Ezekieli 8:1-18
Ezekieli 8:1-18 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Katika siku ya tano ya mwezi wa sita mwaka wa sita, baada ya kupelekwa uhamishoni nilipokuwa nimeketi katika nyumba yangu na wazee wa Yuda walikuwa wameketi mbele yangu, mkono wa BWANA Mwenyezi ulikuja juu yangu. Nikatazama, nikaona umbo mfano wa mwanadamu. Kutokana na kile kilichoonekana kuwa kiuno chake kuelekea chini alifanana na moto. Kuanzia kwenye kiuno kuelekea juu sura yake kama chuma kingʼaavyo kikiwa ndani ya moto. Akanyoosha kitu kilichoonekana kama mkono, akaniinua kwa kushika nywele za kichwa changu. Roho akaniinua juu kati ya nchi na mbingu nikiwa katika maono ya Mungu akanichukua mpaka Yerusalemu, kwenye ingilio la lango la upande wa kaskazini ya ukumbi wa ndani, mahali iliposimama ile sanamu ichocheayo wivu. Hapo mbele yangu palikuwa na utukufu wa Mungu wa Israeli, kama utukufu ule niliouona katika maono kule ua wa ndani. Kisha akaniambia, “Mwanadamu, tazama kuelekea kaskazini.” Hivyo nikatazama na kwenye ingilio upande wa kaskazini wa lango la madhabahu, nikaona sanamu hii ya wivu. Ndipo akaniambia, “Mwanadamu, je, unaona yale wanayofanya, haya mambo ya machukizo kabisa nyumba ya Israeli wanayotenda hapa, ambayo yatanifanya niende mbali na mahali pangu patakatifu? Lakini utaona vitu ambavyo vinachukiza zaidi hata kuliko hivi.” Kisha akanileta mpaka ingilio la ukumbi. Nikatazama, nami nikaona tundu ukutani. Akaniambia, “Mwanadamu, sasa toboa kwenye ukuta huu.” Ndipo nikatoboa ule ukuta, nikaona hapo pana mlango. Naye akaniambia, “Ingia ndani, ukaone maovu na machukizo wanayofanya humu.” Hivyo nikaingia ndani na kutazama, nikaona kuta zote zimechorwa kila aina ya vitu vitambaavyo na ya wanyama wachukizao wa kila aina na sanamu zote za nyumba ya Israeli. Mbele yao walisimama wazee sabini wa nyumba ya Israeli, naye Yaazania mwana wa Shafani alikuwa amesimama miongoni mwao. Kila mmoja alikuwa na chetezo mkononi na moshi wa harufu nzuri ya uvumba ulikuwa unapanda juu. Akaniambia, “Mwanadamu, umeona wanayoyafanya wazee wa nyumba ya Israeli gizani, kila mmoja kwenye sehemu yake mwenyewe ya kufanyia ibada za sanamu yake? Wao husema, ‘BWANA hatuoni, BWANA ameiacha nchi.’ ” Akasema tena, “Bado utaona machukizo wanayofanya ambayo ni makubwa kuliko haya.” Ndipo akanileta mpaka ingilio la lango la kaskazini la nyumba ya BWANA, nami nikaona wanawake wameketi hapo, wakimwombolezea Tamuzi. Akaniambia, “Unaliona hili, mwanadamu? Utaona vitu ambavyo ni machukizo kuliko hili.” Ndipo akanileta mpaka kwenye ukumbi wa ndani wa nyumba ya BWANA, nako huko katika ingilio la Hekalu, kati ya baraza na madhabahu, walikuwepo wanaume wapatao ishirini na watano. Wakiwa wamelipa kisogo Hekalu la BWANA na kuelekeza nyuso zao upande wa mashariki, wakilisujudia jua huko mashariki. Akaniambia, “Je, umeona hili mwanadamu? Je, ni jambo dogo sana kwa nyumba ya Yuda kufanya machukizo wanayoyafanya hapa? Je, ni lazima pia waijaze nchi dhuluma na kuendelea siku zote kunikasirisha? Watazame wanavyonibania pua kana kwamba ninanuka! Kwa hiyo nitashughulika nao kwa hasira, sitawaonea huruma wala kuwaachilia. Wajapopiga makelele masikioni mwangu, sitawasikiliza.”
Ezekieli 8:1-18 Biblia Habari Njema (BHN)
Katika mwaka wa sita, siku ya tano ya mwezi wa sita, nilikuwa nyumbani kwangu pamoja na wazee wa Yuda. Basi, ghafla nikakumbwa na nguvu ya Mwenyezi-Mungu. Nilipotazama, nikaona maono: Kitu kilichofanana na binadamu. Sehemu yake ya chini, iliyoonekana kama ndio kiuno chake, ilikuwa kama moto. Toka kiuno chake kwenda juu alikuwa na mngao kama wa shaba ingaayo. Basi, akanyosha kitu kama mkono, akanishika kwa nywele zangu. Roho ya Mungu ikaninyanyua kati ya ardhi na mbingu, ikanipeleka mpaka Yerusalemu nikiwa katika maono hayo ya Mungu. Nikafika kwenye kiingilio cha lango la ukumbi wa ndani linaloelekea upande wa kaskazini, mahali palipowekwa sanamu iliyomchukiza Mungu. Utukufu wa Mungu wa Israeli ulikuwapo hapo; nao ulikuwa kama utukufu ule niliouona katika maono kule bondeni. Kisha Mungu akaniambia, “Wewe mtu, tazama upande wa kaskazini.” Nami nikatazama upande wa kaskazini, na huko upande wa kaskazini wa lango la madhabahu, niliona ile sanamu iliyomchukiza Mungu. Basi, Mungu akaniambia, “Wewe mtu, je, waona mambo wanayofanya, machukizo makubwa wanayofanya Waisraeli ili wapate kunifukuza kutoka maskani yangu? Tena utaona machukizo mengine makubwa zaidi.” Kisha akanipeleka mpaka lango la ua. Nilipoangalia nikaona tundu ukutani. Naye akaniambia, “Wewe mtu, toboa ukuta huu.” Nami, nikatoboa, nikaona kulikuwa na mlango. Naye akaniambia, “Ingia ndani ukaangalie machukizo mabaya wanayofanya humo.” Basi, nikaingia, nikaona sanamu za wadudu na za wanyama wa kila aina ya kuchukiza na vinyago vyote vya miungu ya Waisraeli, vimechorwa kuuzunguka ukuta. Na mbele ya sanamu hizo walisimama wazee sabini wa watu wa Israeli pamoja na Yaazania mwana wa Shafani. Kila mmoja alikuwa na chetezo mkononi, na moshi wa ubani ulipanda juu. Kisha Mungu akaniambia, “Wewe mtu, umeona wanayotenda wazee wa Waisraeli gizani, kila mtu katika chumba chake cha sanamu. Wanadai ati Mwenyezi-Mungu hatuoni. Mwenyezi-Mungu ameiacha nchi.” Tena akaniambia, “Bado utaona machukizo makubwa zaidi wanayotenda.” Kisha akanichukua mpaka lango la kaskazini la nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Huko kulikuwa na wanawake wameketi wakimwombolezea Tamuzi. Mungu akaniambia: “Wewe mtu, umeyaona hayo? Bado utaona machukizo mengine makubwa kuliko hayo.” Kisha akanipeleka mpaka ua wa ndani ya nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Huko mlangoni mwa hekalu, kati ya ukumbi na madhabahu, walikuwapo wanaume wapatao ishirini na watano, wakilipa kisogo hekalu, na nyuso zao zimeelekea upande wa mashariki. Walikuwa wanaabudu jua wakielekea upande wa mashariki. Mungu akaniambia, “Wewe mtu, je umeyaona mambo hayo? Hata hivyo, watu wa Yuda wanaona machukizo hayo kuwa ni kidogo. Wanaijaza nchi dhuluma na kuzidi kunikasirisha. Angalia jinsi wamekaa hapo, wananiudhi kupita kiasi. Kwa sababu ya mambo hayo watasikia uzito wa ghadhabu yangu. Sitamwacha hata mmoja aponyoke wala sitamwonea huruma mtu yeyote. Hata wakinililia kwa sauti kubwa mimi sitawasikiliza.”
Ezekieli 8:1-18 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ikawa katika mwaka wa sita, mwezi wa sita, siku ya tano ya mwezi, nilipokuwa nikikaa nyumbani mwangu, wazee wa Yuda nao wakiwa wamekaa mbele yangu, mkono wa Bwana MUNGU ukaniangukia huko. Ndipo nikaangalia, na tazama, palikuwa na kitu kilichofanana na mwanadamu; kuanzia kilichoonekana kama viuno vyake kwenda chini ilikuwa moto; na kuanzia kilichoonekana kama viuno vyake kwenda juu, ilikuwa mfano wa mwangaza, kama rangi ya kaharabu. Naye akanyosha mfano wa mkono, akanishika kwa kishungi kimoja cha nywele za kichwa changu; nayo roho ikaniinua kati ya dunia na mbingu, ikanileta katika maono ya Mungu mpaka Yerusalemu, mpaka mlango wa kuingilia ua wa ndani uelekeao upande wa kaskazini; mahali palipokuwa pamewekwa sanamu ya wivu, itiayo wivu. Na tazama, huo utukufu wa Mungu wa Israeli ulikuwapo hapo, sawasawa na maono yale niliyoyaona katika bonde. Ndipo akaniambia, Mwanadamu, inua macho yako sasa, uangalie upande wa kaskazini. Basi nikainua macho yangu, nikaangalia upande wa kaskazini, na tazama, upande wa kaskazini wa mlango, ilikuwako sanamu ile ya wivu, mahali pale pa kuingilia. Akaniambia, Mwanadamu, je! Unayaona wanayoyafanya, yaani, haya machukizo makubwa wanayoyafanya nyumba ya Israeli hapa, ili niende zangu mbali na patakatifu pangu? Lakini utaona tena machukizo makubwa mengine. Akanileta hadi katika mlango wa ua; nami nilipoangalia, tazama, pana tundu katika ukuta. Ndipo akaniambia, Mwanadamu, toboa sasa katika ukuta huu; nami nilipotoboa, tazama, pana mlango. Akaniambia, Ingia uyaone machukizo mabaya wanayoyafanya hapa. Basi, nikaingia, nikaona; na tazama, kila namna ya wadudu, na wanyama wachukizao, na taswira za vinyago vyote vya nyumba ya Israeli, zimepigwa ukutani pande zote. Na watu sabini wa wazee wa Israeli walikuwa wamesimama na kuzielekea, na katikati yao alisimama Yaazania, mwana wa Shafani; kila mmoja ana chetezo mkononi mwake, na harufu ya moshi wa uvumba ilipaa juu. Kisha akaniambia, Mwanadamu, umeyaona wanayotenda wazee wa nyumba ya Israeli gizani, kila mtu ndani ya vyumba vyake vya sanamu? Maana husema, BWANA hatuoni; BWANA ameiacha nchi hii. Akaniambia tena, Utaona tena machukizo makubwa mengine wanayoyatenda. Ndipo akanileta mpaka maingilio ya lango la kaskazini mwa nyumba ya BWANA, ulioelekea upande wa kaskazini, na tazama, wanawake wameketi wakimlilia Tamuzi. Akaniambia, Mwanadamu umeyaona haya? Utaona tena machukizo makubwa kuliko hayo. Akanileta mpaka ua wa ndani wa nyumba ya BWANA, na tazama, mlangoni pa hekalu la BWANA, kati ya ukumbi na madhabahu, walikuwako watu kama ishirini na watano, wamelipa kisogo hekalu la BWANA, na nyuso zao zimeelekea upande wa mashariki, nao wanaliabudu jua, kwa kuuelekea upande wa mashariki. Basi, akaniambia, Umeyaona haya, Ee mwanadamu? Je! Ni jambo dogo sana kwa nyumba ya Yuda, wayafanye machukizo wanayoyafanya hapa? Kwa maana wameijaza nchi hii udhalimu, tena wamerejea nyuma ili kunikasirisha; na, tazama, wanaliweka tawi puani. Kwa sababu hiyo mimi nami nitatenda kwa ghadhabu; jicho langu halitaachilia, wala sitawaonea huruma, na wajapolia masikioni mwangu kwa sauti kuu, sitawasikiliza.
Ezekieli 8:1-18 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ikawa katika mwaka wa sita, mwezi wa sita, siku ya tano ya mwezi, nilipokuwa nikikaa nyumbani mwangu, wazee wa Yuda nao wali wamekaa mbele yangu, mkono wa Bwana MUNGU ukaniangukia huko. Ndipo nikaangalia, na tazama, kana kwamba ni mfano wa moto; tangu mfano wa viuno vyake na chini, moto; na tangu mfano wa viuno vyake na juu, kana kwamba ni mfano wa mwangaza, kama rangi ya kaharabu. Naye akanyosha mfano wa mkono, akanishika kwa kishungi kimoja cha nywele za kichwa changu; nayo roho ikaniinua kati ya dunia na mbingu, ikanileta katika maono ya Mungu mpaka Yerusalemu, mpaka mlango wa kuingilia ua wa ndani uelekeao upande wa kaskazini; mahali palipokuwa pamewekwa sanamu ya wivu, itiayo wivu. Na tazama, huo utukufu wa Mungu wa Israeli ulikuwapo hapo, sawasawa na maono yale niliyoyaona katika uwanda. Ndipo akaniambia, Mwanadamu, inua macho yako sasa, uangalie upande wa kaskazini. Basi nikainua macho yangu, nikaangalia upande wa kaskazini, na tazama, upande wa kaskazini wa mlango, ilikuwako sanamu ile ya wivu, mahali pale pa kuingilia. Akaniambia, Mwanadamu, je! Unayaona wanayoyafanya, yaani, haya machukizo makubwa wanayoyafanya nyumba ya Israeli hapa, hata niende zangu mbali na patakatifu pangu? Lakini utaona tena machukizo makubwa mengine. Akanileta hata mlango wa ua; nami nilipoangalia, tazama, pana tundu katika ukuta. Ndipo akaniambia, Mwanadamu, toboa sasa katika ukuta huu; nami nilipotoboa, tazama, pana mlango. Akaniambia, Ingia uyaone machukizo mabaya wanayoyafanya hapa. Basi, nikaingia, nikaona; na tazama, kila namna ya wadudu, na wanyama wachukizao, na taswira za vinyago vyote vya nyumba ya Israeli, zimepigwa ukutani pande zote. Na watu sabini wa wazee wa Israeli walikuwa wamesimama na kuzielekea, na katikati yao alisimama Yaazania, mwana wa Shafani; kila mmoja ana chetezo mkononi mwake, na harufu ya moshi wa uvumba ilipaa juu. Kisha akaniambia, Mwanadamu, umeyaona wanayotenda wazee wa nyumba ya Israeli gizani, kila mtu ndani ya vyumba vyake vya sanamu? Maana husema, BWANA hatuoni; BWANA ameiacha nchi hii. Akaniambia tena, Utaona tena machukizo makubwa mengine wanayoyatenda. Ndipo akanileta mpaka mlango wa kuingilia katika nyumba ya BWANA, ulioelekea upande wa kaskazini, na tazama, wanawake wameketi wakimlilia Tamuzi. Akaniambia, Mwanadamu umeyaona haya? Utaona tena machukizo makubwa kuliko hayo. Akanileta mpaka ua wa ndani wa nyumba ya BWANA, na tazama, mlangoni pa hekalu la BWANA, kati ya ukumbi na madhabahu, walikuwako watu kama ishirini na watano, wamelipa kisogo hekalu la BWANA, na nyuso zao zimeelekea upande wa mashariki, nao wanaliabudu jua, kwa kuuelekea upande wa mashariki. Basi, akaniambia, Umeyaona haya, Ee mwanadamu? Je! Ni jambo dogo sana kwa nyumba ya Yuda, wayafanye machukizo wanayoyafanya hapa? Kwa maana wameijaza nchi hii udhalimu, tena wamerejea nyuma ili kunikasirisha; na, tazama, wanaliweka tawi puani. Kwa sababu hiyo mimi nami nitatenda kwa ghadhabu; jicho langu halitaachilia, wala sitaona huruma, na wajapolia masikioni mwangu kwa sauti kuu, sitawasikiliza.