Hosea 11:1-11
Hosea 11:1-11 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Israeli alipokuwa mtoto, nalikuwa nikimpenda, nikamwita mwanangu atoke Misri. Kadiri walivyowaita ndivyo walivyoondoka na kuwaacha; waliwatolea dhabihu Mabaali, na kuzifukizia uvumba sanamu za kuchonga. Lakini nalimfundisha Efraimu kwenda kwa miguu; naliwachukua mikononi mwangu; hawakujua ya kuwa naliwaponya. Naliwavuta kwa kamba za kibinadamu, kwa mafungo ya upendo; nami nalikuwa kwao kama hao waondoao kongwa tayani mwao, nikaandika chakula mbele yao. Hatarudi tena nchi ya Misri; bali huyo Mwashuri atakuwa mfalme wake; kwa sababu walikataa kurejea. Na upanga utaiangukia miji yake, utayaharibu makomeo yake na kuyala, kwa sababu ya mashauri yao wenyewe. Na watu wangu wamejipinda kuniacha; ingawa wawaita kwenda kwake Aliye juu, hapana hata mmoja atakayemtukuza. Niwezeje kukuacha, Efraimu? Niwezeje kukuponya, Israeli? Niwezeje kukufanya kama Adma? Niwezeje kukuweka kama Seboimu? Moyo wangu umegeuka ndani yangu, huruma zangu zimewaka pamoja. Sitatumia ukali wa hasira yangu, sitarudi kumwangamiza Efraimu; kwa maana mimi ni Mungu, si mwanadamu mimi; mimi ndiye aliye Mtakatifu katikati yenu; wala sitaingia ndani ya mji. Watakwenda kumfuata BWANA, atakayenguruma kama simba; kwa maana atanguruma, nao watoto watakuja kutoka magharibi wakitetemeka. Watakuja wakitetemeka kama shomoro, toka Misri, na kama hua, toka nchi ya Ashuru; nami nitawakalisha katika nyumba zao, asema BWANA.
Hosea 11:1-11 Biblia Habari Njema (BHN)
“Israeli alipokuwa mtoto, nilimpenda, Kutoka Misri nilimwita mwanangu. Lakini kadiri nilivyozidi kuwaita, ndivyo walivyozidi kwenda mbali nami; waliendelea kuyatambikia Mabaali, na kuvifukizia ubani vinyago vya miungu. Mimi ndiye niliyemfundisha Efraimu kutembea! Mimi mwenyewe niliwachukua mikononi mwangu; lakini hawakutambua kuwa mimi ndiye niliyewatunza. Niliwaongoza kwa kamba za huruma naam, kwa kamba za upendo; kama baba amwinuaye mtoto mpaka shavuni mwake, ndivyo nami nilivyokuwa kwao. Mimi niliinama chini na kuwalisha. Basi, watarudi nchini Misri; watatawaliwa na mfalme wa Ashuru, kwa sababu wamekataa kunirudia. “Upanga utavuma katika miji yao, utavunjavunja miimo ya malango yake na kuwaangamiza katika ngome zao. Watu wangu wamepania kuniacha mimi, wakiitwa waje juu, hakuna hata mmoja anayeweza. Ewe Efraimu, nawezaje kukuacha? Nawezaje kukutupa ewe Israeli? Nitawezaje kukufanya kama mji wa Adma? Nitawezaje kukutenda kama Seboimu! Nazuiwa na moyo wangu; huruma yangu imezidi kuwa motomoto. Nitaizuia hasira yangu kali; sitamwangamiza tena Efraimu, maana mimi ni Mungu, wala si binadamu. “Mimi ndimi Mtakatifu miongoni mwenu, nami sitakuja kuwaangamiza. “Watanifuata mimi Mwenyezi-Mungu ningurumaye kama simba; nitakaponguruma watanijia toka magharibi wakitetemeka. Watakuja kutoka Misri wakitetemeka kama ndege, wataruka kutoka Ashuru kama hua nami nitawarudisha makwao; mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.
Hosea 11:1-11 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Israeli alipokuwa mtoto, nilikuwa nikimpenda, nikamwita mwanangu atoke Misri. Kadiri walivyowaita ndivyo walivyoondoka na kuwaacha; waliwatolea dhabihu Mabaali, na kuzifukizia uvumba sanamu za kuchonga. Lakini nilimfundisha Efraimu kwenda kwa miguu; niliwachukua mikononi mwangu; hawakujua ya kuwa niliwaponya. Niliwavuta kwa kamba za kibinadamu, kwa mafungo ya upendo; nami nilikuwa kwao kama hao waondoao kongwa tayani mwao, nikaandaa chakula mbele yao. Hatarudi tena nchi ya Misri; bali huyo Mwashuri atakuwa mfalme wake; kwa sababu walikataa kurejea. Na upanga utaiangukia miji yake, utayaharibu makomeo yake na kuyala, kwa sababu ya mashauri yao wenyewe. Na watu wangu wamejipinda kuniacha; ingawa wawaita kwenda kwake Aliye Juu, hapana hata mmoja atakayemtukuza. Niwezeje kukuacha, Efraimu? Niwezeje kukuachilia Israeli? Niwezeje kukufanya kama Adma? Niwezeje kukuweka kama Seboimu? Moyo wangu umegeuka ndani yangu, huruma zangu zimewaka pamoja. Sitatumia ukali wa hasira yangu, sitamwangamiza Efraimu tena; kwa maana mimi ni Mungu, si mwanadamu mimi; mimi ndiye aliye Mtakatifu katikati yenu; wala sitaingia ndani ya mji. Watakwenda kumfuata BWANA, atakayenguruma kama simba; kwa maana atanguruma, nao watoto watakuja kutoka magharibi wakitetemeka. Watakuja wakitetemeka kama shomoro, toka Misri, na kama hua, toka nchi ya Ashuru; nami nitawakalisha katika nyumba zao, asema BWANA.
Hosea 11:1-11 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
“Wakati Israeli alipokuwa mtoto, nilimpenda, nilimwita mwanangu kutoka Misri. Lakini kadiri nilivyomwita Israeli, ndivyo walivyokwenda mbali nami. Walitoa dhabihu kwa Mabaali na kufukiza uvumba kwa vinyago. Mimi ndiye niliyemfundisha Efraimu kutembea, nikiwashika mikono; lakini hawakutambua kuwa ni mimi niliyewaponya. Niliwaongoza kwa kamba za huruma ya kibinadamu, kwa vifungo vya upendo; niliondoa nira shingoni mwao nami nikainama kuwalisha. “Je, hawatarudi Misri, nayo Ashuru haitawatawala kwa sababu wamekataa kutubu? Panga zitametameta katika miji yao, zitaharibu makomeo ya malango yao na kukomesha mipango yao. Watu wangu wamedhamiria kuniacha. Hata kama wakimwita Yeye Aliye Juu Sana, kwa vyovyote hatawainua. “Efraimu, ninawezaje kukuacha? Ee Israeli, ninawezaje kukutoa? Nitawezaje kukutendea kama Adma? Nitawezaje kukufanya kama Seboimu? Moyo wangu umegeuka ndani yangu, huruma zangu zote zimeamshwa. Sitatimiza hasira yangu kali, wala sitageuka na kumharibu Efraimu. Kwa kuwa mimi ndimi Mungu, wala si mwanadamu, Aliye Mtakatifu miongoni mwenu. Sitakuja kwa ghadhabu. Watamfuata BWANA; atanguruma kama simba. Wakati angurumapo, watoto wake watakuja wakitetemeka kutoka magharibi. Watakuja wakitetemeka kama ndege wakitoka Misri, kama hua wakitoka Ashuru. Nitawakalisha katika nyumba zao,” asema BWANA.