Mwanzo 43:23-28
Mwanzo 43:23-28 Biblia Habari Njema (BHN)
Yule msimamizi akawajibu, “Msiwe na wasiwasi, wala msiogope. Bila shaka Mungu wenu, Mungu wa baba yenu, ndiye aliyewarudishieni fedha katika magunia yenu. Mimi nilipokea fedha yenu.” Kisha akawaletea Simeoni, ndugu yao. Huyo msimamizi alipowakaribisha nyumbani kwa Yosefu, akawapa maji ya kunawa miguu yao, na punda wao akawalisha. Nao wakatayarisha zawadi zao za kumpa Yosefu, kwa sababu walisikia kuwa watakula pamoja naye. Yosefu, aliporudi nyumbani, wakamletea zile zawadi walizokuwa nazo, wakamwinamia kwa heshima. Yosefu akawauliza habari zao na kusema, “Mlinisimulia habari za mzee, baba yenu. Je, hajambo? Angali hai?” Wakamjibu, “Mtumishi wako, baba yetu, hajambo na angali hai.” Kisha wakainama kwa heshima.
Mwanzo 43:23-28 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Akawaambia, Amani iwe kwenu, msiogope; Mungu wenu, naye ni Mungu wa baba yenu, amewapa akiba katika magunia yenu; fedha zenu zilinifikia. Kisha akawatolea Simeoni kwao. Mtu yule akawaleta wale watu nyumbani mwa Yusufu, akawapa maji, wakanawa miguu, akawapa punda wao chakula. Wakaiweka tayari ile zawadi hadi atakapokuja Yusufu adhuhuri, maana wamesikia ya kwamba watakula chakula huko. Alipokuja Yusufu nyumbani, wakamletea ile zawadi iliyokuwa mikononi mwao nyumbani mwake, wakamwinamia mpaka chini. Akawaulizia hali yao, akasema, Je! Baba yenu, yule mzee mliyemnena, hajambo? Angali hai? Wakasema, Mtumishi wako baba yetu hajambo, angali hai; wakainama, wakasujudu.
Mwanzo 43:23-28 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Akawaambia, Amani iwe kwenu, msiogope; Mungu wenu, naye ni Mungu wa baba yenu, amewapa akiba katika magunia yenu; fedha zenu ziliniwasilia. Kisha akawatolea Simeoni. Mtu yule akawaleta wale watu nyumbani mwa Yusufu, akawapa maji, wakatawadha miguu, akawapa punda zao chakula. Wakaiweka tayari ile zawadi hata atakapokuja Yusufu adhuhuri, maana wamesikia ya kwamba watakula chakula huko. Alipokuja Yusufu nyumbani, wakamletea ile zawadi iliyokuwa mikononi mwao nyumbani mwake, wakamwinamia mpaka nchi. Akawaulizia hali yao, akasema, Je! Baba yenu, yule mzee mliyemnena, hajambo? Angali hai? Wakasema, Mtumwa wako baba yetu hajambo, angali hai; wakainama, wakasujudu.
Mwanzo 43:23-28 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Akawaambia, “Vema, msiogope. Mungu wenu, Mungu wa baba yenu, amewapa ninyi hazina katika magunia yenu; mimi nilipokea fedha yenu.” Ndipo akawaletea Simeoni. Msimamizi akawapeleka wale watu katika nyumba ya Yosefu, akawapa maji ya kunawa miguu na kuwapa punda wao majani. Wakaandaa zawadi zao ili wampe Yosefu wakati atakapofika adhuhuri, kwa kuwa walikuwa wamesikia kwamba watakula chakula huko. Yosefu alipokuja nyumbani, walimkabidhi zile zawadi walizokuwa nazo, ambazo walikuwa wamezileta mle nyumbani, nao wakamsujudia hadi nchi. Akawauliza kuhusu hali yao, kisha akawaambia, “Yule baba yenu mzee mliyeniambia habari zake, yu hali gani? Je, bado yu hai?” Wakamjibu, “Mtumishi wako baba yetu bado anaishi na ni mzima.” Kisha wakainama chini kumpa heshima.