Mwanzo 43:15-23
Mwanzo 43:15-23 Biblia Habari Njema (BHN)
Hapo, wakachukua zile zawadi, na fedha mara mbili ya zile za awali, wakaenda Misri pamoja na ndugu yao Benyamini. Walipowasili, wakaenda na kusimama mbele ya Yosefu. Yosefu alipomwona Benyamini pamoja nao, akamwambia msimamizi wa nyumba yake, “Wapeleke watu hawa nyumbani, umchinje mnyama mmoja na kumtengeneza vizuri, maana watu hawa watakula nami chakula cha mchana.” Msimamizi huyo akafanya kama alivyoagizwa: Akawapeleka wale wageni nyumbani kwa Yosefu. Walipoona wamepelekwa nyumbani kwa Yosefu, wakashikwa na hofu, wakasema wao kwa wao, “Tumeletwa huku kwa sababu ya ile fedha tuliyorudishiwa katika magunia yetu tulipokuja safari ya kwanza ili apate kisingizio cha kutushambulia ghafla na kutunyanganya punda wetu na kutufanya watumwa wake.” Kwa hiyo wakamwendea yule msimamizi wa nyumba ya Yosefu wakaongea naye wakiwa mlangoni, wakamwambia, “Samahani, bwana! Sisi tulikuja hapa mara ya kwanza kununua chakula. Tulipofika mahali pa kulala wageni huko njiani, tulifungua magunia yetu, tukashangaa kukuta fedha ya kila mmoja wetu mdomoni mwa gunia lake bila kuguswa. Sasa tumeirudisha fedha hiyo. Tumeleta na fedha nyingine kununulia chakula. Hatujui ni nani aliyeweka fedha yetu katika magunia yetu.” Yule msimamizi akawajibu, “Msiwe na wasiwasi, wala msiogope. Bila shaka Mungu wenu, Mungu wa baba yenu, ndiye aliyewarudishieni fedha katika magunia yenu. Mimi nilipokea fedha yenu.” Kisha akawaletea Simeoni, ndugu yao.
Mwanzo 43:15-23 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Basi hao watu wakatwaa zawadi ile, wakatwaa na fedha maradufu mikononi mwao, na Benyamini; wakaondoka, wakashuka mpaka Misri, wakasimama mbele ya Yusufu. Naye Yusufu alipomwona Benyamini pamoja nao, akamwambia msimamizi wa nyumba yake, Uwalete watu hawa nyumbani, ukachinje mnyama na kuwaandalia, maana watu hawa watakula pamoja nami adhuhuri. Yule mtu akafanya kama Yusufu alivyomwambia Naye akawaleta watu hao nyumbani mwa Yusufu. Lakini watu hao wakaogopa kwa sababu wameletwa nyumbani mwa Yusufu, wakasema, Kwa sababu ya fedha zile zilizorudishwa katika magunia yetu mara ya kwanza tumeletwa humu; apate kutushitaki, na kutushika, atutwae sisi kuwa watumwa, na punda wetu. Wakamkaribia yule msimamizi wa nyumba ya Yusufu, wakasema naye mlangoni pa nyumba. Wakamwambia, Tazama, bwana, kweli tulishuka mara ya kwanza ili tununue chakula. Ikawa, tulipofika nyumba ya wageni, tukafungua magunia yetu, kumbe! Fedha za kila mtu zilikuwako kinywani mwa gunia lake, fedha zetu kwa uzani wake kamili; nasi tumezileta tena mikononi mwetu. Nasi tumeleta fedha nyingine mikononi mwetu ili tununue chakula; hatujui ni nani aliyezitia fedha zetu katika magunia yetu. Akawaambia, Amani iwe kwenu, msiogope; Mungu wenu, naye ni Mungu wa baba yenu, amewapa akiba katika magunia yenu; fedha zenu zilinifikia. Kisha akawatolea Simeoni kwao.
Mwanzo 43:15-23 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Basi hao watu wakatwaa zawadi ile, wakatwaa na fedha maradufu mikononi mwao, na Benyamini; wakaondoka, wakashuka mpaka Misri, wakasimama mbele ya Yusufu. Naye Yusufu alipomwona Benyamini pamoja nao, akamwambia msimamizi wa nyumba yake, Uwalete watu hawa nyumbani, ukachinje na kuandalia, maana watu hawa watakula pamoja nami adhuhuri. Yule mtu akafanya kama Yusufu alivyomwambia Naye akawaleta watu hao nyumbani mwa Yusufu. Lakini watu hao wakaogopa kwa sababu wameletwa nyumbani mwa Yusufu, wakasema, Kwa sababu ya fedha zile zilizorudishwa katika magunia yetu mara ya kwanza tumeletwa humu; apate kutushitaki, na kutuangukia, atutwae sisi kuwa watumwa, na punda zetu. Wakamkaribia yule msimamizi wa nyumba ya Yusufu, wakasema naye mlangoni pa nyumba. Wakamwambia, Tazama, bwana, kweli tulishuka mara ya kwanza ili tununue chakula. Ikawa, tulipofika nyumba ya wageni, tukafungua magunia yetu, kumbe! Fedha za kila mtu zilikuwako kinywani mwa gunia lake, fedha zetu kwa uzani wake kamili; nasi tumezileta tena mikononi mwetu. Nasi tumeleta fedha nyingine mikononi mwetu ili tununue chakula; hatujui ni nani aliyezitia fedha zetu katika magunia yetu. Akawaambia, Amani iwe kwenu, msiogope; Mungu wenu, naye ni Mungu wa baba yenu, amewapa akiba katika magunia yenu; fedha zenu ziliniwasilia. Kisha akawatolea Simeoni.
Mwanzo 43:15-23 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)
Basi hao watu wakazichukua zile zawadi na zile fedha mara mbili pamoja na Benyamini. Wakafanya haraka kwenda Misri na wakajionesha kwa Yusufu. Yusufu alipomwona Benyamini pamoja nao, akamwambia msimamizi wa nyumba yake, “Wachukue watu hawa nyumbani mwangu, mchinje mnyama na kuandalia chakula, kwa kuwa watakula chakula cha mchana pamoja nami.” Msimamizi akafanya kama Yusufu alivyomwambia na akawachukua wale watu nyumbani mwa Yusufu. Basi watu hao wakaogopa walipopelekwa nyumbani mwa Yusufu. Wakafikiri, “Tumeletwa hapa kwa ajili ya zile fedha zilizorudishwa katika magunia yetu mara ile ya kwanza. Anataka kutushambulia na kutushinda, atuchukue sisi kama watumwa, na atwae hawa punda wetu.” Hivyo wakamwendea msimamizi wa nyumba wa Yusufu na kuzungumza naye kwenye ingilio la nyumba. Wakasema, “Tafadhali bwana, tulikuja hapa mara ya kwanza kununua chakula. Lakini mahali pale tulipotua wakati wa jioni tulifungua magunia yetu, na kila mmoja wetu akakuta fedha zake katika gunia lake, kiasi kile kile tulicholeta. Kwa hiyo tumezirudisha. Pia tumeleta fedha nyingine kwa ajili ya kununulia chakula. Hatujui ni nani aliziweka fedha hizo katika magunia yetu.” Akawaambia, “Vema, msiogope. Mungu wenu, Mungu wa baba yenu, amewapa ninyi hazina katika magunia yenu; mimi nilipokea fedha yenu.” Ndipo akawaletea Simeoni.