Mwanzo 36:1-8
Mwanzo 36:1-8 Biblia Habari Njema (BHN)
Wafuatao ni wazawa wa Esau (yaani Edomu). Esau alioa wake Wakanaani: Ada binti Eloni Mhiti, Oholibama binti Ana, binti Sibeoni, Mhivi, na Basemathi, binti Ishmaeli, dada yake Nebayothi. Ada alimzalia Esau Elifazi, naye Basemathi akamzalia Reueli. Oholibama alimzalia Yeushi, Yalamu na Kora. Hao ndio watoto wa kiume wa Esau ambao wake zake walimzalia alipokaa katika nchi ya Kanaani. Kisha, Esau akawachukua wake zake, watoto wake wa kiume na wa kike, watu wote wa nyumbani mwake, ng'ombe wake, wanyama wake wengine wote na mali yake yote ambayo alikuwa ameipata katika nchi ya Kanaani, akahamia mahali pengine, mbali na nduguye Yakobo. Alifanya hivyo kwa sababu mali zao zilikuwa nyingi hata wasiweze kuishi pamoja. Nchi waliyokaa kama wageni haikuweza kuwatosha kwa sababu ya wingi wa mifugo yao. Kwa hiyo, Esau akaenda kukaa katika nchi ya milima ya Seiri. Jina lingine la Esau ni Edomu.
Mwanzo 36:1-8 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Hivi ndivyo vizazi vya Esau, ndiye Edomu. Esau alitwaa binti za Kanaani, kuwa wakeze; Ada, binti Eloni, Mhiti, na Oholibama, binti Ana, binti Sibeoni, Mhivi; na Basemathi, binti Ishmaeli, nduguye Nebayothi. Ada akamzalia Esau Elifazi; na Basemathi alizaa Reueli. Oholibama alizaa Yeushi, na Yalamu, na Kora. Hao ndio wana wa Esau aliozaliwa katika nchi ya Kanaani. Esau akawatwaa wakeze, na wanawe, na binti zake, na watu wote wa nyumbani mwake, na ng'ombe zake, na wanyama wake wote, na mali yake yote, aliyoyapata katika nchi ya Kanaani; akaenda mpaka nchi iliyo mbali na Yakobo nduguye. Maana mali yao ilikuwa nyingi wasiweze kukaa pamoja, wala nchi ya ugeni haikuweza kuwapokea kwa sababu ya wingi wa mifugo wao. Esau akakaa katika mlima Seiri, Esau ndiye Edomu.
Mwanzo 36:1-8 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Hivi ndivyo vizazi vya Esau, ndiye Edomu. Esau alitwaa binti za Kanaani, kuwa wakeze; Ada, binti Eloni, Mhiti, na Oholibama, binti Ana, binti Sibeoni, Mhivi; na Basemathi, binti Ishmaeli, nduguye Nebayothi. Ada akamzalia Esau Elifazi; na Basemathi alizaa Reueli. Oholibama alizaa Yeushi, na Yalamu, na Kora. Hao ndio wana wa Esau aliozaliwa katika nchi ya Kanaani. Esau akawatwaa wakeze, na wanawe, na binti zake, na watu wote wa nyumbani mwake, na ng’ombe zake, na wanyama wake wote, na mali yake yote, aliyoyapata katika nchi ya Kanaani; akaenda mpaka nchi iliyo mbali na Yakobo nduguye. Maana mali yao yalikuwa mengi wasiweze kukaa pamoja, wala haikuweza nchi ya kusafiri kwao kuwachukua, kwa sababu ya wanyama wao. Esau akakaa katika mlima Seiri, Esau ndiye Edomu.
Mwanzo 36:1-8 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Hivi ndivyo vizazi vya Esau (yaani Edomu). Esau akaoa wake kutoka miongoni mwa wanawake wa Kanaani: Ada binti wa Eloni Mhiti, Oholibama binti wa Ana, mjukuu wa kike wa Sibeoni Mhivi, pia akaoa Basemathi binti wa Ishmaeli, dada yake Nebayothi. Ada akamzalia Esau Elifazi, Basemathi akamzaa Reueli, Oholibama akamzaa Yeushi, Yalamu na Kora. Hawa ndio wana wa Esau waliozaliwa kwake huko Kanaani. Esau akawachukua wake zake, watoto wake wa kiume na wa kike na wote wa nyumbani mwake, mifugo yake pamoja na wanyama wake wengine wote na mali yake yote ambayo alikuwa ameipata akiwa Kanaani, akahamia katika nchi iliyo mbali na Yakobo ndugu yake. Mali zao zilikuwa nyingi sana kiasi kwamba haikuwa rahisi wao kuishi pamoja, nchi waliyokuwa wakiishi isingewatosha wote kwa ajili ya mifugo yao. Kwa hiyo Esau (ambaye ni Edomu) aliishi katika nchi ya kilima huko Seiri.