Ezekieli 31:15-18
Ezekieli 31:15-18 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Bwana MUNGU asema hivi, Katika siku ile alipoteremka mpaka kuzimu niliamuru matanga, nilikifunika kilindi kwa ajili yake, nikiizuia mito yake, nayo maji makuu yalizuiwa; niliamuru Lebanoni kumwombolezea, na miti yote ya shambani ilizimia kwa ajili yake. Niliwatetemesha mataifa kwa mshindo wa kuanguka kwake, hapo nilipomtupa chini mpaka kuzimu, pamoja nao washukao shimoni; na miti yote ya Adeni, miti iliyo miteule na iliyo mizuri ya Lebanoni, yote inywayo maji, ilifarijika pande za chini za nchi. Hao nao waliteremka kuzimuni pamoja naye kwa watu waliouawa kwa upanga; naam, wale waliowasaidia, waliokaa chini ya uvuli wake kati ya mataifa. Umefanana na nani, hivi katika utukufu na ukuu, kati ya miti ya Adeni? Lakini utashushwa pamoja na miti ya Adeni, hata pande za chini za nchi; utalala kati ya hao wasiotahiriwa; pamoja na hao waliouawa kwa upanga. Huyu ndiye Farao, na jamii yote ya watu wake, asema Bwana MUNGU.
Ezekieli 31:15-18 Biblia Habari Njema (BHN)
“Kwa hiyo mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Siku ileile mwerezi ulipofika kuzimu nilitandaza giza nene juu yake nikaufunika; mito yake niliikausha na mtiririko wa maji yake mengi nikaukomesha. Nayo Lebanoni niliiweka gizani kwa ajili yake, na miti yote msituni ikazirai kwa ajili yake. Niliyafanya mataifa yatetemeke kwa sauti ya kuanguka kwake, naam, wakati nilipouangusha chini kuzimu pamoja nao washukao shimoni kwa wafu nayo miti yote ya Edeni, miti mizuri na ya pekee ya Lebanoni ambayo ilimwagiliwa maji ilifarijiwa huko chini kwa wafu. Hiyo nayo ilishuka huko kuzimu pamoja nao, ikajiunga na wale waliofungamana nao na ambao waliburudika chini ya kivuli chake. “Kwa uzuri na ukuu wa mti huo, hamna mti wowote bustanini Edeni ambao uliweza kulinganishwa nao. Sasa, mti huo ni wewe mfalme Farao. Wewe utatupwa chini kwa wafu pamoja na miti ya Edeni. Utalala karibu na wale wasiomjua Mungu na wale waliouawa kwa upanga. Hiyo itakuwa hali yako ewe Farao, wewe na watu wako. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nimesema.”
Ezekieli 31:15-18 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Bwana MUNGU asema hivi, Katika siku ile alipotelemka mpaka kuzimu naliamuru matanga, nalikifunika kilindi kwa ajili yake, nikiizuia mito yake, nayo maji makuu yalizuiwa; naliamuru Lebanoni kumwombolezea, na miti yote ya kondeni ilizimia kwa ajili yake. Niliwatetemesha mataifa kwa mshindo wa kuanguka kwake, hapo nilipomtupa chini mpaka kuzimu, pamoja nao washukao shimoni; na miti yote ya Adeni, miti iliyo miteule na iliyo mizuri ya Lebanoni, yote inywayo maji, ilifarijika pande za chini za nchi. Hao nao walitelemka kuzimuni pamoja naye kwa watu waliouawa kwa upanga; naam, wale waliokuwa mkono wake, waliokaa chini ya uvuli wake kati ya mataifa. Umefanana na nani, hivi katika utukufu na ukuu, kati ya miti ya Adeni? Lakini utashushwa pamoja na miti ya Adeni, hata pande za chini za nchi; utalala kati ya hao wasiotahiriwa; pamoja na hao waliouawa kwa upanga. Huyu ndiye Farao, na jamii yote ya watu wake, asema Bwana MUNGU.
Ezekieli 31:15-18 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
“ ‘Hili ndilo BWANA Mwenyezi asemalo: Katika siku ile mwerezi uliposhushwa chini kaburini nilizifunika chemchemi zenye maji mengi kwa maombolezo: Nilivizuia vijito vyake na wingi wa maji yake nikauzuia. Kwa sababu yake niliivika Lebanoni huzuni, nayo miti yote ya shambani ikanyauka. Niliyafanya mataifa yatetemeke kwa kishindo cha kuanguka kwake wakati nilipoushusha chini kaburini pamoja na wale washukao shimoni. Ndipo miti yote ya Edeni, miti iliyo bora kuliko yote na iliyo mizuri sana ya Lebanoni, miti yote ile iliyokunywa maji vizuri, ilifarijika hapa duniani. Wale walioishi katika kivuli chake, wale walioungana naye miongoni mwa mataifa, nao pia walikuwa wamezikwa pamoja naye, wakiungana na wale waliouawa kwa upanga. “ ‘Ni miti ipi ya Edeni inayoweza kulinganishwa nawe kwa fahari na utukufu? Hata hivyo, wewe pia, utashushwa chini pamoja na miti ya Edeni mpaka kuzimu, utalala miongoni mwa wasiotahiriwa, pamoja na wale waliouawa kwa upanga. “ ‘Huyu ni Farao pamoja na makundi yake yote ya wajeuri, asema BWANA Mwenyezi.’ ”