Ezekieli 48:8-35
Ezekieli 48:8-35 Biblia Habari Njema (BHN)
Baada ya eneo la kabila la Yuda, utatenga eneo lenye urefu wa kilomita 12 na upana kama huohuo, kutoka kaskazini hadi kusini, na urefu huohuo kutoka mashariki hadi magharibi, sawasawa na eneo la kabila lolote. Hapo katikati ya eneo hilo patakuwa na maskani ya Mungu. Eneo utakalotenga kwa ajili ya Mwenyezi-Mungu litakuwa lenye urefu wa kilomita kumi na mbili u nusu kwa kilomita 10. Makuhani watakuwa na eneo lao katika eneo hilo. Eneo hilo litakuwa na urefu wa kilomita kumi na mbili u nusu kutoka mashariki hadi magharibi, na kilomita 5 kutoka kaskazini hadi kusini. Maskani ya Mungu itakuwa katikati ya eneo hilo. Eneo hilo litakuwa kwa ajili ya makuhani wa wazawa wa Sadoki, ambao walinitumikia kwa uaminifu na hawakuasi wakati Waisraeli walipoasi kama Walawi walivyofanya. Hilo litakuwa eneo lao maalumu kutoka katika eneo takatifu la nchi, eneo takatifu kabisa, litakalopakana na eneo la Walawi. Nao Walawi, eneo lao litakuwa kusini mwa eneo la makuhani. Eneo hilo litakuwa na urefu wa kilomita kumi na mbili u nusu kutoka mashariki hadi magharibi, na upana kilomita 5 kutokea kaskazini hadi kusini. Hakuna sehemu yoyote ya eneo hilo itakayouzwa au kutolewa kwa mtu yeyote, kwa sababu eneo hilo ni takatifu kwa Mwenyezi-Mungu; nalo ni bora kuliko yote nchini. Ile sehemu ya eneo maalumu iliyobaki, yenye urefu wa kilomita kumi na mbili u nusu na upana kilomita 2.5, hilo ni kwa matumizi ya kawaida ya mji: Mahali pa kuishi na eneo la mashamba. Katikati yake kutakuwa na mji, nao utakuwa wa mraba, kila upande mita 2,250. Kuuzunguka mji, kutakuwa na eneo wazi lenye upana wa mita 125. Eneo ambalo litabaki baada ya kujengwa hekalu, kusini mwa mji, kilomita 5 kwa kilomita 2.5, upande wa mashariki, na kilomita 5 kwa kilomita 2.5 upande wa magharibi, litakuwa eneo la wakulima kwa wakazi wa mji. Wafanyakazi wa mjini wa kabila lolote la Israeli wanaweza kulima katika eneo hilo. Hivyo, eneo lote utakalotenga, yaani eneo takatifu pamoja na eneo la mji, litakuwa la mraba, kilomita kumi na mbili u nusu kila upande. Eneo linalosalia katika pande zote za eneo takatifu na eneo la mji, yaani lile eneo lenye eneo mraba likiwa na kilomita kumi na mbili u nusus kwa kila upande tokea mashariki hadi magharibi, mkabala na maeneo ya makabila, litakuwa la mtawala. Lile eneo takatifu ambamo maskani ya Mungu itakuwa katikati yake, na eneo la Walawi pamoja na lile eneo la mji, yatakuwa katikati ya eneo la mtawala. Eneo la mtawala litakuwa katika mpaka wa eneo la kabila la Yuda na eneo la kabila la Benyamini. Makabila yaliyobaki yatagawiwa maeneo yao hivi: Kabila la Benyamini litapewa eneo kutoka mashariki hadi magharibi. Eneo linalopakana na eneo la Benyamini kutoka upande wa mashariki kuelekea upande wa magharibi litakuwa la kabila la Simeoni. Eneo linalopakana na kabila la Simeoni kutoka upande wa mashariki kuelekea upande wa magharibi litakuwa eneo la kabila la Isakari. Eneo linalopakana na kabila la Isakari kutoka upande wa mashariki kuelekea upande wa magharibi, litakuwa eneo la kabila la Zebuluni. Eneo linalopakana na kabila la Zebuluni, kutoka mashariki kuelekea magharibi, litakuwa eneo la kabila la Gadi. Eneo linalopakana na kabila la Gadi kuelekea kusini, mpaka utatoka mji wa Tamari hadi kwenye chemchemi za Meriba-kadeshi na kupitia upande wa mashariki ya Misri hadi Bahari ya Mediteranea. Hilo ndilo eneo la makabila ya Israeli. Humo ndimo watapewa maeneo yao, kila kabila eneo lake. Bwana Mwenyezi-Mungu amesema. Mji wa Yerusalemu utakuwa na ukuta ambao utakuwa na malango haya ya kutokea na kuingia: Upande wa kaskazini urefu wa ukuta utakuwa mita 2,250. Upande huo wa kaskazini utakuwa na malango matatu: Lango la Reubeni, lango la Yuda na lango la Lawi. Ukuta wa Mashariki utakuwa na urefu wa mita 2,250. Upande huo utakuwa na malango matatu: Lango la Yosefu, lango la Benyamini na lango la Dani. Ukuta wa upande wa kusini utakuwa na urefu wa mita 2,250. Upande huo utakuwa na malango matatu: Lango la Simeoni, lango la Isakari na lango la Zebuluni. Ukuta wa upande wa magharibi utakuwa na urefu wa mita 2,250. Upande huo nao utakuwa na malango matatu: Lango la Gadi, lango la Asheri na lango la Naftali. Jumla ya urefu wa kuta zote nne utakuwa ni mita 9,000. Jina la mji kutokea sasa na kuendelea litakuwa: “Mwenyezi-Mungu Yupo Hapa.”
Ezekieli 48:8-35 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Na mpakani mwa Yuda, toka upande wa mashariki hadi upande wa magharibi, yatakuwapo matoleo mtakayotoa, upana wake mianzi elfu ishirini na tano, na urefu wake sawasawa na moja la mafungu hayo, toka upande wa mashariki hadi upande wa magharibi; na mahali patakatifu ni katikati yake. Matoleo hayo, mtakayomtolea BWANA, urefu wake ni mianzi elfu ishirini na tano, na upana wake elfu kumi. Maeneo hayo matakatifu yatakuwa kwa ajili ya makuhani; upande wa kaskazini urefu wake mianzi elfu ishirini na tano, na upande wa magharibi upana wake mianzi elfu kumi, na upande wa mashariki upana wake mianzi elfu kumi, na upande wa kusini urefu wake mianzi elfu ishirini na tano; na mahali patakatifu pa BWANA patakuwa katikati yake. Patakuwa kwa makuhani wa wana wa Sadoki, waliotakasika, waliofuata maagizo yangu, wasioasi, wana wa Israeli walipoasi, kama Walawi walivyoasi. Na matoleo hayo ya nchi yatolewayo, yatakuwa kwao kitu kitakatifu sana, karibu na mpaka wa Walawi. Na kuukabili mpaka wa makuhani, Walawi watakuwa na fungu, urefu wake mianzi elfu ishirini na tano, na upana wake mianzi elfu kumi; urefu wote utakuwa mianzi elfu ishirini na tano, na upana wake mianzi elfu kumi. Wala hawatauza sehemu yake, wala kuibadili, wala hawatawapa wengine malimbuko ya nchi; maana ni matakatifu kwa BWANA. Na mianzi elfu tano iliyosalia katika upana, kuikabili hiyo elfu ishirini na tano, itatumiwa na watu wote, kwa huo mji, na kwa maskani, na kwa viunga, na huo mji utakuwa katikati yake. Na vipimo vyake ni hivi; upande wa kaskazini mianzi elfu nne na mia tano, na upande wa kusini mianzi elfu nne na mia tano, na upande wa mashariki mianzi elfu nne na mia tano, na upande wa magharibi mianzi elfu nne na mia tano. Nao mji utakuwa na malisho; upande wa kaskazini mianzi mia mbili na hamsini, na upande wa kusini mianzi mia mbili na hamsini, na upande wa mashariki mianzi mia mbili na hamsini, na upande wa magharibi mianzi mia mbili na hamsini. Na mabaki ya urefu wake yaelekeayo matoleo matakatifu, upande wa mashariki yatakuwa mianzi elfu kumi, na upande wa magharibi mianzi elfu kumi; nayo yatakuwa sawasawa na matoleo matakatifu; na mazao yake yatakuwa ni chakula cha watu wafanyao kazi humo mjini. Na hao wafanyao kazi mjini, wa kabila zote za Israeli, watailima nchi hiyo. Matoleo yote yatakuwa mianzi elfu ishirini na tano, kwa mianzi elfu ishirini na tano; mtatoa matoleo matakatifu, nchi ya mraba, pamoja na milki ya mji. Nayo mabaki yake yatakuwa ya huyo mkuu, upande huu na upande huu wa matoleo matakatifu, na milki ya mji, kuikabili hiyo mianzi elfu ishirini na tano ya matoleo, kuelekea mpaka wa mashariki; tena upande wa magharibi kuikabili hiyo mianzi elfu ishirini na tano, upande wa kuelekea mpaka wa magharibi; sawa na yale mafungu, hayo yatakuwa ya huyo mkuu; na matoleo matakatifu na mahali patakatifu pa nyumba patakuwa katikati yake. Tena tokea milki ya Walawi, na tokea milki ya mji, kwa kuwa ni katikati ya nchi iliyo ya mkuu, katikati ya mpaka wa Yuda na mpaka wa Benyamini, itakuwa ya mkuu. Na katika habari za kabila zilizosalia; toka upande wa mashariki hadi upande wa magharibi; Benyamini, fungu moja. Tena mpakani mwa Benyamini, toka upande wa mashariki hata upande wa magharibi; Simeoni, fungu moja. Tena mpakani mwa Simeoni, toka upande wa mashariki hata upande wa magharibi; Isakari, fungu moja. Na mpakani mwa Isakari, toka upande wa mashariki hadi upande wa magharibi; Zabuloni, fungu moja. Na mpakani mwa Zabuloni, toka upande wa mashariki hata upande wa magharibi; Gadi, fungu moja. Na mpakani mwa Gadi, upande wa kusini kuelekea kusini, mpaka wake utakuwa toka Tamari, mpaka maji ya Meriba-Kadeshi, mpaka kijito cha Misri, mpaka bahari kubwa. Hiyo ndiyo nchi mtakayoyagawanyia makabila ya Israeli, kuwa urithi wao, na hayo ndiyo mafungu yao, asema Bwana MUNGU. Na matokeo ya mji ndiyo haya; upande wa kaskazini, mianzi elfu nne na mia tano, kwa kipimo; na malango ya mji yatatajwa kwa majina ya makabila ya Israeli, malango matatu upande wa kaskazini; lango la Reubeni, moja; lango la Yuda, moja; na lango la Lawi, moja. Na upande wa mashariki, mianzi elfu nne na mia tano, kwa kipimo; na malango matatu; lango la Yusufu, lango la Benyamini; lango la Dani. Na upande wa kusini, mianzi elfu nne na mia tano kwa kupima; na malango matatu; lango la Simeoni; lango la Isakari, lango la Zabuloni. Na upande wa magharibi, mianzi elfu nne na mia tano; pamoja na malango yake matatu; lango la Gadi, lango la Asheri; na lango la Naftali. Kuuzunguka ni mianzi elfu kumi na nane; na jina la mji huo tangu siku hiyo litakuwa hili, BWANA yupo.
Ezekieli 48:8-35 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Na mpakani mwa Yuda, toka upande wa mashariki hata upande wa magharibi, yatakuwapo matoleo mtakayotoa, upana wake mianzi ishirini na tano elfu, na urefu wake sawasawa na moja la mafungu hayo, toka upande wa mashariki hata upande wa magharibi; na mahali patakatifu ni katikati yake. Matoleo hayo, mtakayomtolea BWANA, urefu wake ni mianzi ishirini na tano elfu, na upana wake elfu kumi. Matoleo hayo matakatifu yatakuwa kwa watu hawa, kwa makuhani; upande wa kaskazini urefu wake ishirini na tano elfu, na upande wa magharibi upana wake elfu kumi, na upande wa mashariki upana wake elfu kumi, na upande wa kusini urefu wake ishirini na tano elfu; na mahali patakatifu pa BWANA patakuwa katikati yake. Patakuwa kwa makuhani wa wana wa Sadoki, waliotakasika, walioulinda ulinzi wangu, wasioasi, wana wa Israeli walipoasi, kama Walawi walivyoasi. Na matoleo hayo ya nchi yatolewayo, yatakuwa kwao kitu kitakatifu sana, karibu na mpaka wa Walawi. Na kuukabili mpaka wa makuhani, Walawi watakuwa na fungu, urefu wake ishirini na tano elfu, na upana wake elfu kumi; urefu wote utakuwa ishirini na tano elfu, na upana wake elfu kumi. Wala hawatauza sehemu yake, wala kuibadili, wala hawatawapa wengine malimbuko ya nchi; maana ni matakatifu kwa BWANA. Na mianzi elfu tano iliyosalia katika upana, kuikabili hiyo ishirini na tano elfu, itatumiwa na watu wote, kwa huo mji, na kwa maskani, na kwa viunga, na huo mji utakuwa katikati yake. Na vipimo vyake ni hivi; upande wa kaskazini elfu nne na mia tano, na upande wa kusini elfu nne na mia tano, na upande wa mashariki elfu nne na mia tano, na upande wa magharibi elfu nne na mia tano. Nao mji utakuwa na malisho; upande wa kaskazini mia mbili na hamsini, na upande wa kusini mia mbili na hamsini, na upande wa mashariki mia mbili na hamsini, na upande wa magharibi mia mbili na hamsini. Na mabaki ya urefu wake yaelekeayo matoleo matakatifu, upande wa mashariki yatakuwa elfu kumi, na upande wa magharibi elfu kumi; nayo yatakuwa sawasawa na matoleo matakatifu; na mazao yake yatakuwa ni chakula cha watu wafanyao kazi humo mjini. Na hao wafanyao kazi mjini, wa kabila zote za Israeli, watailima nchi hiyo. Matoleo yote yatakuwa ishirini na tano elfu, kwa ishirini na tano elfu; mtatoa matoleo matakatifu, nchi ya mraba, pamoja na milki ya mji. Nayo mabaki yake yatakuwa ya huyo mkuu, upande huu na upande huu wa matoleo matakatifu, na milki ya mji, kuikabili hiyo ishirini na tano elfu ya matoleo, kuelekea mpaka wa mashariki; tena upande wa magharibi kuikabili hiyo ishirini na tano elfu, upande wa kuelekea mpaka wa magharibi; sawa na yale mafungu, hayo yatakuwa ya huyo mkuu; na matoleo matakatifu na mahali patakatifu pa nyumba patakuwa katikati yake. Tena tokea milki ya Walawi, na tokea milki ya mji, kwa kuwa ni katikati ya nchi iliyo ya mkuu, katikati ya mpaka wa Yuda na mpaka wa Benyamini, itakuwa ya mkuu. Na katika habari za kabila zilizosalia; toka upande wa mashariki hata upande wa magharibi; Benyamini, fungu moja. Tena mpakani mwa Benyamini, toka upande wa mashariki hata upande wa magharibi; Simeoni, fungu moja. Tena mpakani mwa Simeoni, toka upande wa mashariki hata upande wa magharibi; Isakari, fungu moja. Na mpakani mwa Isakari, toka upande wa mashariki hata upande wa magharibi; Zabuloni, fungu moja. Na mpakani mwa Zabuloni, toka upande wa mashariki hata upande wa magharibi; Gadi, fungu moja. Na mpakani mwa Gadi, upande wa kusini kuelekea kusini, mpaka wake utakuwa toka Tamari, mpaka maji ya Meriba-Kadeshi, mpaka kijito cha Misri, mpaka bahari kubwa. Hiyo ndiyo nchi mtakayozigawanyia kabila za Israeli, kuwa urithi wao, na hayo ndiyo mafungu yao, asema Bwana MUNGU. Na matokeo ya mji ndiyo haya; upande wa kaskazini, mianzi elfu nne na mia tano, kwa kupima; na malango ya mji yatatajwa kwa majina ya kabila za Israeli, malango matatu upande wa kaskazini; lango la Reubeni, moja; lango la Yuda, moja; na lango la Lawi, moja. Na upande wa mashariki, elfu nne na mia tano, kwa kupima; na malango matatu; lango la Yusufu, moja; lango la Benyamini, moja; lango la Dani, moja. Na upande wa kusini, elfu nne na mia tano kwa kupima; na malango matatu; lango la Simeoni, moja; lango la Isakari, moja; lango la Zabuloni, moja. Na upande wa magharibi, elfu nne na mia tano; pamoja na malango yake matatu; lango la Gadi, moja; lango la Asheri, moja; na lango la Naftali, moja. Kuuzunguka ni mianzi kumi na nane elfu; na jina la mji huo tangu siku hiyo litakuwa hili, BWANA yupo hapa.
Ezekieli 48:8-35 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
“Kupakana na nchi ya Yuda kuanzia mashariki mpaka magharibi itakuwa ndiyo sehemu utakayoitoa ili kuwa toleo maalum. Itakuwa na upana wa dhiraa elfu ishirini na tano, nao urefu wake kuanzia mashariki hadi magharibi utakuwa sawa na sehemu moja ya kabila; mahali patakatifu patakuwa katikati ya eneo hilo. “Hiyo sehemu maalum mtakayotoa kwa BWANA itakuwa na urefu wa dhiraa elfu ishirini na tano, na upana wa dhiraa elfu kumi. Hii itakuwa ni sehemu takatifu kwa ajili ya makuhani. Itakuwa na urefu wa dhiraa elfu ishirini na tano upande wa kaskazini, upana wa dhiraa elfu kumi upande wa magharibi, dhiraa elfu kumi upande wa mashariki, na urefu wa dhiraa elfu ishirini na tano upande wa kusini. Katikati yake patakuwa mahali patakatifu pa BWANA. Hii itakuwa kwa ajili ya makuhani waliowekwa wakfu, Wasadoki, waliokuwa waaminifu katika kunitumikia, nao hawakupotoka kama Walawi walivyofanya wakati Waisraeli walipopotoka. Itakuwa toleo maalum kwao kutoka sehemu takatifu ya nchi, yaani sehemu takatifu sana, inayopakana na nchi ya Walawi. “Kando ya nchi ya makuhani, Walawi watakuwa na mgawo wa urefu wa dhiraa elfu ishirini na tano, na upana wa dhiraa elfu kumi. Urefu wake utakuwa jumla dhiraa elfu ishirini na tano, na upana wa dhiraa elfu kumi. Hawataruhusiwa kuuza wala kuibadilisha hata mojawapo. Hii ndiyo sehemu nzuri ya nchi kuliko nyingine zote, hivyo haitakuwa mikononi mwa watu wengine, kwa sababu ni takatifu kwa BWANA. “Eneo linalobaki lenye upana wa dhiraa elfu tano, na urefu wa dhiraa elfu ishirini na tano litakuwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida ya mji, kwa ajili ya ujenzi wa nyumba na maeneo ya malisho. Mji utakuwa katikati yake nao utakuwa na vipimo hivi: upande wa kaskazini dhiraa elfu nne na mia tano, upande wa kusini dhiraa elfu nne na mia tano, upande wa mashariki dhiraa elfu nne na mia tano, na upande wa magharibi dhiraa elfu nne na mia tano. Eneo la malisho kwa ajili ya mji litakuwa na eneo la dhiraa mia mbili na hamsini upande wa kaskazini, dhiraa mia mbili na hamsini upande wa kusini, dhiraa mia mbili na hamsini upande wa mashariki, na dhiraa mia mbili na hamsini upande wa magharibi. Eneo linalobaki, linalopakana na sehemu takatifu likiwa na urefu sawa nalo, litakuwa dhiraa elfu kumi upande wa mashariki, na dhiraa elfu kumi upande wa magharibi. Mazao yake yatawapa watumishi wa mji chakula. Watumishi wa mji wanaolima shamba hili watatoka katika makabila yote ya Israeli. Eneo lote la hiyo sehemu litakuwa mraba, yaani dhiraa elfu ishirini na tano kila upande. Kama toleo maalum mtatenga sehemu takatifu, pamoja na milki ya mji. “Eneo linalobaki pande mbili za eneo linalofanya sehemu takatifu na milki ya mji litakuwa mali ya mkuu anayetawala. Eneo hili litaenea upande wa mashariki, kuanzia kwenye dhiraa elfu ishirini na tano za sehemu takatifu hadi mpaka wa mashariki, na kuelekea upande wa magharibi, kuanzia kwenye dhiraa elfu ishirini na tano hadi mpaka wa magharibi. Maeneo haya mawili yanayoenda sambamba na urefu wa sehemu za makabila yatakuwa ya mkuu anayetawala, na sehemu ile takatifu pamoja na mahali patakatifu pa Hekalu itakuwa katikati yake. Kwa hiyo milki ya Walawi na milki ya mji vitakuwa katikati ya eneo lile ambalo ni mali ya mkuu anayetawala. Eneo la mkuu anayetawala litakuwa kati ya mpaka wa Yuda na mpaka wa Benyamini. “Kuhusu makabila yaliyobaki: “Benyamini atakuwa na sehemu moja; itakayoanzia upande wa mashariki hadi upande wa magharibi. Simeoni atakuwa na sehemu moja; itakayopakana na nchi ya Benyamini kuanzia mashariki hadi magharibi. Isakari atakuwa na sehemu moja; itakayopakana na nchi ya Simeoni kuanzia mashariki hadi magharibi. Zabuloni atakuwa na sehemu moja; itakayopakana na nchi ya Isakari kuanzia mashariki hadi magharibi. Gadi atakuwa na sehemu moja; itakayopakana na nchi ya Zabuloni kuanzia mashariki hadi magharibi. Mpaka wa kusini wa Gadi utapita kusini kuanzia Tamari hadi maji ya Meriba-Kadeshi, kisha kupitia upande wa Kijito cha Misri hadi Bahari Kuu. “Hii ndiyo nchi mtakayogawanya kuwa urithi kwa makabila ya Israeli, nazo zitakuwa sehemu zao,” asema BWANA Mwenyezi. “Haya yatakuwa ndiyo malango ya mji ya kutokea: “Kuanzia upande wa kaskazini, ambayo urefu wake ni dhiraa elfu nne na mia tano, utakuwa na malango matatu, malango hayo ya mji yatapewa majina ya makabila ya Israeli. Malango hayo matatu ya upande wa kaskazini moja litakuwa lango la Reubeni, lango la Yuda na lango la Lawi. Upande wa mashariki, wenye urefu wa dhiraa elfu nne na mia tano, utakuwa na malango matatu: lango la Yusufu, lango la Benyamini na lango la Dani. Upande wa kusini, wenye urefu wa dhiraa elfu nne na mia tano, utakuwa na malango matatu: lango la Simeoni, lango la Isakari na lango la Zabuloni. Upande wa magharibi, wenye urefu wa dhiraa elfu nne na mia tano, utakuwa na malango matatu: lango la Gadi, lango la Asheri na lango la Naftali. “Urefu wote kuzunguka utakuwa dhiraa elfu kumi na nane.