Mwanzo 36:1-8
Mwanzo 36:1-8 BHN
Wafuatao ni wazawa wa Esau (yaani Edomu). Esau alioa wake Wakanaani: Ada binti Eloni Mhiti, Oholibama binti Ana, binti Sibeoni, Mhivi, na Basemathi, binti Ishmaeli, dada yake Nebayothi. Ada alimzalia Esau Elifazi, naye Basemathi akamzalia Reueli. Oholibama alimzalia Yeushi, Yalamu na Kora. Hao ndio watoto wa kiume wa Esau ambao wake zake walimzalia alipokaa katika nchi ya Kanaani. Kisha, Esau akawachukua wake zake, watoto wake wa kiume na wa kike, watu wote wa nyumbani mwake, ng'ombe wake, wanyama wake wengine wote na mali yake yote ambayo alikuwa ameipata katika nchi ya Kanaani, akahamia mahali pengine, mbali na nduguye Yakobo. Alifanya hivyo kwa sababu mali zao zilikuwa nyingi hata wasiweze kuishi pamoja. Nchi waliyokaa kama wageni haikuweza kuwatosha kwa sababu ya wingi wa mifugo yao. Kwa hiyo, Esau akaenda kukaa katika nchi ya milima ya Seiri. Jina lingine la Esau ni Edomu.