Waebrania 10:1-18
Waebrania 10:1-18 Biblia Habari Njema (BHN)
Kwa vile sheria ni kivuli tu cha mambo mema yatakayokuja na si picha kamili ya mambo yale halisi, tambiko zilezile za sheria zinazotolewa mwaka hata mwaka, haziwezi kamwe kuwafanya wale wanaoabudu wawe wakamilifu! Kama hao watu wanaomwabudu Mungu wangekuwa wametakaswa dhambi zao kweli, hawangejisikia tena kuwa na dhambi, na tambiko hizo zote zingekoma. Lakini tambiko hizo hufanyika kila mwaka kuwakumbusha watu dhambi zao. Maana damu ya fahali na mbuzi haiwezi kamwe kuondoa dhambi. Ndiyo maana Kristo alipokuwa anakuja ulimwenguni, alimwambia Mungu: “Hukutaka tambiko wala sadaka, lakini umenitayarishia mwili. Sadaka za kuteketezwa au za kuondoa dhambi hazikupendezi. Hapo nikasema: ‘Niko hapa, ee Mungu, kutimiza matakwa yako kama ilivyoandikwa juu yangu katika kitabu cha sheria.’” Kwanza alisema: “Hutaki wala hupendezwi na tambiko, sadaka za kuteketezwa na za kuondoa dhambi.” Alisema hivyo ingawa sadaka hizi zote hutolewa kufuatana na sheria. Kisha akasema: “Niko hapa, ee Mungu, tayari kufanya matakwa yako.” Hivyo Mungu alibatilisha tambiko za zamani na mahali pake akaweka tambiko nyingine moja. Kwa kuwa Yesu Kristo alitimiza matakwa ya Mungu, sisi tunatakaswa dhambi zetu kwa ile tambiko ya mwili wake aliyotoa mara moja tu, ikatosha. Kila kuhani Myahudi hutoa huduma yake ya ibada ya kila siku na kutoa tambiko zilezile mara nyingi, tambiko ambazo haziwezi kuondoa dhambi. Lakini Kristo alitoa tambiko moja kwa ajili ya dhambi, tambiko ifaayo milele, kisha, akaketi upande wa kulia wa Mungu, anangoja maadui zake wafanywe kama kibao chini ya miguu yake. Basi, kwa tambiko yake moja, amewafanya kuwa wakamilifu milele wote wale wanaotakaswa dhambi zao. Naye Roho Mtakatifu anatupa ushahidi wake. Kwanza anasema: “Hili ndilo agano nitakalofanya nao, siku zijazo, asema Bwana: Nitaweka sheria zangu mioyoni mwao, na kuziandika akilini mwao.” Kisha akaongeza kusema: “Sitakumbuka tena dhambi zao, wala vitendo vyao vya uhalifu.” Basi, dhambi zikisha ondolewa, hakutakuwa na haja tena ya kutoa tambiko za kuondoa dhambi.
Waebrania 10:1-18 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Basi torati, kwa kuwa ni kivuli cha mema yatakayokuwa, wala si sura yenyewe ya mambo hayo, kwa dhabihu zile zile wanazozitoa kila mwaka daima, haiwezi wakati wowote kuwakamilisha wakaribiao. Kama ndivyo, je! Dhabihu hazingekoma kutolewa; kwa maana waabuduo, wakiisha kusafishwa mara moja, wasingejiona tena kuwa na dhambi? Lakini katika dhabihu hizo liko kumbukumbu la dhambi kila mwaka. Maana haiwezekani damu ya mafahali na mbuzi kuondoa dhambi. Kwa hiyo alipokuja ulimwenguni, alisema, Dhabihu na matoleo hukutaka, Lakini mwili uliniwekea tayari; Sadaka za kuteketezwa na sadaka za dhambi hukupendezwa nazo; Ndipo niliposema, Tazama, nimekuja (katika gombo la kitabu nimeandikiwa) Niyafanye mapenzi yako, Mungu. Hapo juu asemapo, Dhabihu na matoleo na sadaka za kuteketezwa na hizo za dhambi hukuzitaka, wala hukupendezwa nazo (zitolewazo kama ilivyoamuru torati), ndipo aliposema, Tazama, nimekuja niyafanye mapenzi yako. Aondoa la kwanza, ili kusudi alisimamishe la pili. Katika mapenzi hayo mmepata utakaso, kwa kutolewa mwili wa Yesu Kristo mara moja tu. Na kila kuhani husimama kila siku akifanya ibada, na kutoa dhabihu zile zile mara nyingi; ambazo haziwezi kabisa kuondoa dhambi. Lakini huyu, alipokwisha kutoa kwa ajili ya dhambi dhabihu moja idumuyo hata milele, aliketi mkono wa kulia wa Mungu; tangu hapo akingojea hata adui zake wawekwe kuwa chini ya miguu yake. Maana kwa toleo moja amewakamilisha hata milele hao wanaotakaswa. Na Roho Mtakatifu naye amshuhudia; kwa maana, baada ya kusema, Hili ni agano nitakaloagana nao baada ya siku zile, anena Bwana, Nitatia sheria zangu mioyoni mwao, Na katika fikira zao nitaziandika; ndipo anenapo, Dhambi zao na uasi wao sitaukumbuka tena kabisa. Basi, ondoleo la hayo likiwapo, hapana toleo tena kwa ajili ya dhambi.
Waebrania 10:1-18 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Basi torati, kwa kuwa ni kivuli cha mema yatakayokuwa, wala si sura yenyewe ya mambo hayo, kwa dhabihu zile zile wanazozitoa kila mwaka daima, haiwezi wakati wo wote kuwakamilisha wakaribiao. Kama ndivyo, je! Dhabihu hazingekoma kutolewa; kwa maana waabuduo, wakiisha kusafishwa mara moja, wasingejiona tena kuwa na dhambi? Lakini katika dhabihu hizo liko kumbukumbu la dhambi kila mwaka. Maana haiwezekani damu ya mafahali na mbuzi kuondoa dhambi. Kwa hiyo ajapo ulimwenguni, asema, Dhabihu na toleo hukutaka, Lakini mwili uliniwekea tayari; Sadaka za kuteketezwa na sadaka za dhambi hukupendezwa nazo; Ndipo niliposema, Tazama, nimekuja (katika gombo la chuo nimeandikiwa) Niyafanye mapenzi yako, Mungu. Hapo juu asemapo, Dhabihu na matoleo na sadaka za kuteketezwa na hizo za dhambi hukuzitaka, wala hukupendezwa nazo (zitolewazo kama ilivyoamuru torati), ndipo aliposema, Tazama, nimekuja niyafanye mapenzi yako. Aondoa la kwanza, ili kusudi alisimamishe la pili. Katika mapenzi hayo mmepata utakaso, kwa kutolewa mwili wa Yesu Kristo mara moja tu. Na kila kuhani husimama kila siku akifanya ibada, na kutoa dhabihu zile zile mara nyingi; ambazo haziwezi kabisa kuondoa dhambi. Lakini huyu, alipokwisha kutoa kwa ajili ya dhambi dhabihu moja idumuyo hata milele, aliketi mkono wa kuume wa Mungu; tangu hapo akingojea hata adui zake wawekwe kuwa chini ya miguu yake. Maana kwa toleo moja amewakamilisha hata milele hao wanaotakaswa. Na Roho Mtakatifu naye amshuhudia; kwa maana, baada ya kusema, Hili ni agano nitakaloagana nao baada ya siku zile, anena Bwana, Nitatia sheria zangu mioyoni mwao, Na katika nia zao nitaziandika; ndipo anenapo, Dhambi zao na uasi wao sitaukumbuka tena kabisa. Basi, ondoleo la hayo likiwapo, hapana toleo tena kwa ajili ya dhambi.
Waebrania 10:1-18 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Sheria ni kivuli tu cha mambo mema yajayo, wala si uhalisi wa mambo yenyewe. Kwa sababu hii, haiwezekani kamwe kwa njia ya dhabihu zitolewazo mwaka hadi mwaka kuwakamilisha wale wanaokaribia ili kuabudu. Kama dhabihu hizo zingeweza kuwakamilisha, hazingeendelea kutolewa tena. Kwa kuwa hao waabuduo wangekuwa wametakaswa mara moja tu, wala wasingejiona tena kuwa na dhambi. Lakini zile dhabihu zilikuwa ukumbusho wa dhambi kila mwaka, kwa sababu haiwezekani damu ya mafahali na mbuzi kuondoa dhambi. Kwa hiyo, Kristo alipokuja duniani, alisema: “Dhabihu na sadaka hukuzitaka, bali mwili uliniandalia; sadaka za kuteketezwa na za dhambi hukupendezwa nazo. Ndipo niliposema, ‘Mimi hapa, nimekuja, imeandikwa kunihusu katika kitabu: Nimekuja kuyafanya mapenzi yako, Ee Mungu.’ ” Kwanza alisema, “Dhabihu na sadaka, sadaka za kuteketezwa na za dhambi hukuzitaka, wala hukupendezwa nazo” (ingawa sheria iliagiza zitolewe). Kisha akasema “Mimi hapa, nimekuja kuyafanya mapenzi yako.” Aondoa lile Agano la kwanza ili kuimarisha la pili. Katika mapenzi hayo sisi tumetakaswa na kufanywa watakatifu kwa njia ya sadaka ya mwili wa Yesu Kristo alioutoa mara moja tu. Kila kuhani husimama siku kwa siku akifanya huduma yake ya ibada, na kutoa tena na tena dhabihu zile zile ambazo haziwezi kamwe kuondoa dhambi. Lakini huyu kuhani akiisha kutoa dhabihu moja kwa ajili ya dhambi kwa wakati wote, aliketi mkono wa kuume wa Mungu. Tangu wakati huo anangoja mpaka adui zake wawekwe chini ya miguu yake, kwa sababu kwa dhabihu moja amewafanya kuwa wakamilifu milele wale wote wanaotakaswa. Pia Roho Mtakatifu anatushuhudia kuhusu jambo hili. Kwanza anasema: “Hili ndilo Agano nitakalofanya nao baada ya siku hizo, asema Bwana. Nitaziweka sheria zangu mioyoni mwao, na kuziandika katika nia zao.” Kisha aongeza kusema: “Dhambi zao na kutokutii kwao sitakumbuka tena.” Basi haya yakiisha kusamehewa, hakuna tena dhabihu yoyote inayotolewa kwa ajili ya dhambi.