Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mwanzo 7:13-24

Mwanzo 7:13-24 NEN

Siku hiyo Noa, na mkewe, na wanawe Shemu, Hamu na Yafethi pamoja na wake zao wakaingia katika ile safina. Nao walikuwa pamoja na kila mnyama wa mwituni kufuatana na aina yake, wanyama wote wafugwao kufuatana na aina zao, kila kiumbe kitambaacho juu ya ardhi kwa aina yake, na kila ndege kufuatana na aina yake, naam kila kiumbe chenye mabawa. Viumbe vyote vyenye pumzi ya uhai ndani yake vikaja kwa Noa viwili viwili, vikaingia katika safina. Wanyama walioingia katika safina walikuwa wa kiume na wa kike, wa kila kiumbe chenye uhai kama Mungu alivyomwamuru Noa, ndipo BWANA akamfungia ndani. Kwa siku arobaini mafuriko yaliendelea kujaa duniani na maji yalivyozidi kuongezeka, yaliinua safina juu sana kutoka kwenye uso wa nchi. Maji yakajaa na kuongezeka sana juu ya nchi, na safina ikaelea juu ya uso wa maji. Maji yakazidi kujaa juu ya nchi, yakaifunika milima yote mirefu chini ya mbingu yote. Maji yakaendelea kujaa yakaifunika milima kwa kina cha zaidi ya dhiraa kumi na tano. Kila kiumbe hai kitambaacho juu ya nchi kikaangamia: Ndege, wanyama wa kufugwa, wanyama pori, viumbe vyote juu ya nchi na wanadamu wote. Kila kiumbe juu ya nchi kavu chenye pumzi ya uhai kikafa. Kila kitu chenye uhai juu ya uso wa nchi kilifutiliwa mbali, watu, wanyama, viumbe vitambaavyo na ndege warukao angani wakafutiliwa mbali toka duniani. Waliobaki ni Noa peke yake na wale waliokuwa pamoja naye ndani ya safina. Maji yakaifunika dunia kwa siku 150.

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na Mwanzo 7:13-24