Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Hagai 1:1-11

Hagai 1:1-11 NEN

Katika mwaka wa pili wa utawala wa Mfalme Dario wa Uajemi, katika siku ya kwanza ya mwezi wa sita, neno la BWANA lilikuja kupitia kwa nabii Hagai kwenda kwa Zerubabeli mwana wa Shealtieli, mtawala wa Yuda na kwa Yoshua mwana wa kuhani mkuu Yehosadaki: Hivi ndivyo asemavyo BWANA Mwenye Nguvu Zote: “Hawa watu husema, ‘Wakati haujawadia wa kujenga nyumba ya BWANA.’ ” Kisha neno la BWANA likaja kupitia kwa nabii Hagai: “Je, ni wakati wenu ninyi wa kuishi katika nyumba zenu zilizojengwa vizuri, wakati hii nyumba ikibaki, gofu?” Sasa hili ndilo asemalo BWANA Mwenye Nguvu Zote: “Zitafakarini vyema njia zenu. Mmepanda vingi, lakini mmevuna haba. Mnakula lakini hamshibi, mnakunywa, lakini hamtosheki. Mnavaa nguo, lakini hamsikii joto. Mnapata mishahara, lakini inatoweka kama imewekwa kwenye mfuko uliotobokatoboka.” Hili ndilo asemalo BWANA Mwenye Nguvu Zote: “Zitafakarini vyema njia zenu. Pandeni milimani mkalete miti na kujenga nyumba, ili nipate kuifurahia, na nitukuzwe,” asema BWANA. “Mlitarajia mengi, kumbe, yametokea kidogo. Ulichokileta nyumbani nilikipeperusha. Kwa nini?” asema BWANA Mwenye Nguvu Zote. “Ni kwa sababu ya nyumba yangu, inayobaki katika hali ya magofu, wakati kila mmoja wenu anajishughulisha na nyumba yake mwenyewe. Kwa hiyo, kwa sababu yenu mbingu zimezuia umande wake na ardhi mavuno yake. Niliita ukame mashambani na milimani, kwenye nafaka, mvinyo mpya, mafuta pamoja na chochote kinachozalishwa na ardhi, juu ya watu na ngʼombe, pamoja na kazi za mikono yenu.”