Ezekieli 48:8-35
Ezekieli 48:8-35 NENO
“Kupakana na nchi ya Yuda kuanzia mashariki mpaka magharibi itakuwa ndiyo sehemu utakayoitoa ili kuwa toleo maalum. Itakuwa na upana wa dhiraa elfu ishirini na tano, nao urefu wake kuanzia mashariki hadi magharibi utakuwa sawa na sehemu moja ya kabila; mahali patakatifu patakuwa katikati ya eneo hilo. “Hiyo sehemu maalum mtakayotoa kwa Mwenyezi Mungu itakuwa na urefu wa dhiraa elfu ishirini na tano, na upana wa dhiraa elfu kumi. Hii itakuwa ni sehemu takatifu kwa ajili ya makuhani. Itakuwa na urefu wa dhiraa elfu ishirini na tano upande wa kaskazini, upana wa dhiraa elfu kumi upande wa magharibi, dhiraa elfu kumi upande wa mashariki, na urefu wa dhiraa elfu ishirini na tano upande wa kusini. Katikati yake patakuwa mahali patakatifu pa Mwenyezi Mungu. Hii itakuwa kwa ajili ya makuhani waliowekwa wakfu, Wasadoki, waliokuwa waaminifu katika kunitumikia, nao hawakupotoka kama Walawi walivyofanya wakati Waisraeli walipopotoka. Itakuwa toleo maalum kwao kutoka sehemu takatifu ya nchi, yaani sehemu takatifu sana, inayopakana na nchi ya Walawi. “Kando ya nchi ya makuhani, Walawi watakuwa na mgawo wa urefu wa dhiraa elfu ishirini na tano, na upana wa dhiraa elfu kumi. Urefu wake utakuwa jumla dhiraa elfu ishirini na tano, na upana wa dhiraa elfu kumi. Hawataruhusiwa kuuza wala kuibadilisha hata mojawapo. Hii ndiyo sehemu nzuri ya nchi kuliko nyingine zote, hivyo haitakuwa mikononi mwa watu wengine, kwa sababu ni takatifu kwa Mwenyezi Mungu. “Eneo linalobaki lenye upana wa dhiraa elfu tano, na urefu wa dhiraa elfu ishirini na tano litakuwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida ya mji, kwa ajili ya ujenzi wa nyumba na maeneo ya malisho. Mji utakuwa katikati yake nao utakuwa na vipimo hivi: upande wa kaskazini dhiraa elfu nne na mia tano, upande wa kusini dhiraa elfu nne na mia tano, upande wa mashariki dhiraa elfu nne na mia tano, na upande wa magharibi dhiraa elfu nne na mia tano. Eneo la malisho kwa ajili ya mji litakuwa na eneo la dhiraa mia mbili na hamsini upande wa kaskazini, dhiraa mia mbili na hamsini upande wa kusini, dhiraa mia mbili na hamsini upande wa mashariki, na dhiraa mia mbili na hamsini upande wa magharibi. Eneo linalobaki, linalopakana na sehemu takatifu likiwa na urefu sawa nalo, litakuwa dhiraa elfu kumi upande wa mashariki, na dhiraa elfu kumi upande wa magharibi. Mazao yake yatawapa watumishi wa mji chakula. Watumishi wa mji wanaolima shamba hili watatoka katika makabila yote ya Israeli. Eneo lote la hiyo sehemu litakuwa mraba, yaani dhiraa elfu ishirini na tano kila upande. Kama toleo maalum mtatenga sehemu takatifu, pamoja na milki ya mji. “Eneo linalobaki pande mbili za eneo linalofanya sehemu takatifu na milki ya mji litakuwa mali ya mkuu anayetawala. Eneo hili litaenea upande wa mashariki, kuanzia kwenye dhiraa elfu ishirini na tano za sehemu takatifu hadi mpaka wa mashariki, na kuelekea upande wa magharibi, kuanzia kwenye dhiraa elfu ishirini na tano hadi mpaka wa magharibi. Maeneo haya mawili yanayoenda sambamba na urefu wa sehemu za makabila yatakuwa ya mkuu anayetawala, na sehemu ile takatifu pamoja na mahali patakatifu pa Hekalu itakuwa katikati yake. Kwa hiyo milki ya Walawi na milki ya mji vitakuwa katikati ya eneo lile ambalo ni mali ya mkuu anayetawala. Eneo la mkuu anayetawala litakuwa kati ya mpaka wa Yuda na mpaka wa Benyamini. “Kuhusu makabila yaliyobaki: “Benyamini atakuwa na sehemu moja; itakayoanzia upande wa mashariki hadi upande wa magharibi. Simeoni atakuwa na sehemu moja; itakayopakana na nchi ya Benyamini kuanzia mashariki hadi magharibi. Isakari atakuwa na sehemu moja; itakayopakana na nchi ya Simeoni kuanzia mashariki hadi magharibi. Zabuloni atakuwa na sehemu moja; itakayopakana na nchi ya Isakari kuanzia mashariki hadi magharibi. Gadi atakuwa na sehemu moja; itakayopakana na nchi ya Zabuloni kuanzia mashariki hadi magharibi. Mpaka wa kusini wa Gadi utapita kusini kuanzia Tamari hadi maji ya Meriba-Kadeshi, kisha kupitia upande wa Kijito cha Misri hadi Bahari Kuu. “Hii ndiyo nchi mtakayogawanya kuwa urithi kwa makabila ya Israeli, nazo zitakuwa sehemu zao,” asema Bwana Mungu Mwenyezi. “Haya yatakuwa ndiyo malango ya mji ya kutokea: “Kuanzia upande wa kaskazini, ambayo urefu wake ni dhiraa elfu nne na mia tano, utakuwa na malango matatu, malango hayo ya mji yatapewa majina ya makabila ya Israeli. Malango hayo matatu ya upande wa kaskazini moja litakuwa lango la Reubeni, lango la Yuda na lango la Lawi. Upande wa mashariki, wenye urefu wa dhiraa elfu nne na mia tano, utakuwa na malango matatu: lango la Yusufu, lango la Benyamini na lango la Dani. Upande wa kusini, wenye urefu wa dhiraa elfu nne na mia tano, utakuwa na malango matatu: lango la Simeoni, lango la Isakari na lango la Zabuloni. Upande wa magharibi, wenye urefu wa dhiraa elfu nne na mia tano, utakuwa na malango matatu: lango la Gadi, lango la Asheri na lango la Naftali. “Urefu wote kuzunguka utakuwa dhiraa elfu kumi na nane.