Hagai 1:1-11
Hagai 1:1-11 Biblia Habari Njema (BHN)
Siku ya kwanza ya mwezi wa sita mwaka wa pili wa utawala wa mfalme Dario wa Persia, Mwenyezi-Mungu alimpa Hagai ujumbe aupeleke kwa Zerubabeli mwana wa Shealtieli, mkuu wa Yuda, na kuhani mkuu Yoshua mwana wa Yehosadaki. Hagai akasema: “Mwenyezi-Mungu wa majeshi asema hivi: Watu hawa wanasema kwamba wakati wa kulijenga upya hekalu langu haujafika.” Lakini Mwenyezi-Mungu ameniambia mimi nabii Hagai, “Je, ni sawa kwenu kukaa katika majumba yenu ya fahari hali hekalu langu ni magofu matupu?” Sasa, asema hivi Mwenyezi-Mungu: “Fikirini kama mnafanya sawa! Nyinyi mmepanda mbegu kwa wingi, lakini mmevuna kidogo; mnakula, lakini hamshibi; mnakunywa divai, lakini hamtosheki; mnavaa nguo, lakini bado mnasikia baridi; mfanyakazi mshahara wake huwa kama umetumbukizwa katika mfuko uliotoboka.” Mwenyezi-Mungu wa majeshi asema hivi: “Fikirini kama mnafanya sawa! Sasa, basi, nendeni milimani mkalete miti, mlijenge upya hilo hekalu, nipate kulifurahia na kutukuzwa. “Mlitazamia mavuno mengi, lakini mlipata kidogo tu. Na mlipoyaleta nyumbani, niliyapeperusha mbali. Kwa nini? Kwa sababu hekalu langu ni magofu matupu hali kila mmoja wenu anashughulikia nyumba yake. Ndio maana mbingu zimeacha kunyesha mvua, nayo ardhi haioteshi mavuno. Nimeleta ukame nchini, ukaathiri vilima na mashamba ya nafaka, mashamba ya mizabibu na mashamba ya mizeituni na kila mmea, watu na wanyama, na chochote mlichotolea jasho.”
Hagai 1:1-11 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Katika mwaka wa pili wa utawala wa mfalme Dario, mwezi wa sita, siku ya kwanza ya mwezi, neno la BWANA lilimjia Zerubabeli, mwana wa Shealtieli, mtawala wa Yuda, na Yoshua, mwana wa Yehosadaki, kuhani mkuu, kwa kinywa chake nabii Hagai, kusema, BWANA wa majeshi asema hivi, ya kwamba, Watu hawa husema, Wakati wa kuijenga upya nyumba ya BWANA haujafika. Ndipo neno la BWANA lilikuja kwa kinywa cha nabii Hagai, kusema, Je! Huu ndio wakati wa ninyi kukaa katika nyumba zenye mapambo ya mbao, iwapo nyumba hii inakaa hali ya kuharibika? Basi sasa, BWANA wa majeshi asema hivi, Zitafakarini njia zenu. Mmepanda mbegu nyingi mkavuna kidogo; mnakula lakini hamshibi; mnakunywa lakini hamtosheki na vinywaji; mnajivika nguo lakini hampati joto; na yeye apataye mshahara apata mshahara ili kuutia katika mfuko uliotobokatoboka. BWANA wa majeshi asema hivi, Zitafakarini njia zenu. Pandeni milimani, mkalete miti, mkaijenge nyumba; nami nitaifurahia, nami nitatukuzwa, asema BWANA. Mlitazamia vingi, kumbe vikatokea vichache; tena mlipovileta nyumbani nikavipeperusha mbali. Ni kwa sababu gani? Asema BWANA wa majeshi. Ni kwa sababu yumba yangu imebaki kuwa gofu la nyumba, wakati ambapo kila mmoja wenu anakimbilia nyumbani kwake. Basi, kwa ajili yenu mbingu zimezuiliwa zisitoe umande, nayo nchi imezuiliwa isitoe matunda yake. Nami nikaita wakati wa joto uje juu ya nchi, na juu ya milima, na juu ya nafaka, na juu ya divai mpya, na juu ya mafuta, na juu ya kila kitu itoacho nchi, na juu ya wanadamu, na juu ya wanyama, na juu ya kazi zote za mikono.
Hagai 1:1-11 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Katika mwaka wa pili wa Dario mfalme, mwezi wa sita, siku ya kwanza ya mwezi, neno la BWANA lilimjia Zerubabeli, mwana wa Shealtieli, liwali wa Yuda, na Yoshua, mwana wa Yehosadaki, kuhani mkuu, kwa kinywa chake Hagai nabii, kusema, BWANA wa majeshi asema hivi, ya kwamba, Watu hawa husema, Huu sio wakati utupasao kuja, huu sio wakati wa kujenga nyumba ya BWANA. Ndipo neno la BWANA lilikuja kwa kinywa cha nabii Hagai, kusema, Je! Huu ndio wakati wa ninyi kukaa katika nyumba zenye mapambo ya mbao, iwapo nyumba hii inakaa hali ya kuharibika? Basi sasa, BWANA wa majeshi asema hivi, Zitafakarini njia zenu. Mmepanda mbegu nyingi mkavuna kidogo; mnakula lakini hamshibi; mnakunywa lakini hamkujazwa na vinywaji; mnajivika nguo lakini hapana aonaye moto; na yeye apataye mshahara apata mshahara ili kuutia katika mfuko uliotoboka-toboka. BWANA wa majeshi asema hivi, Zitafakarini njia zenu. Pandeni milimani, mkalete miti, mkaijenge nyumba; nami nitaifurahia, nami nitatukuzwa, asema BWANA. Mlitazamia vingi, kumbe vikatokea vichache; tena mlipovileta nyumbani nikavipeperusha. Ni kwa sababu gani? Asema BWANA wa majeshi. Ni kwa sababu ya nyumba yangu inayokaa hali ya kuharibika, wakati ambapo ninyi mnakimbilia kila mtu nyumbani kwake. Basi, kwa ajili yenu mbingu zimezuiliwa zisitoe umande, nayo nchi imezuiliwa isitoe matunda yake. Nami nikaita wakati wa joto uje juu ya nchi, na juu ya milima, na juu ya nafaka, na juu ya divai mpya, na juu ya mafuta, na juu ya kila kitu itoacho nchi, na juu ya wanadamu, na juu ya wanyama, na juu ya kazi zote za mikono.
Hagai 1:1-11 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Katika mwaka wa pili wa utawala wa Mfalme Dario wa Uajemi, katika siku ya kwanza ya mwezi wa sita, neno la BWANA lilikuja kupitia kwa nabii Hagai kwenda kwa Zerubabeli mwana wa Shealtieli, mtawala wa Yuda na kwa Yoshua mwana wa kuhani mkuu Yehosadaki: Hivi ndivyo asemavyo BWANA Mwenye Nguvu Zote: “Hawa watu husema, ‘Wakati haujawadia wa kujenga nyumba ya BWANA.’ ” Kisha neno la BWANA likaja kupitia kwa nabii Hagai: “Je, ni wakati wenu ninyi wa kuishi katika nyumba zenu zilizojengwa vizuri, wakati hii nyumba ikibaki, gofu?” Sasa hili ndilo asemalo BWANA Mwenye Nguvu Zote: “Zitafakarini vyema njia zenu. Mmepanda vingi, lakini mmevuna haba. Mnakula lakini hamshibi, mnakunywa, lakini hamtosheki. Mnavaa nguo, lakini hamsikii joto. Mnapata mishahara, lakini inatoweka kama imewekwa kwenye mfuko uliotobokatoboka.” Hili ndilo asemalo BWANA Mwenye Nguvu Zote: “Zitafakarini vyema njia zenu. Pandeni milimani mkalete miti na kujenga nyumba, ili nipate kuifurahia, na nitukuzwe,” asema BWANA. “Mlitarajia mengi, kumbe, yametokea kidogo. Ulichokileta nyumbani nilikipeperusha. Kwa nini?” asema BWANA Mwenye Nguvu Zote. “Ni kwa sababu ya nyumba yangu, inayobaki katika hali ya magofu, wakati kila mmoja wenu anajishughulisha na nyumba yake mwenyewe. Kwa hiyo, kwa sababu yenu mbingu zimezuia umande wake na ardhi mavuno yake. Niliita ukame mashambani na milimani, kwenye nafaka, mvinyo mpya, mafuta pamoja na chochote kinachozalishwa na ardhi, juu ya watu na ngʼombe, pamoja na kazi za mikono yenu.”