Mwanzo 30:1-14
Mwanzo 30:1-14 NENO
Raheli alipoona hamzalii Yakobo watoto, akamwonea dada yake wivu. Hivyo akamwambia Yakobo, “Nipe watoto, la sivyo nitakufa!” Yakobo akamkasirikia, akamwambia, “Je, mimi ni badala ya Mungu, ambaye amekuzuia kuzaa watoto?” Ndipo Raheli akamwambia, “Hapa yupo Bilha, mjakazi wangu. Kutana naye kimwili ili aweze kunizalia watoto, na kupitia kwake mimi pia niweze kuwa na uzao.” Hivyo Raheli akampa Yakobo Bilha awe mke wake. Yakobo akakutana naye kimwili, naye Bilha akapata mimba, akamzalia Yakobo mwana. Ndipo Raheli akasema, “Mungu amenipa haki yangu; amesikiliza maombi yangu na kunipa mwana.” Kwa hiyo akamwita jina Dani. Bilha mjakazi wa Raheli akapata mimba tena, akamzalia Yakobo mwana wa pili. Ndipo Raheli akasema, “Nilikuwa na mashindano makubwa na dada yangu, nami nimeshinda.” Kwa hiyo akamwita jina Naftali. Lea alipoona kuwa amekoma kuzaa watoto, alimchukua mjakazi wake Zilpa, naye akampa Yakobo awe mke wake. Zilpa mjakazi wa Lea akamzalia Yakobo mwana. Ndipo Lea akasema, “Hii ni bahati nzuri aje!” Kwa hiyo akamwita jina Gadi. Mjakazi wa Lea akamzalia Yakobo mwana wa pili. Ndipo Lea akasema, “Nina furaha kiasi gani! Wanawake wataniita furaha.” Kwa hiyo akamwita jina Asheri. Msimu wa kuvuna ngano, Reubeni akaenda shambani akachuma tunguja ambazo alizileta kwa Lea mama yake. Raheli akamwambia Lea, “Tafadhali nakuomba unipe baadhi ya tunguja za mwanao.”