Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Hosea 11:1-11

Hosea 11:1-11 SRUV

Israeli alipokuwa mtoto, nilikuwa nikimpenda, nikamwita mwanangu atoke Misri. Kadiri walivyowaita ndivyo walivyoondoka na kuwaacha; waliwatolea dhabihu Mabaali, na kuzifukizia uvumba sanamu za kuchonga. Lakini nilimfundisha Efraimu kwenda kwa miguu; niliwachukua mikononi mwangu; hawakujua ya kuwa niliwaponya. Niliwavuta kwa kamba za kibinadamu, kwa mafungo ya upendo; nami nilikuwa kwao kama hao waondoao kongwa tayani mwao, nikaandaa chakula mbele yao. Hatarudi tena nchi ya Misri; bali huyo Mwashuri atakuwa mfalme wake; kwa sababu walikataa kurejea. Na upanga utaiangukia miji yake, utayaharibu makomeo yake na kuyala, kwa sababu ya mashauri yao wenyewe. Na watu wangu wamejipinda kuniacha; ingawa wawaita kwenda kwake Aliye Juu, hapana hata mmoja atakayemtukuza. Niwezeje kukuacha, Efraimu? Niwezeje kukuachilia Israeli? Niwezeje kukufanya kama Adma? Niwezeje kukuweka kama Seboimu? Moyo wangu umegeuka ndani yangu, huruma zangu zimewaka pamoja. Sitatumia ukali wa hasira yangu, sitamwangamiza Efraimu tena; kwa maana mimi ni Mungu, si mwanadamu mimi; mimi ndiye aliye Mtakatifu katikati yenu; wala sitaingia ndani ya mji. Watakwenda kumfuata BWANA, atakayenguruma kama simba; kwa maana atanguruma, nao watoto watakuja kutoka magharibi wakitetemeka. Watakuja wakitetemeka kama shomoro, toka Misri, na kama hua, toka nchi ya Ashuru; nami nitawakalisha katika nyumba zao, asema BWANA.

Soma Hosea 11