Isaya 11:1-10
Isaya 11:1-10 NEN
Chipukizi litatokea kutoka shina la Yese, kutoka mizizi yake Tawi litazaa tunda. Roho wa BWANA atakaa juu yake, Roho wa hekima na wa ufahamu, Roho wa shauri na wa uweza, Roho wa maarifa na wa kumcha BWANA naye atafurahia kumcha BWANA. Hatahukumu kwa yale ayaonayo kwa macho yake, wala kuamua kwa yale ayasikiayo kwa masikio yake, bali kwa uadilifu atahukumu wahitaji, kwa haki ataamua wanyenyekevu wa dunia. Ataipiga dunia kwa fimbo ya kinywa chake, kwa pumzi ya midomo yake atawaua waovu. Haki itakuwa mkanda wake na uaminifu utakuwa mshipi kiunoni mwake. Mbwa mwitu ataishi pamoja na mwana-kondoo, naye chui atalala pamoja na mbuzi, ndama, mwana simba na ngʼombe wa mwaka mmoja watakaa pamoja, naye mtoto mdogo atawaongoza. Ngʼombe na dubu watalisha pamoja, watoto wao watalala pamoja, na simba atakula majani makavu kama maksai. Mtoto mchanga atacheza karibu na shimo la nyoka, naye mtoto mdogo ataweka mkono wake kwenye kiota cha fira. Hawatadhuru wala kuharibu juu ya mlima wangu mtakatifu wote, kwa kuwa dunia itajawa na kumjua BWANA kama maji yajazavyo bahari. Katika siku hiyo, Shina la Yese atasimama kama bendera kwa ajili ya mataifa. Mataifa yatakusanyika kwake, na mahali pake pa kupumzikia patakuwa utukufu.