Mwanzo 27:1-17
Mwanzo 27:1-17 Biblia Habari Njema (BHN)
Isaka alikuwa amezeeka na macho yake yalikuwa hayaoni. Basi, alimwita Esau mwanawe mkubwa, akamwambia, “Mwanangu!” Naye akaitika “Naam baba, nasikiliza!” Isaka akasema, “Tazama, mimi ni mzee, wala siku ya kufa kwangu siijui. Basi, chukua silaha zako, yaani podo na upinde wako, uende porini ukaniwindie mnyama. Halafu unitengenezee chakula kitamu, kile nipendacho, uniletee ili nile, nipate kukubariki kabla ya kufa kwangu.” Kumbe, wakati huo Isaka alipokuwa akiongea na Esau mwanawe, Rebeka alikuwa anasikiliza. Kwa hiyo, Esau alipokwenda porini kuwinda, Rebeka alimwambia mwanawe Yakobo, “Nimemsikia baba yako akimwambia kaka yako Esau, amwindie mnyama na kumtengenezea chakula kitamu, ili ale, apate kumbariki mbele ya Mwenyezi-Mungu kabla ya kufa kwake. Sasa mwanangu, sikiliza maneno yangu na utii ninayokuagiza. Nenda kwenye kundi la mbuzi uniletee wanambuzi wawili wazuri, nimtengenezee baba yako chakula kitamu, kile apendacho. Kisha utampelekea baba yako ale, apate kukubariki kabla hajafa.” Lakini Yakobo akamwambia mama yake Rebeka, “Kumbuka kaka yangu Esau amejaa nywele mwilini, hali mimi sina. Labda baba atataka kunipapasa, nami nitaonekana kama ninamdhihaki, kwa hiyo nitajiletea laana badala ya baraka.” Mama yake akamwambia, “Laana yako na inipate mimi, mwanangu; wewe fanya ninavyokuagiza: Nenda ukaniletee hao wanambuzi.” Basi, Yakobo akaenda, akachukua wanambuzi wawili, akamletea mama yake; naye akatayarisha chakula kitamu, kile apendacho Isaka baba yake. Kisha Rebeka akatwaa mavazi bora ya Esau, mwanawe mkubwa, aliyokuwa nayo nyumbani, akamvika Yakobo, mwanawe mdogo. Akamvika pia ngozi za wale wanambuzi mikononi na kwenye sehemu laini shingoni mwake. Kisha akampa kile chakula kitamu na mkate aliokuwa ametayarisha.
Mwanzo 27:1-17 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ikawa Isaka alipokuwa mzee, na macho yake yamepofuka asione, akamwita Esau, mwanawe mkubwa, akamwambia, Mwanangu. Naye akamwitikia, Mimi hapa. Akasema, Tazama, sasa mimi nimekuwa mzee, wala sijui siku ya kufa kwangu. Basi, nakuomba, chukua uta wako, podo lako na upinde wako, ukaende nyikani uniwindie mawindo; ukaniandalie chakula kitamu namna ile niipendayo, ukaniletee, ili nile; na roho yangu ikubariki, kabla sijafa. Na Rebeka akasikia, Isaka aliposema na Esau mwanawe. Basi Esau akaenda mbugani awinde mawindo, ayalete. Rebeka akamwambia Yakobo mwanawe, akisema, Angalia, nimemsikia baba yako akisema na Esau, ndugu yako, akinena, Niletee mawindo, ukanifanyie chakula kitamu ili nile, na kukubariki mbele za BWANA kabla ya kufa kwangu. Basi, mwanangu, sikiliza sauti yangu kama nitakavyokuagiza. Nenda sasa kundini ukanitwalie wana-mbuzi wawili walio wema, nami nitawafanya chakula kitamu kwa baba yako, namna ile aipendayo. Kisha utampelekea baba yako, apate kula, ili akubariki kabla ya kufa kwake. Yakobo akamwambia Rebeka mamaye, Esau ndugu yangu ni mtu mwenye malaika, na mimi ni mtu laini. Labda baba yangu atanipapasa, nami nitakuwa machoni pake kama mdanganyifu; nami nitaleta juu yangu laana wala si baraka. Mamaye akamwambia, Laana yako na iwe juu yangu, mwanangu, usikie sauti yangu tu, nenda ukaniletee wana-mbuzi. Akaenda, akawatwaa, akamletea mamaye. Mamaye akafanya chakula kitamu namna ile aliyopenda babaye. Kisha Rebeka akatwaa mavazi mazuri ya Esau mwanawe mkubwa, aliyokuwa nayo nyumbani, akamvika Yakobo mwanawe mdogo. Na ngozi za wana-mbuzi akamvika mikononi, na katika ulaini wa shingo yake. Naye akampa Yakobo mwanawe mikononi mwake hicho chakula kitamu, na mkate aliouandaa.
Mwanzo 27:1-17 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ikawa Isaka alipokuwa mzee, na macho yake yamepofuka asione, akamwita Esau, mwanawe mkubwa, akamwambia, Mwanangu. Naye akamwitikia, Mimi hapa. Akasema, Tazama, sasa mimi nimekuwa mzee, wala sijui siku ya kufa kwangu. Basi, nakuomba, chukua mata yako, podo lako na upinde wako, ukaende nyikani uniwindie mawindo; ukanifanyie chakula kitamu namna ile niipendayo, ukaniletee, ili nile; na roho yangu ikubariki, kabla sijafa. Na Rebeka akasikia, Isaka aliposema na Esau mwanawe. Basi Esau akaenda nyikani awinde mawindo, ayalete. Rebeka akamwambia Yakobo mwanawe, akisema, Angalia, nimemsikia baba yako akisema na Esau, ndugu yako, akinena, Niletee mawindo, ukanifanyie chakula kitamu ili nile, na kukubariki mbele za BWANA kabla ya kufa kwangu. Basi, mwanangu, sikiliza sauti yangu kama nitakavyokuagiza. Enenda sasa kundini ukanitwalie wana-mbuzi wawili walio wema, nami nitawafanya chakula kitamu kwa baba yako, namna ile aipendayo. Kisha utampelekea baba yako, apate kula, ili akubariki kabla ya kufa kwake. Yakobo akamwambia Rebeka mamaye, Esau ndugu yangu ni mtu mwenye malaika, na mimi ni mtu laini. Labda baba yangu atanipapasa, nami nitakuwa machoni pake kama mdanganyifu; nami nitaleta juu yangu laana wala si mbaraka. Mamaye akamwambia, Laana yako na iwe juu yangu, mwanangu, usikie sauti yangu tu, enenda ukaniletee wana-mbuzi. Akaenda, akawatwaa, akamletea mamaye. Mamaye akafanya chakula kitamu namna ile aliyopenda babaye. Kisha Rebeka akatwaa mavazi mazuri ya Esau mwanawe mkubwa, aliyokuwa nayo nyumbani, akamvika Yakobo mwanawe mdogo. Na ngozi za wana-mbuzi akamvika mikononi, na katika ulaini wa shingo yake. Naye akampa Yakobo mwanawe mikononi mwake hicho chakula kitamu, na mkate alioufanya.
Mwanzo 27:1-17 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)
Isaka alipokuwa mzee na macho yake yakapofuka kwa kukosa nguvu, akamwita Esau mwanawe mkubwa, akamwambia, “Mwanangu.” Akajibu, “Mimi hapa.” Isaka akasema, “Mimi sasa ni mzee na sijui siku ya kufa kwangu. Sasa basi chukua silaha zako, podo na upinde, uende nyikani, ukaniwindie mawindo. Uniandalie chakula kitamu nikipendacho uniletee nile, ili nikubariki kabla sijafa.” Rebeka alikuwa akisikiliza Isaka akizungumza na mwanawe Esau. Basi Esau alipoenda nyikani kuwinda mawindo ayalete, Rebeka akamwambia Yakobo mwanawe, “Tazama, nimemsikia baba yako akimwambia ndugu yako Esau, ‘Niletee mawindo, kisha ukaniandalie chakula kitamu nile, ili nikubariki mbele za Mwenyezi Mungu kabla sijafa.’ Sasa mwanangu, nisikilize kwa makini na ufanye yale ninayokuambia: Nenda sasa katika kundi ukaniletee wana-mbuzi wawili wazuri, ili nimwandalie baba yako chakula kitamu kile anachokipenda. Kisha umpelekee baba yako ale, ili akubariki kabla hajafa.” Yakobo akamwambia Rebeka mama yake, “Lakini ndugu yangu Esau ana nywele mwilini, nami nina ngozi nyororo. Itakuwaje baba yangu akinigusa? Ataona kama ninamfanyia ujanja, nami nijiletee laana badala ya baraka.” Mama yake akamwambia, “Mwanangu, laana na iwe juu yangu. Fanya tu ninalokuambia: nenda ukaniletee hao wana-mbuzi.” Kwa hiyo alienda akawaleta, akampa mama yake, naye Rebeka akaandaa chakula kitamu, kile alichokipenda baba yake. Kisha Rebeka akachukua nguo nzuri za Esau mwanawe wa kwanza, alizokuwa nazo nyumbani, akamvika Yakobo mwanawe mdogo. Pia akamfunika mikononi na sehemu laini ya shingo kwa ngozi za mbuzi. Hatimaye akampa Yakobo hicho chakula kitamu pamoja na mkate aliouoka.