Ezra 6:1-12
Ezra 6:1-12 NEN
Kisha Mfalme Dario alitoa amri, nao wakafanya uchunguzi katika kumbukumbu zilizohifadhiwa katika hazina huko Babeli. Karatasi moja ndefu ya maandishi ilipatikana huko Ekbatana katika jimbo la Umedi. Haya ndiyo yaliyokuwa yameandikwa humo: Kumbukumbu: Katika mwaka wa kwanza wa kutawala Mfalme Koreshi, mfalme alitoa amri kuhusu Hekalu la Mungu katika Yerusalemu: Hekalu na lijengwe tena mahali palepale Wayahudi walipokuwa wakitoa dhabihu, kwenye msingi ule ule. Iwe na kimo cha mikono sitini, upana wa mikono sitini, kuta zijengwe kwa safu tatu za mawe makubwa kisha ifuate safu moja ya mbao. Gharama zitalipwa kutoka hazina ya mfalme. Pia, vyombo vya dhahabu na vya fedha vya nyumba ya Mungu, ambavyo Nebukadneza alivichukua kutoka kwenye Hekalu huko Yerusalemu akavileta Babeli, yapasa virudishwe mahali pake ndani ya Hekalu huko Yerusalemu, yapasa viwekwe ndani ya nyumba ya Mungu. Sasa basi, Tatenai, mtawala wa Ngʼambo ya Mto Frati na Shethar-Bozenai pamoja na ninyi, maafisa wenzao wa jimbo hilo kaeni mbali na mahali hapo. Msiingilie kazi ya Hekalu hili la Mungu. Mwacheni mtawala wa Wayahudi na viongozi Wayahudi wajenge upya nyumba hii ya Mungu mahali pake. Zaidi ya hayo, hapa natoa amri kuhusu mtakalofanya kwa ajili ya wazee wa Wayahudi katika ujenzi wa nyumba hii ya Mungu: Gharama za watu hawa zitalipwa kikamilifu kutoka hazina ya mfalme, kutoka kwenye mapato ya Ngʼambo ya Mto Frati, ili ujenzi usisimame. Chochote kinachohitajika kama mafahali wachanga, kondoo dume, wana-kondoo kwa ajili ya sadaka za kuteketezwa kwa Mungu wa mbinguni, ngano, chumvi, divai na mafuta kama vitakavyohitajika na makuhani huko Yerusalemu, lazima wapewe kila siku pasipo kukosa, ili waweze kutoa dhabihu inayompendeza Mungu wa mbinguni na kumwombea mfalme na wanawe hali njema. Zaidi ya hayo, ninaamuru kwamba mtu yeyote atakayebadilisha amri hii, boriti itangʼolewa kutoka nyumba yake, ichongwe upande mmoja na atumbuliwe nayo. Kwa ajili ya kosa hili nyumba yake ifanywe lundo la taka. Naye Mungu, aliyeliweka Jina lake huko, amwangushe mfalme yeyote au watu watakaoinua mikono kubadili amri hii au kuharibu Hekalu hili lililoko Yerusalemu. Mimi Dario nimetoa amri hii. Nayo itekelezwe kwa bidii na kwa makini.