Mwanzo 25:29-34
Mwanzo 25:29-34 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Yakobo akapika chakula cha dengu. Esau akaja kutoka mbugani, naye alikuwa amechoka sana. Esau akamwambia Yakobo, Tafadhali, unipe hicho chakula chekundu nile, kwa kuwa ninazimia mimi. Kwa hiyo walimwita jina lake Edomu. Yakobo akamwambia, Kwanza niuzie leo haki yako ya mzaliwa wa kwanza. Esau akasema, Tazama, mimi ni karibu kufa, itanifaa nini haki hii ya uzazi? Yakobo akamwambia, Niapie kwanza. Naye akamwapia, akamwuzia Yakobo haki yake ya mzaliwa wa kwanza. Yakobo akampa Esau mkate na chakula cha dengu, naye akala, akanywa, kisha akaondoka, akaenda zake. Hivyo Esau akaidharau haki yake ya mzaliwa wa kwanza.
Mwanzo 25:29-34 Biblia Habari Njema (BHN)
Siku moja, Yakobo alipokuwa anapika dengu, Esau alirudi nyumbani kutoka mawindoni ana njaa sana. Kwa hiyo akamwambia Yakobo, “Nafa njaa; tafadhali, nigawie chakula hicho chekundu nile.” (Ndiyo maana walimpanga jina Edomu yaani mwekundu). Yakobo akajibu, “Kwanza niuzie haki yako ya mzaliwa wa kwanza.” Esau akasema, “Sawa! Niko karibu kufa; haki yangu ya mzaliwa wa kwanza itanifaa nini?” Yakobo akamwambia, “Niapie kwanza.” Basi, Esau akamwapia na kumwuzia Yakobo haki yake ya mzaliwa wa kwanza. Ndipo Yakobo akampa Esau mkate na dengu kiasi. Esau akala, akanywa, kisha akaondoka, akaenda zake. Hivyo ndivyo Esau alivyoidharau haki yake ya mzaliwa wa kwanza.
Mwanzo 25:29-34 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Yakobo akapika chakula cha dengu. Esau akaja kutoka nyikani, naye alikuwa amechoka sana. Esau akamwambia Yakobo, Tafadhali, unipe hicho chakula chekundu nile, kwa kuwa ninazimia mimi. Kwa hiyo walimwita jina lake Edomu. Yakobo akamwambia, Kwanza niuzie leo haki yako ya mzaliwa wa kwanza. Esau akasema, Tazama, mimi ni karibu kufa, itanifaa nini haki hii ya uzazi? Yakobo akamwambia, Uniapie kwanza. Naye akamwapia, akamwuzia Yakobo haki yake ya mzaliwa wa kwanza. Yakobo akampa Esau mkate na chakula cha dengu, naye akala, akanywa, kisha akaondoka, akaenda zake. Hivyo Esau akaidharau haki yake ya mzaliwa wa kwanza.
Mwanzo 25:29-34 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Siku moja Yakobo alipika mchuzi wa dengu, Esau akarudi kutoka porini akiwa na njaa kali. Esau akamwambia Yakobo, “Haraka, nipe huo mchuzi mwekundu! Nina njaa kali sana!” (Hii ndiyo sababu pia aliitwa Edomu.) Yakobo akamjibu, “Niuzie kwanza haki yako ya mzaliwa wa kwanza.” Esau akasema, “Tazama, mimi niko karibu ya kufa, itanifaa nini haki ya mzaliwa wa kwanza?” Yakobo akamwambia, “Niapie kwanza.” Hivyo Esau akamwapia, akamuuzia Yakobo haki yake ya kuzaliwa. Ndipo Yakobo akampa Esau mkate na ule mchuzi wa dengu. Akala na kunywa, kisha akainuka akaenda zake. Kwa hiyo Esau alidharau haki yake ya mzaliwa wa kwanza.