Waebrania 10:1-8
Waebrania 10:1-8 Biblia Habari Njema (BHN)
Kwa vile sheria ni kivuli tu cha mambo mema yatakayokuja na si picha kamili ya mambo yale halisi, tambiko zilezile za sheria zinazotolewa mwaka hata mwaka, haziwezi kamwe kuwafanya wale wanaoabudu wawe wakamilifu! Kama hao watu wanaomwabudu Mungu wangekuwa wametakaswa dhambi zao kweli, hawangejisikia tena kuwa na dhambi, na tambiko hizo zote zingekoma. Lakini tambiko hizo hufanyika kila mwaka kuwakumbusha watu dhambi zao. Maana damu ya fahali na mbuzi haiwezi kamwe kuondoa dhambi. Ndiyo maana Kristo alipokuwa anakuja ulimwenguni, alimwambia Mungu: “Hukutaka tambiko wala sadaka, lakini umenitayarishia mwili. Sadaka za kuteketezwa au za kuondoa dhambi hazikupendezi. Hapo nikasema: ‘Niko hapa, ee Mungu, kutimiza matakwa yako kama ilivyoandikwa juu yangu katika kitabu cha sheria.’” Kwanza alisema: “Hutaki wala hupendezwi na tambiko, sadaka za kuteketezwa na za kuondoa dhambi.” Alisema hivyo ingawa sadaka hizi zote hutolewa kufuatana na sheria.
Waebrania 10:1-8 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Basi torati, kwa kuwa ni kivuli cha mema yatakayokuwa, wala si sura yenyewe ya mambo hayo, kwa dhabihu zile zile wanazozitoa kila mwaka daima, haiwezi wakati wowote kuwakamilisha wakaribiao. Kama ndivyo, je! Dhabihu hazingekoma kutolewa; kwa maana waabuduo, wakiisha kusafishwa mara moja, wasingejiona tena kuwa na dhambi? Lakini katika dhabihu hizo liko kumbukumbu la dhambi kila mwaka. Maana haiwezekani damu ya mafahali na mbuzi kuondoa dhambi. Kwa hiyo alipokuja ulimwenguni, alisema, Dhabihu na matoleo hukutaka, Lakini mwili uliniwekea tayari; Sadaka za kuteketezwa na sadaka za dhambi hukupendezwa nazo; Ndipo niliposema, Tazama, nimekuja (katika gombo la kitabu nimeandikiwa) Niyafanye mapenzi yako, Mungu. Hapo juu asemapo, Dhabihu na matoleo na sadaka za kuteketezwa na hizo za dhambi hukuzitaka, wala hukupendezwa nazo (zitolewazo kama ilivyoamuru torati)
Waebrania 10:1-8 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Basi torati, kwa kuwa ni kivuli cha mema yatakayokuwa, wala si sura yenyewe ya mambo hayo, kwa dhabihu zile zile wanazozitoa kila mwaka daima, haiwezi wakati wo wote kuwakamilisha wakaribiao. Kama ndivyo, je! Dhabihu hazingekoma kutolewa; kwa maana waabuduo, wakiisha kusafishwa mara moja, wasingejiona tena kuwa na dhambi? Lakini katika dhabihu hizo liko kumbukumbu la dhambi kila mwaka. Maana haiwezekani damu ya mafahali na mbuzi kuondoa dhambi. Kwa hiyo ajapo ulimwenguni, asema, Dhabihu na toleo hukutaka, Lakini mwili uliniwekea tayari; Sadaka za kuteketezwa na sadaka za dhambi hukupendezwa nazo; Ndipo niliposema, Tazama, nimekuja (katika gombo la chuo nimeandikiwa) Niyafanye mapenzi yako, Mungu. Hapo juu asemapo, Dhabihu na matoleo na sadaka za kuteketezwa na hizo za dhambi hukuzitaka, wala hukupendezwa nazo (zitolewazo kama ilivyoamuru torati)
Waebrania 10:1-8 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Sheria ni kivuli tu cha mambo mema yajayo, wala si uhalisi wa mambo yenyewe. Kwa sababu hii, haiwezekani kamwe kwa njia ya dhabihu zitolewazo mwaka hadi mwaka kuwakamilisha wale wanaokaribia ili kuabudu. Kama dhabihu hizo zingeweza kuwakamilisha, hazingeendelea kutolewa tena. Kwa kuwa hao waabuduo wangekuwa wametakaswa mara moja tu, wala wasingejiona tena kuwa na dhambi. Lakini zile dhabihu zilikuwa ukumbusho wa dhambi kila mwaka, kwa sababu haiwezekani damu ya mafahali na mbuzi kuondoa dhambi. Kwa hiyo, Kristo alipokuja duniani, alisema: “Dhabihu na sadaka hukuzitaka, bali mwili uliniandalia; sadaka za kuteketezwa na za dhambi hukupendezwa nazo. Ndipo niliposema, ‘Mimi hapa, nimekuja, imeandikwa kunihusu katika kitabu: Nimekuja kuyafanya mapenzi yako, Ee Mungu.’ ” Kwanza alisema, “Dhabihu na sadaka, sadaka za kuteketezwa na za dhambi hukuzitaka, wala hukupendezwa nazo” (ingawa sheria iliagiza zitolewe).