Mwanzo 25:20-24
Mwanzo 25:20-24 Biblia Habari Njema (BHN)
Isaka alipokuwa na umri wa miaka arubaini alimwoa Rebeka, binti Bethueli, Mwaramu wa Padan-aramu. Rebeka alikuwa dada yake Labani. Rebeka alikuwa tasa, kwa hiyo Isaka akamwomba Mwenyezi-Mungu. Naye Mwenyezi-Mungu akakubali ombi lake, Rebeka akapata mimba. Mimba hiyo ilikuwa ya mapacha. Watoto hao wakashindana tumboni mwake Rebeka, naye akasema, “Kama hivi ndivyo mambo yalivyo, ya nini kuishi?” Basi, akaenda kumwuliza Mwenyezi-Mungu. Mwenyezi-Mungu akamwambia, “Mataifa mawili yamo tumboni mwako; makabila mawili yatakayozaliwa nawe, yatafarakana. Moja litakuwa lenye nguvu kuliko lingine; mkubwa atamtumikia mdogo.” Siku zake za kujifungua zilipotimia, Rebeka alijifungua mapacha.
Mwanzo 25:20-24 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Isaka akawa mwenye miaka arubaini alipomtwaa Rebeka binti Bethueli, Mshami, wa Padan-aramu, ndugu wa Labani, Mshami, kuwa mke wake. Isaka akamwomba BWANA kwa ajili ya mke wake, maana alikuwa tasa. Naye BWANA akamwitikia, na Rebeka mkewe akachukua mimba. Watoto wakashindana tumboni mwake. Naye akasema, Ikiwa ni hivi, kuishi kwanifaa nini? Akaenda kumwuliza BWANA. BWANA akamwambia, Mataifa mawili yako tumboni mwako, Na makabila mawili ya watu watafarakana tangu tumboni mwako. Kabila moja litakuwa hodari kuliko la pili, Na mkubwa atamtumikia mdogo. Siku zake za kuzaa zilipotimia, tazama! Mapacha walikuwamo tumboni mwake.
Mwanzo 25:20-24 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Isaka akawa mwenye miaka arobaini alipomtwaa Rebeka binti Bethueli, Mshami, wa Padan-aramu, ndugu wa Labani, Mshami, kuwa mke wake. Isaka akamwomba BWANA kwa ajili ya mke wake, maana alikuwa tasa. Naye BWANA akamwitikia, na Rebeka mkewe akachukua mimba. Watoto wakashindana tumboni mwake. Naye akasema, Ikiwa ni hivi, kuishi kwanifaa nini? Akaenda kumwuliza BWANA. BWANA akamwambia, Mataifa mawili yako tumboni mwako, Na kabila mbili za watu watafarakana tangu tumboni mwako. Kabila moja litakuwa hodari kuliko la pili, Na mkubwa atamtumikia mdogo. Siku zake za kuzaa zilipotimia, tazama! Mapacha walikuwamo tumboni mwake.
Mwanzo 25:20-24 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Isaki alikuwa na umri wa miaka arobaini alipomwoa Rebeka binti Bethueli Mwaramu kutoka Padan-Aramu, nduguye Labani Mwaramu. Isaki akamwomba BWANA kwa ajili ya mke wake, kwa sababu alikuwa tasa. BWANA akajibu maombi yake na Rebeka mkewe akapata mimba. Watoto wakashindana tumboni mwake, akasema, “Kwa nini haya yanatokea kwangu?” Kwa hiyo akaenda kumuuliza BWANA. BWANA akamjibu, “Mataifa mawili yamo tumboni mwako, na mataifa hayo mawili kutoka ndani yako watatenganishwa. Mmoja atakuwa na nguvu zaidi kuliko mwingine, na yule mkubwa atamtumikia yule mdogo.” Wakati wake wa kujifungua ulipotimia, walikuwepo mapacha wa kiume tumboni mwake.