Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Ezra 6:1-12

Ezra 6:1-12 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Ndipo mfalme Dario akatoa amri, na watu wakatafuta katika nyumba ya vyuo vya tarehe, hapo akiba zilipowekwa katika Babeli. Na chuo kimoja kilipatikana huko Akmetha, katika nyumba ya mfalme iliyo katika wilaya ya Umedi, na ndani yake maneno haya yameandikwa ili yakumbukwe. Katika mwaka wa kwanza wa mfalme Koreshi, mfalme Koreshi alitoa amri, Kwa habari ya nyumba ya Mungu huko Yerusalemu, nyumba hiyo na ijengwe, mahali watoapo dhabihu, na misingi yake ipigwe na kufanywa imara sana; kuinuka kwake kuwe mikono sitini, na upana wake mikono sitini; ziwepo safu tatu za mawe makubwa, na safu moja ya miti mipya; gharama zake zitolewe katika nyumba ya mfalme. Na vyombo vya dhahabu na fedha, vya nyumba ya Mungu, ambavyo mfalme Nebukadreza alivitoa katika nyumba ya Mungu, iliyoko Yerusalemu, akavileta mpaka Babeli, na virudishwe, vikaingizwe tena katika hekalu lililoko Yerusalemu, kila kimoja mahali pake, na wewe uvitie katika nyumba ya Mungu. Basi sasa ninyi, Tatenai, liwali wa ng’ambo ya Mto, na Shethar-Bozenai, na hao wenzi wenu wa Kiajemi, mlio ng’ambo ya Mto, jitengeni na mahali pale; iacheni kazi hii ya nyumba ya Mungu, msiizuie; waacheni liwali wa Wayahudi, na wazee wa Wayahudi, waijenge nyumba hii ya Mungu mahali pake. Tena, natoa amri kuwaagiza ninyi mtakayowatendea wazee hao wa Wayahudi, kwa kazi hii ya kuijenga nyumba ya Mungu; katika mali ya mfalme, yaani, katika kodi za nchi iliyo ng’ambo ya Mto, watu hao wapewe gharama zote kwa bidii, ili wasizuiliwe. Na kila kitu wanachokihitaji, katika ng’ombe wachanga, na kondoo waume, na wana-kondoo, kwa sadaka za kuteketezwa watakazomtolea Mungu wa mbinguni, na ngano, na chumvi, na divai, na mafuta, kama makuhani walioko Yerusalemu watakavyosema, na wapewe vitu hivyo vyote siku kwa siku, msikose kuwapa; wapate kumtolea Mungu wa mbinguni sadaka zenye harufu nzuri, na kumwombea mfalme, na wanawe, wapate uzima. Pia nimetoa amri kwamba, mtu awaye yote atakayelibadili neno hili, boriti na itolewe katika nyumba yake, akainuliwe na kutungikwa juu yake; tena nyumba yake ikafanywe jaa kwa ajili ya neno hili. Na Mungu huyu, aliyelifanya jina lake likae pale, na aangamize wafalme wote, na watu wote, watakaonyosha mikono yao kulibadili neno hili, na kuiharibu nyumba hii ya Mungu, iliyoko Yerusalemu. Mimi, Dario, nimetoa amri; na ifanyike kwa bidii nyingi.

Shirikisha
Soma Ezra 6

Ezra 6:1-12 Biblia Habari Njema (BHN)

Mfalme Dario alitoa amri na uchunguzi ulifanywa mjini Babuloni katika nyumba ya kumbukumbu za kifalme. Lakini kitabu kilipatikana mjini Ekbatana katika mkoa wa Media, nacho kilikuwa na maagizo yafuatayo: “Mnamo mwaka wa kwanza wa utawala wake, mfalme Koreshi alitoa amri nyumba ya Mungu ijengwe upya mjini Yerusalemu, na iwe mahali pa kutolea tambiko na sadaka za kuteketezwa. Kimo chake kitakuwa mita 27 na upana wake mita 27. Kuta zake zitajengwa kwa safu moja ya miti juu ya kila safu tatu za mawe makubwa. Gharama zote zilipwe kutoka katika hazina ya mfalme. Pia, vyombo vyote vya dhahabu na fedha ambavyo mfalme Nebukadneza alivileta Babuloni kutoka katika hekalu la Yerusalemu, vitarudishwa na kuwekwa kila kimoja mahali pake katika nyumba ya Mungu.” Ndipo Dario akapeleka ujumbe ufuatao: “Kwa Tatenai, mtawala wa mkoa wa magharibi ya Eufrate, Shethar-bozenai na maofisa wenzako mkoani. ‘Msiende huko kwenye hekalu, na acheni kazi ya ujenzi wa nyumba hii ya Mungu iendelee. Mwacheni mtawala wa Yuda na viongozi wa Wayahudi waijenge nyumba ya Mungu mahali pake. Zaidi ya hayo, natoa amri kwamba nyinyi mtawasaidia katika kazi hiyo. Gharama zao zote zitalipwa bila kuchelewa kutoka katika hazina ya mfalme inayotokana na kodi kutoka katika mkoa wa magharibi wa mto Eufrate. Kila siku, tena bila kukosa, mtawapa makuhani wa Yerusalemu kila kitu watakachohitaji; iwe ni fahali wachanga, kondoo dume au wanakondoo wa sadaka za kuteketezwa kwa Mungu wa mbinguni, au ngano, chumvi, divai au mafuta. Haya yote yatatendeka ili waweze kumtolea Mungu wa mbinguni tambiko zinazompendeza na waombee maisha yangu mimi mfalme na watoto wangu. Naamuru pia kwamba mtu yeyote ambaye hatatii amri hii, boriti ingolewe kutoka katika nyumba yake, na atumbuliwe kwayo. Tena, nyumba yake na ifanywe kuwa rundo la mavi. Mungu aliyeuchagua mji wa Yerusalemu kuwa mahali pake pa kuabudiwa na amwangushe mfalme au taifa lolote litakalopinga amri hii au kutaka kuiharibu nyumba hii ya Mungu iliyoko mjini Yerusalemu. Mimi Dario nimetoa amri hii. Ni lazima ifuatwe.’”

Shirikisha
Soma Ezra 6

Ezra 6:1-12 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Ndipo mfalme Dario akatoa amri, na watu wakachunguza katika nyumba ya kuhifadhia vitabu vya kumbukumbu ambapo hati ziliwekwa katika Babeli. Na kitabu kimoja kilipatikana huko Akmetha, katika nyumba ya mfalme iliyo katika wilaya ya Umedi, na ndani yake maneno haya yameandikwa ili yakumbukwe. Katika mwaka wa kwanza wa mfalme Koreshi, mfalme Koreshi alitoa amri, Kuhusu nyumba ya Mungu huko Yerusalemu, nyumba hiyo na ijengwe, mahali watoapo dhabihu, na misingi yake ipigwe na kufanywa imara sana; kuinuka kwake kuwe mikono sitini, na upana wake mikono sitini; ziwepo safu tatu za mawe makubwa, na safu moja ya miti mipya; gharama zake zitolewe katika nyumba ya mfalme. Na vyombo vya dhahabu na fedha, vya nyumba ya Mungu, ambavyo mfalme Nebukadneza alivitoa katika nyumba ya Mungu, iliyoko Yerusalemu, akavileta mpaka Babeli, na virudishwe, vikaingizwe tena katika hekalu lililoko Yerusalemu, kila kimoja mahali pake, na wewe uvitie katika nyumba ya Mungu. Basi sasa ninyi, Tatenai, Mkuu wa mkoa wa ng'ambo ya Mto, na Shethar-Bozenai, na hao wenzi wenu wa Kiajemi, mlio ng'ambo ya Mto, jitengeni na mahali pale; iacheni kazi hii ya nyumba ya Mungu, msiizuie; waacheni Mkuu wa mkoa wa Wayahudi, na wazee wa Wayahudi, waijenge nyumba hii ya Mungu mahali pake. Tena, natoa amri kuwaagiza ninyi mtakayowatendea wazee hao wa Wayahudi, kwa kazi hii ya kuijenga nyumba ya Mungu; kwa mali ya mfalme, yaani, kwa kodi za nchi iliyo ng'ambo ya Mto, watu hao wapewe gharama zote bila kukawia, ili wasizuiliwe. Na kila kitu wanachokihitaji, katika ng'ombe wachanga, na kondoo dume, na wana-kondoo, kwa sadaka za kuteketezwa watakazomtolea Mungu wa mbinguni, na ngano, na chumvi, na divai, na mafuta, kama makuhani walioko Yerusalemu watakavyosema, na wapewe vitu hivyo vyote siku kwa siku, msikose kuwapa; wapate kumtolea Mungu wa mbinguni sadaka zenye harufu nzuri, na kumwombea mfalme, na wanawe, wapate uzima. Pia nimetoa amri kwamba, mtu awaye yote atakayelibadili neno hili, boriti na itolewe katika nyumba yake, akainuliwe na kutungikwa juu yake; tena nyumba yake ikafanywe jaa kwa ajili ya neno hili. Na Mungu huyu, aliyelifanya jina lake likae pale, na aangamize wafalme wote, na watu wote, watakaonyosha mikono yao kulibadili neno hili, na kuiharibu nyumba hii ya Mungu, iliyoko Yerusalemu. Mimi, Dario, nimetoa amri; na izingatiwe mara moja.

Shirikisha
Soma Ezra 6

Ezra 6:1-12 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Kisha Mfalme Dario alitoa amri, nao wakafanya uchunguzi katika kumbukumbu zilizohifadhiwa katika hazina huko Babeli. Karatasi moja ndefu ya maandishi ilipatikana huko Ekbatana katika jimbo la Umedi. Haya ndiyo yaliyokuwa yameandikwa humo: Kumbukumbu: Katika mwaka wa kwanza wa kutawala Mfalme Koreshi, mfalme alitoa amri kuhusu Hekalu la Mungu katika Yerusalemu: Hekalu na lijengwe tena mahali palepale Wayahudi walipokuwa wakitoa dhabihu, kwenye msingi ule ule. Iwe na kimo cha mikono sitini, upana wa mikono sitini, kuta zijengwe kwa safu tatu za mawe makubwa kisha ifuate safu moja ya mbao. Gharama zitalipwa kutoka hazina ya mfalme. Pia, vyombo vya dhahabu na vya fedha vya nyumba ya Mungu, ambavyo Nebukadneza alivichukua kutoka kwenye Hekalu huko Yerusalemu akavileta Babeli, yapasa virudishwe mahali pake ndani ya Hekalu huko Yerusalemu, yapasa viwekwe ndani ya nyumba ya Mungu. Sasa basi, Tatenai, mtawala wa Ngʼambo ya Mto Frati na Shethar-Bozenai pamoja na ninyi, maafisa wenzao wa jimbo hilo kaeni mbali na mahali hapo. Msiingilie kazi ya Hekalu hili la Mungu. Mwacheni mtawala wa Wayahudi na viongozi Wayahudi wajenge upya nyumba hii ya Mungu mahali pake. Zaidi ya hayo, hapa natoa amri kuhusu mtakalofanya kwa ajili ya wazee wa Wayahudi katika ujenzi wa nyumba hii ya Mungu: Gharama za watu hawa zitalipwa kikamilifu kutoka hazina ya mfalme, kutoka kwenye mapato ya Ngʼambo ya Mto Frati, ili ujenzi usisimame. Chochote kinachohitajika kama mafahali wachanga, kondoo dume, wana-kondoo kwa ajili ya sadaka za kuteketezwa kwa Mungu wa mbinguni, ngano, chumvi, divai na mafuta kama vitakavyohitajika na makuhani huko Yerusalemu, lazima wapewe kila siku pasipo kukosa, ili waweze kutoa dhabihu inayompendeza Mungu wa mbinguni na kumwombea mfalme na wanawe hali njema. Zaidi ya hayo, ninaamuru kwamba mtu yeyote atakayebadilisha amri hii, boriti itangʼolewa kutoka nyumba yake, ichongwe upande mmoja na atumbuliwe nayo. Kwa ajili ya kosa hili nyumba yake ifanywe lundo la taka. Naye Mungu, aliyeliweka Jina lake huko, amwangushe mfalme yeyote au watu watakaoinua mikono kubadili amri hii au kuharibu Hekalu hili lililoko Yerusalemu. Mimi Dario nimetoa amri hii. Nayo itekelezwe kwa bidii na kwa makini.

Shirikisha
Soma Ezra 6