaa juu yake, Roho wa hekima na wa ufahamu, Roho wa shauri na wa uweza, Roho wa maarifa na wa kumcha BWANA naye atafurahia kumcha BWANA. Hatahukumu kwa yale ayaonayo kwa macho yake, wala kuamua kwa yale ayasikiayo kwa masikio yake, bali kwa uadilifu atahukumu wahitaji, kwa haki ataamua wanyenyekevu wa dunia. Ataipiga dunia kwa fimbo ya kinywa chake, kwa pumzi ya midomo yake atawaua waovu. Haki itakuwa mkanda wake na uaminifu utakuwa mshipi kiunoni mwake. Mbwa mwitu ataishi pamoja na mwana-kondoo, naye chui atalala pamoja na mbuzi, ndama, mwana simba na ngʼombe wa mwaka mmoja watakaa pamoja, naye mtoto mdogo atawaongoza. Ngʼombe na dubu watalisha pamoja, watoto wao watalala pamoja, na simba atakula majani makavu kama maksai. Mtoto mchanga atacheza karibu na shimo la nyoka, naye mtoto mdogo ataweka mkono wake kwenye kiota cha fira. Hawatadhuru wala kuharibu juu ya mlima wangu mtakatifu wote, kwa kuwa dunia itajawa na kumjua BWANA kama maji yajazavyo bahari. Katika siku hiyo, Shina la Yese atasimama kama bendera kwa ajili ya mataifa. Mataifa yatakusanyika kwake, na mahali pake pa kupumzikia patakuwa utukufu.