Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Ezekieli 40:1-27

Ezekieli 40:1-27 SRUV

Katika mwaka wa ishirini na tano wa kuhamishwa kwetu, mwanzo wa mwaka, siku ya kumi ya mwezi, katika mwaka wa kumi na nne baada ya kupigwa mji, siku iyo hiyo, mkono wa BWANA ulikuwa juu yangu, akanileta huko. Katika maono ya Mungu alinileta mpaka nchi ya Israeli, akaniweka juu ya mlima mrefu sana, ambao juu yake palikuwapo kana kwamba ni umbo la mji upande wa kusini. Akanileta huko, na tazama, alikuwapo mtu, ambaye kuonekana kwake kulikuwa kama kuonekana kwa shaba, naye alikuwa na uzi wa kitani mkononi mwake, na mwanzi wa kupimia; akasimama karibu na lango. Mtu yule akaniambia, Mwanadamu, tazama kwa macho yako, sikia kwa masikio yako, ukaweke moyoni mwako, yote nitakayokuonesha; maana umeletwa hapa kusudi nikuoneshe haya; tangaza habari ya yote utakayoyaona kwa nyumba ya Israeli. Na, tazama, kulikuwa na ukuta nje ya nyumba pande zote, na katika mkono wa mtu yule mwanzi wa kupimia, urefu wake dhiraa sita, kila dhiraa, dhiraa na shubiri; basi akaupima upana wa jengo lile, mwanzi mmoja, na urefu wake, mwanzi mmoja. Kisha akaenda hadi katika lango lielekealo upande wa mashariki, akapanda madaraja yake; akakipima kizingiti cha lango; upana wake mwanzi mmoja; na kizingiti cha pili, upana wake mwanzi mmoja. Na kila chumba, upana wake mwanzi mmoja, na urefu wake mwanzi mmoja; na nafasi iliyokuwa kati ya vyumba ni dhiraa tano; na kizingiti cha lango lililokuwa karibu na ukumbi wa lango lililoielekea nyumba, mwanzi mmoja. Akaupima na ukumbi wa lango lililoielekea nyumba, mwanzi mmoja. Kisha akaupima ukumbi wa lango, dhiraa nane; na miimo yake, dhiraa mbili; na ukumbi wa lango uliielekea nyumba. Na vyumba vya walinzi, vya lango upande wa mashariki, vilikuwa vitatu upande huu, na vitatu upande huu; vyote vitatu vya kipimo kimoja; nayo miimo ilikuwa na kipimo kimoja, upande huu na upande huu. Akaupima upana wa mahali pa kuliingilia lango, dhiraa kumi; na urefu wa lango, dhiraa kumi na tatu. Na mpaka, mbele ya vile vyumba, dhiraa moja upande huu, na mpaka, dhiraa moja upande huu; na vile vyumba, dhiraa sita upande huu, na dhiraa sita upande huu. Akalipima lango, toka paa la chumba kimoja hadi paa la chumba cha pili, upana wa dhiraa ishirini na tano; mlango mmoja ukielekea mlango wa pili. Akafanya miimo pia, dhiraa sitini; na uwanda uliufikia mwimo, lango lile likizungukwa pande zote. Na toka mahali palipo mbele ya lango, penye maingilio yake, hata mahali palipo mbele ya ukumbi wa ndani ya lango, dhiraa hamsini. Na kwa vile katika vyumba palikuwa na madirisha yaliyofungwa, na kwa miimo yake ndani ya lango pande zote, na kwa matao yake vivyo hivyo; na madirisha yalikuwako, pande zote upande wa ndani, tena palikuwa na mitende juu ya kila mwimo. Ndipo akanileta mpaka katika ua wa nje, na tazama, palikuwa na vyumba, na sakafu iliyofanyizwa kwa ule ua pande zote; vyumba thelathini vilikuwako juu ya sakafu ile. Na ile sakafu ilikuwa kando ya malango, urefu wake sawasawa na urefu wa malango, yaani, sakafu ya chini. Kisha akaupima upana, toka mahali palipokuwa mbele ya lango la chini hadi mahali palipokuwa mbele ya ua wa ndani, nje yake, dhiraa mia moja upande wa mashariki, na upande wa kaskazini. Nalo lango la ua wa nje, lililoelekea kaskazini, akalipima urefu wake, na upana wake. Na vyumba vyake vya walinzi vilikuwa vitatu upande huu, na vitatu upande huu; na miimo yake, na matao yake, kipimo chake ni sawasawa na kipimo cha lango la kwanza; urefu wake dhiraa hamsini, na upana wake dhiraa ishirini na tano. Na madirisha yake, na matao yake, na mitende yake, kipimo chake ni sawasawa na kipimo cha lango lililoelekea upande wa mashariki; nao hupanda kwa madaraja saba; na matao yake yalikuwa mbele yake. Na ule ua wa ndani ulikuwa na lango lililoelekea lile lango la pili, upande wa kaskazini, na upande wa mashariki; akapima toka lango hadi lango, dhiraa mia moja. Akanileta mpaka upande wa kusini, na tazama, lango lililoelekea kusini; akaipima miimo yake, na matao yake, sawasawa na vipimo hivyo. Tena palikuwa na madirisha ndani yake, na katika matao yake pande zote kama madirisha hayo; urefu wake dhiraa hamsini, na upana wake dhiraa ishirini na tano. Tena palikuwa na madaraja saba ya kulipandia, na matao yake yalikuwa mbele yake; nalo lilikuwa na mitende, mmoja upande huu, na mmoja upande huu, juu ya miimo yake. Tena ua wa ndani ulikuwa na lango, lililoelekea kusini; akapima toka lango hadi lango, kwa kuelekea upande wa kusini, dhiraa mia moja.