Mwanzo 27:41-46
Mwanzo 27:41-46 Biblia Habari Njema (BHN)
Basi, Esau akamchukia Yakobo kwa sababu ya baraka aliyokuwa amepewa na baba yake. Esau akawaza, “Siku za matanga ya baba zitakapokwisha, ndipo nitakapomuua ndugu yangu Yakobo.” Lakini Rebeka alipojua nia ya mwanawe mkubwa, akamwita mwanawe mdogo Yakobo, akamwambia, “Jihadhari, ndugu yako Esau anajifariji kwa kupanga kukuua. Kwa hiyo, mwanangu, sikiliza maneno yangu. Ondoka ukimbilie kwa kaka yangu Labani kule Harani. Kaa naye kwa muda, mpaka ghadhabu ya nduguyo itakapopoa. Ghadhabu yake itakapopoa, naye atakapokuwa amesahau uliyomtendea, nitatuma mtu akurudishe. Kwa nini nifiwe na nyinyi wote wawili siku moja?” Rebeka akamwambia Isaka, “Sina raha kabisa maishani kwa sababu ya hawa wanawake wa Esau Wahiti. Ikiwa Yakobo ataoa mmojawapo wa wanawake hawa Wahiti, maisha yangu yana faida gani?”
Mwanzo 27:41-46 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Esau akamchukia Yakobo kwa ajili ya ule mbaraka babaye aliombarikia. Esau akasema moyoni mwake, Siku za kumlilia baba yangu zinakaribia, ndipo nitakapomwua ndugu yangu Yakobo. Rebeka akaarifiwa maneno ya Esau, mwanawe mkubwa. Akapeleka mtu kumwita Yakobo, mwanawe mdogo, akamwambia, Tazama, katika habari zako Esau, ndugu yako, anajifariji moyo wake, maana anakusudia kukuua. Na sasa, mwanangu, sikia sauti yangu, uondoke, ukimbilie kwa Labani, ndugu yangu huko Harani; ukae kwake siku chache, hata ghadhabu ya ndugu yako igeuke; hata ikuondokee ghadhabu ya ndugu yako, akasahau uliyomtenda. Ndipo nitakapopeleka watu kukuchukua kutoka huko. Kwa nini nifiwe nanyi nyote wawili siku moja? Rebeka akamwambia Isaka, Rohoni mwangu sina raha kwa sababu ya hao binti za Hethi. Kama Yakobo akitwaa mke katika binti za Hethi, kama hawa binti za nchi, maisha yangu yatanifaidia nini?
Mwanzo 27:41-46 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Esau akamchukia Yakobo kwa ajili ya ile baraka babaye aliyombariki. Esau akasema moyoni mwake, Siku za kumlilia baba yangu zinakaribia, ndipo nitakapomwua ndugu yangu Yakobo. Rebeka akaarifiwa maneno ya Esau, mwanawe mkubwa. Akatuma mtu kumwita Yakobo, mwanawe mdogo, akamwambia, Tazama, katika habari zake Esau, ndugu yako, anajifariji moyo wake, maana anakusudia kukuua. Na sasa, mwanangu, sikia sauti yangu, uondoke, ukimbilie kwa Labani, ndugu yangu huko Harani; ukae kwake siku chache, hadi ghadhabu ya ndugu yako iishe; hadi ikuondokee ghadhabu ya ndugu yako, akasahau uliyomtenda. Ndipo nitakapotuma watu kukuchukua kutoka huko. Kwa nini nifiwe nanyi nyote wawili siku moja? Rebeka akamwambia Isaka, Rohoni mwangu sina raha kwa sababu ya hao binti za Hethi. Kama Yakobo akitwaa mke katika binti za Hethi, kama hawa binti za nchi, maisha yangu yatanifaidi nini?
Mwanzo 27:41-46 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Esau akawa na kinyongo dhidi ya Yakobo kwa ajili ya baraka ambazo baba yake alikuwa amembariki. Akasema moyoni mwake, “Siku za kuomboleza kwa ajili ya baba yangu zimekaribia, ndipo nitamuua ndugu yangu Yakobo.” Rebeka alipokwisha kuambiwa yale aliyoyasema Esau mwanawe mkubwa, alimwita Yakobo mwanawe mdogo, akamwambia, “Ndugu yako Esau anajifariji kwa wazo la kukuua. Sasa basi, mwanangu, fanya nisemalo: Kimbilia haraka kwa Labani ndugu yangu kule Harani. Ukae naye kwa muda mpaka ghadhabu ya ndugu yako itulie. Wakati ndugu yako atakapokuwa hana hasira nawe tena na amesahau uliyomtendea, nitakupelekea ujumbe urudi. Kwa nini niwapoteze wote wawili kwa siku moja?” Kisha Rebeka akamwambia Isaki, “Nimechukia kuishi kwa sababu ya hawa wanawake wa Kihiti. Ikiwa Yakobo ataoa mke miongoni mwa wanawake wa nchi hii, wanawake wa Kihiti kama hawa, sitakuwa na faida kuendelea kuishi.”