Mwanzo 30:1-14
Mwanzo 30:1-14 Biblia Habari Njema (BHN)
Raheli alipoona kwamba hajamzalia Yakobo watoto, alimwonea wivu Lea, dada yake, akamwambia Yakobo, “Nipatie watoto, la sivyo, nitakufa.” Yakobo akamkasirikia Raheli sana na kumwambia, “Je, mimi nimekuwa badala ya Mungu aliyekuzuia kupata watoto?” Raheli akamjibu, “Mjakazi wangu Bilha yupo. Lala naye ili azae watoto badala yangu, nami pia nipate watoto kutokana naye.” Kwa hiyo Raheli akampa Yakobo mtumishi wake, Bilha, awe mkewe, naye akalala naye. Bilha akapata mimba na kumzalia Yakobo mtoto wa kiume. Raheli akasema, “Mungu amenitendea sawa, amekisikia kilio changu na kunipa mtoto wa kiume.” Akamwita mtoto huyo Dani. Bilha, mjakazi wa Raheli, akapata mimba tena na kumzalia Yakobo mtoto wa pili wa kiume. Hapo Raheli akasema, “Nimepigana miereka mikali na dada yangu, nami nimeshinda.” Kwa hiyo akamwita mtoto huyo Naftali. Lea alipoona ameacha kuzaa, alimtwaa Zilpa, mjakazi wake, na kumpa Yakobo ili awe mkewe. Zilpa akamzalia Yakobo mtoto wa kiume. Lea akasema, “Bahati njema.” Kwa hiyo akamwita mtoto huyo Gadi. Zilpa, mtumishi wa Lea, alimzalia Yakobo mtoto wa pili wa kiume. Lea akasema, “Bahati njema! Sasa wanawake wataniita heri.” Kwa hiyo akamwita mtoto huyo Asheri. Ikawa wakati wa mavuno ya ngano, Reubeni alikwenda shambani na huko akapata tunguja, akamletea mama yake Lea. Raheli akamwambia Lea, “Tafadhali, nipe baadhi ya tunguja za mwanao.”
Mwanzo 30:1-14 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Naye Raheli alipoona ya kuwa hamzalii Yakobo mwana, Raheli alimwonea dada yake wivu. Akamwambia Yakobo, Nipe wana; kama sivyo, nitakufa mimi. Yakobo akamghadhibikia Raheli, akasema, Je! Mimi ni badala ya Mungu, aliyekuzuilia uzao wa mimba? Akasema, Yuko mjakazi wangu, Bilha, uingie kwake ili kwamba azae kwa niaba yangu, nami nipate uzao kwa yeye. Basi akampa Bilha mjakazi wake kuwa mkewe. Yakobo akaingia kwake. Naye Bilha akapata mimba, akamzalia Yakobo mwana. Raheli akasema, Mungu amenipa haki yangu, naye amesikia sauti yangu, akanipa mwana. Kwa hiyo akamwita jina lake Dani. Bilha, mjakazi wa Raheli, akapata mimba tena, akamzalia Yakobo mwana wa pili. Raheli akasema, Kwa mashindano makuu nimeshindana na dada yangu, nikashinda. Akamwita jina lake Naftali. Lea alipoona ya kuwa ameacha kuzaa, alimtwaa Zilpa, mjakazi wake, akampa Yakobo kuwa mkewe. Zilpa, mjakazi wa Lea, akamzalia Yakobo mwana. Lea akasema, Bahati njema! Akamwita jina lake Gadi. Zilpa, mjakazi wa Lea, akamzalia Yakobo mwana wa pili. Lea akasema, Ni heri mimi, maana wanawake wataniita heri. Akamwita jina lake Asheri. Reubeni akaenda siku za mavuno ya ngano akaona tunguja shambani, akazileta kwa Lea mamaye. Ndipo Raheli akamwambia Lea, Nipe mimi baadhi ya tunguja za mwanao.
Mwanzo 30:1-14 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Naye Raheli alipoona ya kuwa hamzalii Yakobo mwana, Raheli alimwonea ndugu yake wivu. Akamwambia Yakobo, Nipe wana; kama sivyo, nitakufa mimi. Yakobo akamghadhibikia Raheli, akasema, Je! Mimi ni badala ya Mungu, aliyekuzuilia uzao wa mimba? Akasema, Yuko mjakazi wangu, Bilha, uingie kwake ili kwamba azae juu ya magoti yangu, nami nipate uzao kwa yeye. Basi akampa Bilha mjakazi wake kuwa mkewe. Yakobo akaingia kwake. Naye Bilha akapata mimba, akamzalia Yakobo mwana. Raheli akasema, Mungu amenipa haki yangu, naye amesikia sauti yangu, akanipa mwana. Kwa hiyo akamwita jina lake Dani. Bilha, mjakazi wa Raheli, akapata mimba tena, akamzalia Yakobo mwana wa pili. Raheli akasema, Kwa mashindano makuu nimeshindana na ndugu yangu, nikashinda. Akamwita jina lake Naftali. Lea alipoona ya kuwa ameacha kuzaa, alimtwaa Zilpa, mjakazi wake, akampa Yakobo kuwa mkewe. Zilpa, mjakazi wa Lea, akamzalia Yakobo mwana. Lea akasema, Bahati njema! Akamwita jina lake Gadi. Zilpa, mjakazi wa Lea, akamzalia Yakobo mwana wa pili. Lea akasema, Ni heri mimi, maana wanawake wataniita heri. Akamwita jina lake Asheri. Reubeni akaenda siku za mavuno ya ngano akaona tunguja kondeni, akazileta kwa Lea mamaye. Ndipo Raheli akamwambia Lea, Nipe mimi baadhi ya tunguja za mwanao.
Mwanzo 30:1-14 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)
Raheli alipoona hamzalii Yakobo watoto, akamwonea dada yake wivu. Hivyo akamwambia Yakobo, “Nipe watoto, la sivyo nitakufa!” Yakobo akamkasirikia, akamwambia, “Je, mimi ni badala ya Mungu, ambaye amekuzuia kuzaa watoto?” Ndipo Raheli akamwambia, “Hapa yupo Bilha, mjakazi wangu. Kutana naye kimwili ili aweze kunizalia watoto, na kupitia kwake mimi pia niweze kuwa na uzao.” Hivyo Raheli akampa Yakobo Bilha awe mke wake. Yakobo akakutana naye kimwili, naye Bilha akapata mimba, akamzalia Yakobo mwana. Ndipo Raheli akasema, “Mungu amenipa haki yangu; amesikiliza maombi yangu na kunipa mwana.” Kwa hiyo akamwita jina Dani. Bilha mjakazi wa Raheli akapata mimba tena, akamzalia Yakobo mwana wa pili. Ndipo Raheli akasema, “Nilikuwa na mashindano makubwa na dada yangu, nami nimeshinda.” Kwa hiyo akamwita jina Naftali. Lea alipoona kuwa amekoma kuzaa watoto, alimchukua mjakazi wake Zilpa, naye akampa Yakobo awe mke wake. Zilpa mjakazi wa Lea akamzalia Yakobo mwana. Ndipo Lea akasema, “Hii ni bahati nzuri aje!” Kwa hiyo akamwita jina Gadi. Mjakazi wa Lea akamzalia Yakobo mwana wa pili. Ndipo Lea akasema, “Nina furaha kiasi gani! Wanawake wataniita furaha.” Kwa hiyo akamwita jina Asheri. Msimu wa kuvuna ngano, Reubeni akaenda shambani akachuma tunguja ambazo alizileta kwa Lea mama yake. Raheli akamwambia Lea, “Tafadhali nakuomba unipe baadhi ya tunguja za mwanao.”