Waebrania 10:5-10
Waebrania 10:5-10 Biblia Habari Njema (BHN)
Ndiyo maana Kristo alipokuwa anakuja ulimwenguni, alimwambia Mungu: “Hukutaka tambiko wala sadaka, lakini umenitayarishia mwili. Sadaka za kuteketezwa au za kuondoa dhambi hazikupendezi. Hapo nikasema: ‘Niko hapa, ee Mungu, kutimiza matakwa yako kama ilivyoandikwa juu yangu katika kitabu cha sheria.’” Kwanza alisema: “Hutaki wala hupendezwi na tambiko, sadaka za kuteketezwa na za kuondoa dhambi.” Alisema hivyo ingawa sadaka hizi zote hutolewa kufuatana na sheria. Kisha akasema: “Niko hapa, ee Mungu, tayari kufanya matakwa yako.” Hivyo Mungu alibatilisha tambiko za zamani na mahali pake akaweka tambiko nyingine moja. Kwa kuwa Yesu Kristo alitimiza matakwa ya Mungu, sisi tunatakaswa dhambi zetu kwa ile tambiko ya mwili wake aliyotoa mara moja tu, ikatosha.
Waebrania 10:5-10 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Kwa hiyo alipokuja ulimwenguni, alisema, Dhabihu na matoleo hukutaka, Lakini mwili uliniwekea tayari; Sadaka za kuteketezwa na sadaka za dhambi hukupendezwa nazo; Ndipo niliposema, Tazama, nimekuja (katika gombo la kitabu nimeandikiwa) Niyafanye mapenzi yako, Mungu. Hapo juu asemapo, Dhabihu na matoleo na sadaka za kuteketezwa na hizo za dhambi hukuzitaka, wala hukupendezwa nazo (zitolewazo kama ilivyoamuru torati), ndipo aliposema, Tazama, nimekuja niyafanye mapenzi yako. Aondoa la kwanza, ili kusudi alisimamishe la pili. Katika mapenzi hayo mmepata utakaso, kwa kutolewa mwili wa Yesu Kristo mara moja tu.
Waebrania 10:5-10 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Kwa hiyo ajapo ulimwenguni, asema, Dhabihu na toleo hukutaka, Lakini mwili uliniwekea tayari; Sadaka za kuteketezwa na sadaka za dhambi hukupendezwa nazo; Ndipo niliposema, Tazama, nimekuja (katika gombo la chuo nimeandikiwa) Niyafanye mapenzi yako, Mungu. Hapo juu asemapo, Dhabihu na matoleo na sadaka za kuteketezwa na hizo za dhambi hukuzitaka, wala hukupendezwa nazo (zitolewazo kama ilivyoamuru torati), ndipo aliposema, Tazama, nimekuja niyafanye mapenzi yako. Aondoa la kwanza, ili kusudi alisimamishe la pili. Katika mapenzi hayo mmepata utakaso, kwa kutolewa mwili wa Yesu Kristo mara moja tu.
Waebrania 10:5-10 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Kwa hiyo, Kristo alipokuja duniani, alisema: “Dhabihu na sadaka hukuzitaka, bali mwili uliniandalia; sadaka za kuteketezwa na za dhambi hukupendezwa nazo. Ndipo niliposema, ‘Mimi hapa, nimekuja, imeandikwa kunihusu katika kitabu: Nimekuja kuyafanya mapenzi yako, Ee Mungu.’ ” Kwanza alisema, “Dhabihu na sadaka, sadaka za kuteketezwa na za dhambi hukuzitaka, wala hukupendezwa nazo” (ingawa sheria iliagiza zitolewe). Kisha akasema “Mimi hapa, nimekuja kuyafanya mapenzi yako.” Aondoa lile Agano la kwanza ili kuimarisha la pili. Katika mapenzi hayo sisi tumetakaswa na kufanywa watakatifu kwa njia ya sadaka ya mwili wa Yesu Kristo alioutoa mara moja tu.