Mwanzo 43:1-14
Mwanzo 43:1-14 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Njaa ikawa kali katika nchi. Ikawa walipokwisha kula nafaka waliyoileta kutoka Misri, baba yao akawaambia, Rudini huko, mkatununulie chakula kidogo. Yuda akamwambia akisema, Yule mtu alituagizia sana akisema, Hamtaniona uso wangu, ndugu yenu asipokuwa pamoja nanyi. Ukimtuma ndugu yetu pamoja nasi, tutashuka na kukununulia chakula. Ila usipomtuma, hatushuki, maana mtu yule alituambia, Hamtaniona uso wangu, ndugu yenu asipokuwa pamoja nanyi. Israeli akasema, Mbona mmenitendea vibaya hata mkamwarifu mtu yule ya kwamba mna ndugu mwingine? Wakasema, Mtu yule alituhoji sana habari zetu na za jamaa yetu, akisema, Baba yenu angali hai? Mnaye ndugu mwingine? Nasi tukamjibu sawasawa na maswali hayo. Je! Tungaliwezaje kujua ya kwamba atasema, Shukeni pamoja na ndugu yenu? Yuda akamwambia Israeli baba yake, Mtume kijana pamoja nami, tuondoke, tuende zetu, ili tupate kuishi, wala tusife, sisi na wewe na watoto wetu. Mimi nitakuwa mdhamini wake, umtake mkononi mwangu. Nisipomleta tena kwako, na kumweka mbele yako, nitakuwa mwenye hatia mbele yako daima; maana kama hatungalikawia, hakika tungaliisha kurudi mara ya pili. Israeli, baba yao, akawaambia, Kama ndivyo, fanyeni hivi; twaeni tunu za nchi katika vyombo vyenu, mkamchukulie mtu huyo zawadi, zeri kidogo, na asali kidogo, ubani, na manemane, na jozi, na lozi. Mkatwae fedha maradufu mikononi mwenu, na fedha zile zilizorudishwa kinywani mwa magunia yenu zirudisheni mikononi mwenu; labda zilisahauliwa. Mtwaeni na ndugu yenu, mwondoke na kurudi kwa mtu yule. Mungu Mwenyezi na awape rehema usoni pa mtu yule ili awafungulie ndugu yenu huyo mwingine, na Benyamini. Nami nikifiwa na watoto wangu, nimefiwa.
Mwanzo 43:1-14 Biblia Habari Njema (BHN)
Kisha njaa ilizidi kuwa kali katika nchi ya Kanaani. Baada ya kile chakula walichokuwa wamenunua kutoka Misri kumalizika, Yakobo akawaambia wanawe, “Nendeni tena Misri, mkatununulie chakula kidogo.” Lakini Yuda akamwambia baba yake, “Yule mtu alituonya vikali, akisema, ‘Sitawapokea msipokuja na ndugu yenu mdogo.’ Kama utakubali ndugu yetu kwenda pamoja nasi, basi, tutakwenda kukununulia chakula. Lakini iwapo hutakubali aende nasi, basi, hatutakwenda huko, kwani yule mtu alituambia waziwazi, ‘Hamtaniona msipokuja na ndugu yenu mdogo.’” Israeli akasema, “Kwa nini mkanitia taabuni kwa kumwambia huyo mtu kwamba mnaye ndugu mwingine?” Wakamjibu, “Yule mtu alituhoji kwa makini sana kuhusu mambo yetu na jamaa yetu akisema, ‘Je, baba yenu angali hai? Je, mnaye ndugu mwingine?’ Hivyo tulimjibu kulingana na maswali yake. Tungaliwezaje kujua kwamba atatuambia, ‘Mleteni ndugu yenu?’” Yuda akamwambia Israeli, baba yake, “Niruhusu mimi niende naye ili tuondoke mara moja, tuende tukanunue chakula, tusije tukafa njaa pamoja nawe na watoto wetu. Mimi mwenyewe nitakuwa mdhamini wake. Wewe utanidai mimi. Nisipomrudisha ukamwona kwa macho yako mwenyewe, lawama na iwe juu yangu milele. Kama tusingalikawia, tungalikuwa tumekwisha kwenda na kurudi mara mbili.” Hapo Israeli, baba yao, akawaambia, “Haya! Kwa vile ni lazima iwe hivyo basi, fanyeni hivi: Chukueni katika mifuko yenu baadhi ya mazao bora ya nchi yetu, mkampelekee zawadi huyo mkuu. Mchukulieni mafuta kidogo ya mkwaju, asali kidogo, ubani, manemane, kungu na lozi. Chukueni fedha mara mbili ya ile inayohitajika, kwa sababu ni lazima mrudishe fedha ile iliyowekwa midomoni mwa magunia yenu; pengine ilirudishwa kwa makosa. Mchukueni pia ndugu yenu mwende kwa huyo mtu. Mungu Mwenye Nguvu na awajalieni kupata huruma mbele ya mtu huyo, awaachieni yule ndugu yenu mwingine na Benyamini warudi pamoja nanyi. Kwa upande wangu, ikinipasa kufiwa na wanangu basi!”
Mwanzo 43:1-14 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Njaa ikawa nzito katika nchi. Ikawa walipokwisha kula nafaka waliyoileta kutoka Misri, baba yao akawaambia, Rudini huko, mkatununulie chakula kidogo. Yuda akamwambia akisema, Yule mtu alituagizia sana akisema, Hamtaniona uso wangu, ndugu yenu asipokuwa pamoja nanyi. Ukimpeleka ndugu yetu pamoja nasi, tutashuka na kukununulia chakula. Ila usipompeleka, hatushuki, maana mtu yule alituambia, Hamtaniona uso wangu, ndugu yenu asipokuwa pamoja nanyi. Israeli akasema, Mbona mmenitendea vibaya hata mkamwarifu mtu yule ya kwamba mna ndugu mwingine? Wakasema, Mtu yule alituhoji sana habari zetu na za jamaa yetu, akisema, Baba yenu angali hai? Mnaye ndugu mwingine? Nasi tukamjibu sawasawa na maswali hayo. Je! Tuliweza kujua ya kwamba atasema, Shukeni pamoja na ndugu yenu? Yuda akamwambia Israeli babaye, Mpeleke kijana pamoja nami, tuondoke, tuende zetu, ili tupate kuishi, wala tusife, sisi na wewe na watoto wetu. Mimi nitakuwa mdhamini wake, umtake mkononi mwangu. Nisipomleta tena kwako, na kumweka mbele yako, nitakuwa mwenye hatia mbele yako daima; maana kama hatungalikawia, hakika tungaliisha kurudi mara ya pili. Israeli, baba yao, akawaambia, Kama ndivyo, fanyeni hivi; twaeni tunu za nchi katika vyombo vyenu, mkamchukulie mtu huyo zawadi, zeri kidogo, na asali kidogo, ubani, na manemane, na jozi, na lozi. Mkatwae fedha maradufu mikononi mwenu, na fedha zile zilizorudishwa kinywani mwa magunia yenu zirudisheni mikononi mwenu; labda zilisahauliwa. Mtwaeni na ndugu yenu, mwondoke na kurudi kwa mtu yule. Mungu Mwenyezi na awape rehema usoni pa mtu yule ili awafungulie ndugu yenu huyo mwingine, na Benyamini. Nami nikifiwa na watoto wangu, nimefiwa.
Mwanzo 43:1-14 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Wakati huu njaa ilikuwa bado ni kali mno katika nchi. Hivyo wakati walikuwa wamemaliza kula nafaka yote waliyoileta kutoka Misri, Yakobo baba yao akawaambia, “Rudini Misri mkatununulie chakula kingine zaidi.” Lakini Yuda akamwambia, “Mtu yule alituonya kwa msisitizo, ‘Hamtauona uso wangu tena mpaka mje na ndugu yenu.’ Kama utakubali ndugu yetu aende pamoja nasi, tutakwenda kuwanunulia chakula. Lakini ikiwa hutamruhusu aende, hatutakwenda, kwa sababu mtu yule alituambia, ‘Hamtauona uso wangu tena mpaka mje pamoja na ndugu yenu.’ ” Israeli akauliza, “Kwa nini mkaniletea taabu hii kwa kumwambia yule mtu mlikuwa na ndugu mwingine?” Wakamjibu, “Yule mtu alituhoji kwa undani sana habari zetu na za jamaa yetu. Alituuliza, ‘Je, baba yenu bado yungali hai? Je mnaye ndugu mwingine?’ Sisi tulimjibu maswali yake tu. Tungewezaje kujua kwamba angesema, ‘Mleteni mdogo wenu hapa’?” Ndipo Yuda akamwambia baba yake Israeli, “Mtume kijana pamoja nami, nasi tutaondoka mara, ili sisi na wewe pamoja na watoto wetu tuweze kuishi, wala tusife. Mimi mwenyewe nitakuhakikishia usalama wake, mimi mwenyewe nitawajibika kumrudisha. Ikiwa sitamrudisha kwako na kumweka mbele yako, nitakuwa mwenye lawama mbele yako maisha yangu yote. Hakika, kama hatukuchelewa kuondoka, tungekuwa tumekwenda na kurudi mara mbili.” Basi baba yao Israeli akawaambia, “Kama ni lazima iwe hivyo, basi fanyeni hivi: Wekeni baadhi ya mazao bora ya nchi katika mifuko yenu na mpelekeeni yule mtu kama zawadi, zeri kidogo, asali kidogo, vikolezo, manemane, kungu na lozi. Chukueni fedha mara mbili, kwa kuwa mtazirudisha zile fedha zilizowekwa midomoni mwa magunia yenu. Labda ziliwekwa kwa makosa. Mchukueni ndugu yenu pia mrudi kwa huyo mtu mara moja. Naye Mungu Mwenyezi awajalieni rehema mbele ya huyo mtu ili apate kumwachia yule ndugu yenu na Benyamini mweze kurudi pamoja. Kwangu mimi kama nikufiwa nimefiwa.”