Mwanzo 7:13-24
Mwanzo 7:13-24 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Siku ile ile Nuhu akaingia katika safina, yeye, na Shemu na Hamu na Yafethi, wana wa Nuhu, na mkewe Nuhu, na wake watatu wa wanawe pamoja naye; wao na kila mnyama wa mwitu kwa jinsi yake, na kila mnyama wa kufugwa kwa jinsi yake, na kila kitambaacho, chenye kutambaa juu ya nchi, kwa jinsi yake, na kirukacho kwa jinsi yake, kila ndege wa namna yo yote. Waliingia katika safina alimo Nuhu, wawili wawili, wa kila chenye mwili kilicho na pumzi ya uhai ndani yake. Na walioingia, waliingia mume na mke, wa kila kitu chenye mwili, kama vile alivyomwamuru Mungu; BWANA akamfungia. Ile gharika ilikuwako juu ya nchi siku arobaini; nayo maji yakazidi, yakaieleza safina, ikaelea juu ya nchi. Maji yakapata nguvu, yakazidi sana juu ya nchi; na ile safina ikaelea juu ya uso wa maji. Maji yakapata nguvu sana sana juu ya nchi; na milima mirefu yote iliyokuwako chini ya mbingu ikafunikizwa. Maji yakapata nguvu, hata ikafunikwa milima kiasi cha mikono kumi na mitano. Wakafa wote wenye mwili waendao juu ya nchi, na ndege, na wanyama wa kufugwa, na kila mnyama wa mwitu, na kila kitambaacho chenye kutambaa juu ya nchi, na kila mwanadamu; kila kitu chenye pumzi ya roho ya uhai puani mwake kikafa, kila kilichokuwako katika nchi kavu. Kila kilicho hai juu ya uso wa nchi kikafutiliwa mbali tangu mwanadamu hata mnyama wa kufugwa, na kitambaacho, na ndege wa angani; vilifutiliwa mbali katika nchi, akabaki Nuhu tu, na hao walio pamoja naye katika safina. Maji yakapata nguvu juu ya nchi siku mia na hamsini.
Mwanzo 7:13-24 Biblia Habari Njema (BHN)
Siku hiyohiyo mvua ilipoanza kunyesha, Noa, mkewe na wanawe, Shemu, Hamu na Yafethi, pamoja na wake zao, waliingia ndani ya safina. Waliingia wao wenyewe pamoja na aina zote za wanyama wa porini, wanyama wafugwao, wanyama watambaao na ndege wa kila aina. Waliingia ndani ya safina pamoja na Noa wiliwawili wa kila aina ya viumbe hai. Kila aina yao waliingia, dume na jike, kama Mungu alivyomwamuru Noa. Kisha, Mwenyezi-Mungu akaufunga mlango wa safina nyuma yake Noa. Gharika ilidumu nchini kwa muda wa siku arubaini. Maji yakaongezeka na kuiinua safina, ikaelea juu ya ardhi. Maji yakaendelea kuongezeka zaidi nchini na safina ikaelea juu yake. Maji hayo yakawa mengi sana juu ya nchi, yakaifunika milima yote mirefu katika nchi. Yaliongezeka hata kuifunika milima kiasi cha mita saba na nusu. Viumbe wote hai katika nchi wakafa. Ndege, wanyama wa kufugwa, wanyama wa porini, makundi ya viumbe wote katika nchi kavu na wanadamu wote; naam, kila kiumbe hai katika nchi kavu kilikufa. Mungu akaangamiza kila kiumbe kilichokuwa hai duniani: Binadamu, wanyama, viumbe vitambaavyo na ndege wa angani. Vyote viliangamizwa duniani. Noa tu ndiye aliyesalimika na wale waliokuwa pamoja naye ndani ya safina. Maji hayo yalidumu katika nchi siku 150.
Mwanzo 7:13-24 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Siku ile ile Nuhu akaingia katika safina, yeye, na Shemu na Hamu na Yafethi, wana wa Nuhu, na mkewe Nuhu, na wake watatu wa wanawe pamoja naye; wao na kila mnyama wa mwitu kwa jinsi yake, na kila mnyama wa kufugwa kwa jinsi yake, na kila kitambaacho, chenye kutambaa juu ya nchi, kwa jinsi yake, na kirukacho kwa jinsi yake, kila ndege wa namna yoyote. Waliingia katika safina alimokuwa Nuhu, wawili wawili, wa kila chenye mwili kilicho na pumzi ya uhai ndani yake. Na walioingia, waliingia wa kike na wa kiume, wa kila kitu chenye mwili, kama vile alivyomwamuru Mungu; BWANA akamfungia. Ile gharika ilikuwako juu ya nchi siku arubaini; nayo maji yakazidi, yakaifanya safina ielee, ikaelea juu ya nchi. Maji yakaongezeka zaidi juu ya nchi; na safina ikaelea juu ya uso wa maji. Maji yakazidi kuongezeka sana sana juu ya nchi; hata milima mirefu yote iliyokuwako chini ya mbingu ikafunikwa. Maji yakaongezeka hata milima ikafunikwa kiasi cha dhiraa kumi na tano. Wakafa watu wote waendao juu ya nchi, na ndege, na wanyama wa kufugwa, na kila mnyama wa mwitu, na kila kitambaacho chenye kutambaa juu ya nchi, na kila mwanadamu; kila kitu chenye pumzi ya roho ya uhai puani mwake kikafa, kila kilichokuwako katika nchi kavu. Kila kilichokuwa hai juu ya uso wa nchi kikafutiliwa mbali; mwanadamu, wanyama wa kufugwa, kitambaacho na ndege wa angani; vilifutiliwa mbali katika nchi, akabaki Nuhu tu, na hao waliokuwa pamoja naye katika safina. Maji yakapata nguvu juu ya nchi siku mia na hamsini.
Mwanzo 7:13-24 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Siku hiyo Noa, na mkewe, na wanawe Shemu, Hamu na Yafethi pamoja na wake zao wakaingia katika ile safina. Nao walikuwa pamoja na kila mnyama wa mwituni kufuatana na aina yake, wanyama wote wafugwao kufuatana na aina zao, kila kiumbe kitambaacho juu ya ardhi kwa aina yake, na kila ndege kufuatana na aina yake, naam kila kiumbe chenye mabawa. Viumbe vyote vyenye pumzi ya uhai ndani yake vikaja kwa Noa viwili viwili, vikaingia katika safina. Wanyama walioingia katika safina walikuwa wa kiume na wa kike, wa kila kiumbe chenye uhai kama Mungu alivyomwamuru Noa, ndipo BWANA akamfungia ndani. Kwa siku arobaini mafuriko yaliendelea kujaa duniani na maji yalivyozidi kuongezeka, yaliinua safina juu sana kutoka kwenye uso wa nchi. Maji yakajaa na kuongezeka sana juu ya nchi, na safina ikaelea juu ya uso wa maji. Maji yakazidi kujaa juu ya nchi, yakaifunika milima yote mirefu chini ya mbingu yote. Maji yakaendelea kujaa yakaifunika milima kwa kina cha zaidi ya dhiraa kumi na tano. Kila kiumbe hai kitambaacho juu ya nchi kikaangamia: Ndege, wanyama wa kufugwa, wanyama pori, viumbe vyote juu ya nchi na wanadamu wote. Kila kiumbe juu ya nchi kavu chenye pumzi ya uhai kikafa. Kila kitu chenye uhai juu ya uso wa nchi kilifutiliwa mbali, watu, wanyama, viumbe vitambaavyo na ndege warukao angani wakafutiliwa mbali toka duniani. Waliobaki ni Noa peke yake na wale waliokuwa pamoja naye ndani ya safina. Maji yakaifunika dunia kwa siku 150.