Ezekieli 40:1-27
Ezekieli 40:1-27 Biblia Habari Njema (BHN)
Mwaka wa ishirini na tano tangu kuhamishwa kwetu, siku ya kumi ya mwezi wa kwanza, siku hiyo niliusikia uzito wa nguvu ya Mwenyezi-Mungu. Ilikuwa mwaka wa kumi na nne tangu mji wa Yerusalemu ulipotekwa. Basi, nikiwa katika njozi Mwenyezi-Mungu alinichukua mpaka nchini Israeli, akaniweka juu ya mlima mrefu sana, na upande wa kusini kulikuwa na majengo yaliyoonekana kama mji. Basi, alinipeleka huko, nami nikamwona mtu aliyeonekana anangara kama shaba. Mikononi mwake mtu huyo alikuwa na kamba ya kitani ya kupimia pamoja na ufito wa kupimia, naye alikuwa amesimama karibu na lango. Basi, akaniambia: “Wewe mtu! Tazama vizuri na kusikiliza kwa makini. Zingatia kwa moyo uone kila kitu nitakachokuonesha maana umeletwa hapa ili nikuoneshe kitu. Unapaswa kuwatangazia watu wa Israeli kila kitu utakachoona.” Basi, huko, niliona hekalu nalo lilikuwa limezungukwa na ukuta upande wa nje. Yule mtu akauchukua ufito wake wa kupimia ambao ulikuwa na urefu wa mita 3, akaupima ule ukuta. Ukuta huo ulikuwa na kimo cha mita 3 na unene wa mita 3. Kisha, akaenda kwenye lango la mashariki akapanda ngazi na akiwa juu akapima kizingiti cha lango ambacho kilikuwa na kina mita 3. Kulikuwa na vyumba vya walinzi kila upande wa nafasi ya kupitia na kila kimoja kilikuwa cha mraba: Urefu mita 3 upana mita 3. Kuta zilizotenganisha vyumba hivyo zilikuwa na unene mita 2.5. Kulikuwa na ukumbi mrefu wa mita 3 ambao ulielekea kwenye chumba kikubwa mkabala na hekalu. Yule mtu akakipima pia chumba hicho, nacho kilikuwa na kina mita 4. Halafu akapima kuta zake za nje zikaonekana zina unene wa mita moja. Sehemu ya ndani ya lango ilikuwa sehemu iliyokuwa karibu zaidi na hekalu. Kulikuwa na sehemu ya kuingilia iliyokuwa na vyumba vitatu vya walinzi, kila upande na vyote vilikuwa na ukubwa uleule; nazo kuta zilizovitenganisha zilikuwa na unene uleule. Kisha, yule mtu akapima upana wa nafasi ya kupitia katika lango. Upana wake ulikuwa mita 6.5. Ukubwa wote wa ukumbi wa katikati wa kupitia ulikuwa mita 5. Mbele ya vyumba vya walinzi ambavyo vilikuwa mraba: Mita 3 kwa 3, kulikuwa na ukuta mfupi kama kizuizi ukiwa na kimo cha sentimita 50 na unene sentimita 50. Yule mtu akapima umbali kutoka ukuta wa nyuma wa chumba kimojawapo hadi kwenye ukuta wa nyuma ya chumba upande wa pili penye nafasi ya kupitia, akapata mitakumi na mbili u nusu. Chumba cha mwisho kabisa kilielekea kwenye ua. Akakipima chumba hicho nacho kilikuwa na upana mita 10. Kutoka mbele ya lango kwenye mwingilio mpaka ukumbi wa ndani wa lango kulikuwa na mita 25. Kulikuwa na matundu madogomadogo kwenye miimo ya nje ya vyumba vyote na hata kwenye kuta zilizotenganisha vyumba. Kulikuwa na michoro ya mitende kwenye miimo ya ndani iliyoelekea ukumbi wa kupitia. Kisha yule mtu akanipeleka mpaka ua wa nje ya hekalu. Huko kulikuwa na vyumba thelathini kuuzunguka ukuta wa nje na mbele ya vyumba hivyo kulikuwa na sakafu ya mawe. Sakafu hiyo ilitandazwa kuzunguka malango kwa kufuatana na urefu wa malango hayo; hiyo ilikuwa sakafu ya chini. Baadaye, yule mtu akapima umbali wa njia iliyokuwa ikitoka kwenye ua wa ndani wa sehemu ya chini ikielekea nje ya ua huo, akapata mita 50. Kisha, yule mtu akapima urefu na upana wa lango la upande wa kaskazini wa ua wa nje. Kulikuwa na vyumba vitatu vya walinzi kila upande wa lango, vipimo vya miimo yake na matao yake vilikuwa kama vile vya lango la kwanza. Urefu wote wa ile njia ulikuwa kwa jumla mita 25 na upana wake mita kumi na mbili u nusu. Chumba cha kuingilia na madirisha na matao yake, pia ile mitende iliyochorwa ukutani, vyote vilifanana na vile vya lango la mashariki. Hapo palikuwa na ngazi saba za kupandia kwenye lango, na matao yake yalikuwa mbele yake. Kutoka hapo penye njia ya kuingilia ya kaskazini na kuvuka huo ua moja kwa moja kulikuwa na njia nyingine ya kuingilia iliyoelekea kwenye ua wa ndani, kama ilivyokuwa upande wa mashariki. Yule mtu alipima urefu wa kutoka njia mpaka njia, akapata mita 50. Yule mtu akanichukua upande wa kusini; huko nako kulikuwako lango; alipima miimo yake na ukumbi na vipimo vyake vilikuwa sawa na miimo na kumbi nyingine. Kulikuwa na madirisha pande zote kama ilivyokuwa katika vyumba vingine. Urefu wake ulikuwa mita 25 na upana wake mita kumi na mbili u nusu. Kulikuwa na ngazi saba za kupandia kwenye njia hiyo ya kuingilia na mwishoni mwake kulikuwa na ukumbi uliokuwa mkabala na ua. Kulikuwa na michoro ya mitende kwenye kuta za ndani zilizokuwa mkabala na hiyo njia ya kuingilia. Mkabala na njia hiyo ya kuingilia kulikuwa na njia ya kuingilia kwenye ua wa ndani. Yule mtu akapima urefu kati ya hizo njia, akapata mita 50.
Ezekieli 40:1-27 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Katika mwaka wa ishirini na tano wa kuhamishwa kwetu, mwanzo wa mwaka, siku ya kumi ya mwezi, katika mwaka wa kumi na nne baada ya kupigwa mji, siku iyo hiyo, mkono wa BWANA ulikuwa juu yangu, akanileta huko. Katika maono ya Mungu alinileta mpaka nchi ya Israeli, akaniweka juu ya mlima mrefu sana, ambao juu yake palikuwapo kana kwamba ni umbo la mji upande wa kusini. Akanileta huko, na tazama, alikuwapo mtu, ambaye kuonekana kwake kulikuwa kama kuonekana kwa shaba, naye alikuwa na uzi wa kitani mkononi mwake, na mwanzi wa kupimia; akasimama karibu na lango. Mtu yule akaniambia, Mwanadamu, tazama kwa macho yako, sikia kwa masikio yako, ukaweke moyoni mwako, yote nitakayokuonesha; maana umeletwa hapa kusudi nikuoneshe haya; tangaza habari ya yote utakayoyaona kwa nyumba ya Israeli. Na, tazama, kulikuwa na ukuta nje ya nyumba pande zote, na katika mkono wa mtu yule mwanzi wa kupimia, urefu wake dhiraa sita, kila dhiraa, dhiraa na shubiri; basi akaupima upana wa jengo lile, mwanzi mmoja, na urefu wake, mwanzi mmoja. Kisha akaenda hadi katika lango lielekealo upande wa mashariki, akapanda madaraja yake; akakipima kizingiti cha lango; upana wake mwanzi mmoja; na kizingiti cha pili, upana wake mwanzi mmoja. Na kila chumba, upana wake mwanzi mmoja, na urefu wake mwanzi mmoja; na nafasi iliyokuwa kati ya vyumba ni dhiraa tano; na kizingiti cha lango lililokuwa karibu na ukumbi wa lango lililoielekea nyumba, mwanzi mmoja. Akaupima na ukumbi wa lango lililoielekea nyumba, mwanzi mmoja. Kisha akaupima ukumbi wa lango, dhiraa nane; na miimo yake, dhiraa mbili; na ukumbi wa lango uliielekea nyumba. Na vyumba vya walinzi, vya lango upande wa mashariki, vilikuwa vitatu upande huu, na vitatu upande huu; vyote vitatu vya kipimo kimoja; nayo miimo ilikuwa na kipimo kimoja, upande huu na upande huu. Akaupima upana wa mahali pa kuliingilia lango, dhiraa kumi; na urefu wa lango, dhiraa kumi na tatu. Na mpaka, mbele ya vile vyumba, dhiraa moja upande huu, na mpaka, dhiraa moja upande huu; na vile vyumba, dhiraa sita upande huu, na dhiraa sita upande huu. Akalipima lango, toka paa la chumba kimoja hadi paa la chumba cha pili, upana wa dhiraa ishirini na tano; mlango mmoja ukielekea mlango wa pili. Akafanya miimo pia, dhiraa sitini; na uwanda uliufikia mwimo, lango lile likizungukwa pande zote. Na toka mahali palipo mbele ya lango, penye maingilio yake, hata mahali palipo mbele ya ukumbi wa ndani ya lango, dhiraa hamsini. Na kwa vile katika vyumba palikuwa na madirisha yaliyofungwa, na kwa miimo yake ndani ya lango pande zote, na kwa matao yake vivyo hivyo; na madirisha yalikuwako, pande zote upande wa ndani, tena palikuwa na mitende juu ya kila mwimo. Ndipo akanileta mpaka katika ua wa nje, na tazama, palikuwa na vyumba, na sakafu iliyofanyizwa kwa ule ua pande zote; vyumba thelathini vilikuwako juu ya sakafu ile. Na ile sakafu ilikuwa kando ya malango, urefu wake sawasawa na urefu wa malango, yaani, sakafu ya chini. Kisha akaupima upana, toka mahali palipokuwa mbele ya lango la chini hadi mahali palipokuwa mbele ya ua wa ndani, nje yake, dhiraa mia moja upande wa mashariki, na upande wa kaskazini. Nalo lango la ua wa nje, lililoelekea kaskazini, akalipima urefu wake, na upana wake. Na vyumba vyake vya walinzi vilikuwa vitatu upande huu, na vitatu upande huu; na miimo yake, na matao yake, kipimo chake ni sawasawa na kipimo cha lango la kwanza; urefu wake dhiraa hamsini, na upana wake dhiraa ishirini na tano. Na madirisha yake, na matao yake, na mitende yake, kipimo chake ni sawasawa na kipimo cha lango lililoelekea upande wa mashariki; nao hupanda kwa madaraja saba; na matao yake yalikuwa mbele yake. Na ule ua wa ndani ulikuwa na lango lililoelekea lile lango la pili, upande wa kaskazini, na upande wa mashariki; akapima toka lango hadi lango, dhiraa mia moja. Akanileta mpaka upande wa kusini, na tazama, lango lililoelekea kusini; akaipima miimo yake, na matao yake, sawasawa na vipimo hivyo. Tena palikuwa na madirisha ndani yake, na katika matao yake pande zote kama madirisha hayo; urefu wake dhiraa hamsini, na upana wake dhiraa ishirini na tano. Tena palikuwa na madaraja saba ya kulipandia, na matao yake yalikuwa mbele yake; nalo lilikuwa na mitende, mmoja upande huu, na mmoja upande huu, juu ya miimo yake. Tena ua wa ndani ulikuwa na lango, lililoelekea kusini; akapima toka lango hadi lango, kwa kuelekea upande wa kusini, dhiraa mia moja.
Ezekieli 40:1-27 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Katika mwaka wa ishirini na tano wa uhamisho wetu, mwanzoni mwa huo mwaka, siku ya kumi ya mwezi, katika mwaka wa kumi na nne baada ya kuanguka kwa mji, siku hiyo hiyo mkono wa BWANA ulikuwa juu yangu, naye akanipeleka huko. Nikiwa katika maono ya Mungu alinichukua mpaka nchi ya Israeli, naye akaniweka kwenye mlima mrefu sana, ambako upande wa kusini kulikuwepo baadhi ya majengo ambayo yalionekana kama mji. Akanipeleka huko, nami nikamwona mtu ambaye kuonekana kwake kulikuwa kama kuonekana kwa shaba. Alikuwa amesimama kwenye lango akiwa na kamba ya kitani na ufito wa kupimia mkononi mwake. Mtu huyo akaniambia, “Mwanadamu, angalia kwa macho yako na usikie kwa masikio yako nawe uzingatie kitu nitakachokuonyesha, kwa kuwa ndiyo sababu umeletwa hapa. Iambie nyumba ya Israeli kila kitu utakachoona.” Nikaona ukuta uliozunguka eneo lote la Hekalu. Ule ufito wa kupimia uliokuwa mkononi mwa yule mtu ulikuwa na urefu wa dhiraa ndefu sita, yaani, dhiraa ndefu ni sawa na dhiraa na nyanda nne, akapima ule ukuta. Ukuta huo ulikuwa na unene wa dhiraa ndefu sita na kimo cha dhiraa ndefu sita. Kisha akaenda kwenye lango linaloelekea mashariki. Akapanda ngazi zake akapima kizingiti cha lango, nacho kilikuwa na kina cha huo ufito. Vyumba vya kupumzikia vya walinzi vilikuwa na urefu wa huo ufito mmoja na upana wa huo ufito, kuta zilizogawa vyumba hivyo vya mapumziko zilikuwa na unene wa dhiraa tano. Nacho kizingiti cha lango lililokuwa karibu na ukumbi unaoelekea hekaluni ulikuwa na kina cha huo ufito. Kisha akapima baraza ya njia ya lango, ambayo ilikuwa na kina cha dhiraa nane na miimo yake ilikuwa na unene wa dhiraa mbili. Baraza ya lango ilielekea Hekalu. Ndani ya lango la mashariki kulikuwepo vyumba vitatu vya kupumzikia kila upande, vyote vitatu vilikuwa na vipimo vilivyo sawa, nazo nyuso za kuta zilizotenganisha kila upande zilikuwa na vipimo vilivyo sawa. Kisha akapima upana wa ingilio la lango, ilikuwa dhiraa kumi na urefu wake ulikuwa dhiraa kumi na tatu. Mbele ya kila chumba cha kupumzikia kulikuwepo ukuta uliokuwa na kimo cha dhiraa moja kwenda juu, navyo hivyo vyumba vilikuwa dhiraa sita mraba. Kisha akapima njia ya lango kuanzia juu ya ukuta wa nyuma wa chumba kimoja cha kupumzikia hadi juu ya ukuta wa nyuma wa chumba upande wa pili; kukawa na nafasi ya dhiraa ishirini na tano kuanzia lango la ukuta mmoja hadi lango la ukuta uliokuwa upande mwingine. Akapima pia ukumbi, urefu wa dhiraa ishirini na lango linalofuatia hiyo nguzo kila upande wa huo ukumbi. Umbali kuanzia ingilio la njia ya lango hadi mwisho kabisa wa baraza yake ulikuwa dhiraa hamsini. Kulikuwa na vidirisha kwenye hivyo vyumba vya walinzi na nguzo za hivyo vyumba zilikuwa kwenye mzunguko wa hilo lango, vivyo hivyo kulikuwa na madirisha yaliyozunguka kuelekeana na ua na juu ya kila nguzo kulikuwa na mapambo ya miti ya mitende. Kisha akanileta katika ukumbi wa nje. Huko nikaona vyumba vingine pamoja na njia iliyokuwa imejengwa kuzunguka ukumbi wote, kulikuwa na vyumba thelathini vimepangana kando ya hiyo njia. Njia hii iliyojengwa iliambaa na lango, ikiwa na urefu sawa na lango, hii ilikuwa ni njia ya chini. Kisha akapima umbali kutoka ndani ya lango la chini mpaka nje ya ukumbi wa ndani, nao ulikuwa dhiraa mia moja upande wa mashariki na dhiraa mia moja upande wa kaskazini. Kisha akapima urefu na upana wa lango linaloelekea kaskazini, kukabili ukumbi wa nje. Vyumba vyake vilikuwa vitatu kila upande, kuta zilizogawanya vyumba na baraza ilikuwa na vipimo sawa na zile kuta za lango la kwanza. Zilikuwa na urefu wa dhiraa hamsini na upana wa dhiraa ishirini na tano. Madirisha yake, baraza yake na nakshi yake ya miti ya mitende vilikuwa na vipimo sawasawa na vile vya lango linaloelekea mashariki. Kulikuwa na ngazi saba za kupandia huko, pamoja na baraza yake mkabala nazo. Kulikuwa na lango kwenye ukumbi wa ndani lililoelekea lile lango la kaskazini, kama vile ilivyokuwa ule upande wa mashariki. Akapima kutoka lango moja hadi lile lililo mkabala nalo, lilikuwa dhiraa mia moja. Ndipo akaniongoza mpaka upande wa kusini, nami nikaona lango linaloelekea kusini. Akaipima miimo yake na baraza yake, navyo vilikuwa na vipimo sawa kama hivyo vingine. Lango na baraza yake vilikuwa na madirisha membamba pande zote, kama madirisha ya huko kwingine. Ilikuwa na urefu wa dhiraa hamsini na upana wake dhiraa ishirini na tano. Kulikuwa na ngazi saba za kupandia huko, pamoja na baraza yake mkabala nazo. Ilikuwa na nakshi za miti ya mitende kwenye kuta zilizogawanya vyumba kila upande. Ukumbi wa ndani pia ulikuwa na lango lililoelekea kusini. Naye akapima kutoka lango hili mpaka kwenye lango la nje upande wa kusini; ilikuwa dhiraa mia moja.
Ezekieli 40:1-27 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Katika mwaka wa ishirini na tano wa kuhamishwa kwetu, mwanzo wa mwaka, siku ya kumi ya mwezi, katika mwaka wa kumi na nne baada ya kupigwa mji, siku iyo hiyo, mkono wa BWANA ulikuwa juu yangu, akanileta huko. Katika maono ya Mungu alinileta mpaka nchi ya Israeli, akaniweka juu ya mlima mrefu sana, ambao juu yake palikuwapo kana kwamba ni umbo la mji upande wa kusini. Akanileta huko, na tazama, alikuwapo mtu, ambaye kuonekana kwake kulikuwa kama kuonekana kwa shaba, naye alikuwa na uzi wa kitani mkononi mwake, na mwanzi wa kupimia; akasimama karibu na lango. Mtu yule akaniambia, Mwanadamu, tazama kwa macho yako, sikia kwa masikio yako, ukaweke moyoni mwako, yote nitakayokuonyesha; maana umeletwa hapa kusudi nikuonyeshe haya; tangaza habari ya yote utakayoyaona kwa nyumba ya Israeli. Na, tazama, kulikuwa na ukuta nje ya nyumba pande zote, na katika mkono wa mtu yule mwanzi wa kupimia, urefu wake dhiraa sita, kila dhiraa, dhiraa na shubiri; basi akaupima upana wa jengo lile, mwanzi mmoja, na urefu wake, mwanzi mmoja. Kisha akaenda mpaka lango lielekealo upande wa mashariki, akapanda madaraja yake; akakipima kizingiti cha lango; upana wake mwanzi mmoja; na kizingiti cha pili, upana wake mwanzi mmoja. Na kila chumba, upana wake mwanzi mmoja, na urefu wake mwanzi mmoja; na nafasi iliyokuwa kati ya vyumba ni dhiraa tano; na kizingiti cha lango lililokuwa karibu na ukumbi wa lango lililoielekea nyumba, mwanzi mmoja. Akaupima na ukumbi wa lango lililoielekea nyumba, mwanzi mmoja. Kisha akaupima ukumbi wa lango, dhiraa nane; na miimo yake, dhiraa mbili; na ukumbi wa lango uliielekea nyumba. Na vyumba vya walinzi, vya lango upande wa mashariki, vilikuwa vitatu upande huu, na vitatu upande huu; vyote vitatu vya kipimo kimoja; nayo miimo ilikuwa na kipimo kimoja, upande huu na upande huu. Akaupima upana wa mahali pa kuliingilia lango, dhiraa kumi; na urefu wa lango, dhiraa kumi na tatu. Na mpaka, mbele ya vile vyumba, dhiraa moja upande huu, na mpaka, dhiraa moja upande huu; na vile vyumba, dhiraa sita upande huu, na dhiraa sita upande huu. Akalipima lango, toka paa la chumba kimoja hata paa la chumba cha pili, upana wa dhiraa ishirini na tano; mlango mmoja ukielekea mlango wa pili. Akafanya miimo pia, dhiraa sitini; na uwanda uliufikilia mwimo, lango lile likizungukwa pande zote. Na toka mahali palipo mbele ya lango, penye maingilio yake, hata mahali palipo mbele ya ukumbi wa ndani ya lango, dhiraa hamsini. Na kwa vile vyumba palikuwa na madirisha yaliyofungwa, na kwa miimo yake ndani ya lango pande zote, na kwa matao yake vivyo hivyo; na madirisha yalikuwako, pande zote upande wa ndani, tena palikuwa na mitende juu ya kila mwimo. Ndipo akanileta mpaka ua wa nje, na tazama, palikuwa na vyumba, na sakafu iliyofanyizwa kwa ule ua pande zote; vyumba thelathini vilikuwako juu ya sakafu ile. Na ile sakafu ilikuwa kando ya malango, urefu wake sawasawa na urefu wa malango, yaani, sakafu ya chini. Kisha akaupima upana, toka mahali palipokuwa mbele ya lango la chini hata mahali palipokuwa mbele ya ua wa ndani, nje yake, dhiraa mia upande wa mashariki, na upande wa kaskazini. Nalo lango la ua wa nje, lililoelekea kaskazini, akalipima urefu wake, na upana wake. Na vyumba vyake vya walinzi vilikuwa vitatu upande huu, na vitatu upande huu; na miimo yake, na matao yake, kipimo chake ni sawasawa na kipimo cha lango la kwanza; urefu wake dhiraa hamsini, na upana wake dhiraa ishirini na tano. Na madirisha yake, na matao yake, na mitende yake, kipimo chake ni sawasawa na kipimo cha lango lililoelekea upande wa mashariki; nao hupanda kwa madaraja saba; na matao yake yalikuwa mbele yake. Na ule ua wa ndani ulikuwa na lango lililoelekea lile lango la pili, upande wa kaskazini, na upande wa mashariki; akapima toka lango hata lango, dhiraa mia. Akanileta mpaka upande wa kusini, na tazama, lango lililoelekea kusini; akaipima miimo yake, na matao yake, sawasawa na vipimo hivyo. Tena palikuwa na madirisha ndani yake, na katika matao yake pande zote kama madirisha hayo; urefu wake dhiraa hamsini, na upana wake dhiraa ishirini na tano. Tena palikuwa na madaraja saba ya kulipandia, na matao yake yalikuwa mbele yake; nalo lilikuwa na mitende, mmoja upande huu, na mmoja upande huu, juu ya miimo yake. Tena ua wa ndani ulikuwa na lango, lililoelekea kusini; akapima toka lango hata lango, kwa kuelekea upande wa kusini, dhiraa mia.