Ezekieli 8:1-18
Ezekieli 8:1-18 BHN
Katika mwaka wa sita, siku ya tano ya mwezi wa sita, nilikuwa nyumbani kwangu pamoja na wazee wa Yuda. Basi, ghafla nikakumbwa na nguvu ya Mwenyezi-Mungu. Nilipotazama, nikaona maono: Kitu kilichofanana na binadamu. Sehemu yake ya chini, iliyoonekana kama ndio kiuno chake, ilikuwa kama moto. Toka kiuno chake kwenda juu alikuwa na mngao kama wa shaba ingaayo. Basi, akanyosha kitu kama mkono, akanishika kwa nywele zangu. Roho ya Mungu ikaninyanyua kati ya ardhi na mbingu, ikanipeleka mpaka Yerusalemu nikiwa katika maono hayo ya Mungu. Nikafika kwenye kiingilio cha lango la ukumbi wa ndani linaloelekea upande wa kaskazini, mahali palipowekwa sanamu iliyomchukiza Mungu. Utukufu wa Mungu wa Israeli ulikuwapo hapo; nao ulikuwa kama utukufu ule niliouona katika maono kule bondeni. Kisha Mungu akaniambia, “Wewe mtu, tazama upande wa kaskazini.” Nami nikatazama upande wa kaskazini, na huko upande wa kaskazini wa lango la madhabahu, niliona ile sanamu iliyomchukiza Mungu. Basi, Mungu akaniambia, “Wewe mtu, je, waona mambo wanayofanya, machukizo makubwa wanayofanya Waisraeli ili wapate kunifukuza kutoka maskani yangu? Tena utaona machukizo mengine makubwa zaidi.” Kisha akanipeleka mpaka lango la ua. Nilipoangalia nikaona tundu ukutani. Naye akaniambia, “Wewe mtu, toboa ukuta huu.” Nami, nikatoboa, nikaona kulikuwa na mlango. Naye akaniambia, “Ingia ndani ukaangalie machukizo mabaya wanayofanya humo.” Basi, nikaingia, nikaona sanamu za wadudu na za wanyama wa kila aina ya kuchukiza na vinyago vyote vya miungu ya Waisraeli, vimechorwa kuuzunguka ukuta. Na mbele ya sanamu hizo walisimama wazee sabini wa watu wa Israeli pamoja na Yaazania mwana wa Shafani. Kila mmoja alikuwa na chetezo mkononi, na moshi wa ubani ulipanda juu. Kisha Mungu akaniambia, “Wewe mtu, umeona wanayotenda wazee wa Waisraeli gizani, kila mtu katika chumba chake cha sanamu. Wanadai ati Mwenyezi-Mungu hatuoni. Mwenyezi-Mungu ameiacha nchi.” Tena akaniambia, “Bado utaona machukizo makubwa zaidi wanayotenda.” Kisha akanichukua mpaka lango la kaskazini la nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Huko kulikuwa na wanawake wameketi wakimwombolezea Tamuzi. Mungu akaniambia: “Wewe mtu, umeyaona hayo? Bado utaona machukizo mengine makubwa kuliko hayo.” Kisha akanipeleka mpaka ua wa ndani ya nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Huko mlangoni mwa hekalu, kati ya ukumbi na madhabahu, walikuwapo wanaume wapatao ishirini na watano, wakilipa kisogo hekalu, na nyuso zao zimeelekea upande wa mashariki. Walikuwa wanaabudu jua wakielekea upande wa mashariki. Mungu akaniambia, “Wewe mtu, je umeyaona mambo hayo? Hata hivyo, watu wa Yuda wanaona machukizo hayo kuwa ni kidogo. Wanaijaza nchi dhuluma na kuzidi kunikasirisha. Angalia jinsi wamekaa hapo, wananiudhi kupita kiasi. Kwa sababu ya mambo hayo watasikia uzito wa ghadhabu yangu. Sitamwacha hata mmoja aponyoke wala sitamwonea huruma mtu yeyote. Hata wakinililia kwa sauti kubwa mimi sitawasikiliza.”