Kutoka 5:1-23
Kutoka 5:1-23 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Hata baadaye, Musa na Haruni wakaenda wakamwambia Farao, wakasema, BWANA, Mungu wa Israeli, asema hivi, Wape watu wangu ruhusa waende, ili kunifanyia sikukuu jangwani. Farao akasema, BWANA ni nani, hata niisikilize sauti yake, na kuwapa Israeli ruhusa waende zao? Mimi simjui BWANA, wala sitawapa Israeli ruhusa waende zao. Wakasema, Mungu wa Waebrania amekutana nasi; twakuomba, tupe ruhusa twende safari ya siku tatu jangwani, tumtolee dhabihu BWANA, Mungu wetu; asije akatupiga kwa tauni, au kwa upanga. Mfalme wa Misri akawaambia Enyi Musa na Haruni, mbona mnawaachisha watu kazi zao? Enendeni zenu kwa mizigo yenu. Kisha Farao akasema, Tazameni, watu wa nchi sasa ni wengi, nanyi mnawapumzisha, wasichukue mizigo yao. Na siku ile ile Farao akawaamuru wasimamizi wa watu, na wanyapara wao, akisema, Msiwape watu tena majani ya kufanyia matofali, kama mlivyofanya tangu hapo; na waende wakatafute majani wenyewe. Lakini hesabu ya matofali waliyokuwa wakifanya tokea hapo, wawekeeni iyo hiyo, msiipunguze hata kidogo, kwa maana ni wavivu hao; kwa hiyo wanapiga kelele, wakisema, Tupe ruhusa twende kumtolea Mungu wetu dhabihu. Wapeni watu hao kazi nzito zaidi, waitaabikie; wala wasiangalie maneno ya uongo. Hao wasimamizi wa watu na wanyapara wao wakatoka, wakasema na watu, wakanena, Farao asema hivi, Mimi siwapi majani. Enendeni wenyewe, jipatieni majani hapo mtakapoyaona; kwa maana kazi yenu haitapunguzwa hata kidogo. Basi hao watu wakatawanyika katika nchi yote ya Misri ili wapate kukusanya matakataka ya mashamba badala ya majani. Wasimamizi wao wakawahimiza, wakisema, Timizeni kazi zenu, shughuli zenu za kila siku, kama wakati ule majani yalipokuwapo. Na wanyapara wa wana wa Israeli, ambao wasimamizi wa Farao wamewaweka juu yao, wakapigwa, wakiambiwa, Kwa nini hamkutimiza kazi yenu jana na leo; kwa kufanya matofali kama hapo kwanza? Basi wanyapara wa wana wa Israeli wakaenda, wakamlilia Farao, wakisema, Mbona umetutendea hivi, sisi watumwa wako? Watumwa wako hawapewi majani, nao wanatuambia, Fanyeni matofali; na tazama, watumwa wako wapigwa; lakini kosa hilo ni la watu wako mwenyewe. Akasema, Wavivu ninyi; wavivu; kwa ajili hii mwasema, Tupe ruhusa twende kumtolea BWANA dhabihu. Basi, enendeni sasa, mkafanye kazi; kwa maana hamtapewa majani, na pamoja na hayo mtaleta hesabu ile ile ya matofali. Basi wanyapara wa wana wa Israeli wakaona ya kwamba wa katika hali mbaya, walipoambiwa, Hamtapunguza hesabu ya matofali yenu hata kidogo; ndizo shughuli zenu za kila siku. Wakakutana na Musa na Haruni, waliokuwa wanasimama njiani, hapo walipotoka kwa Farao; wakawaambia, BWANA awaangalie na kuamua; kwa kuwa mmefanya harufu yetu kuwa chukizo mbele ya Farao, na mbele ya watumishi wake, mkatia upanga mikononi mwao, watuue. Musa akarudi kwa BWANA, akasema, BWANA, mbona umewatenda mabaya watu hawa? Kwani kunituma mimi? Kwa maana tangu nilipokwenda kwa Farao, kusema naye kwa jina lako, amewatenda mabaya watu hawa; wala hukuwaokoa watu wako hata kidogo.
Kutoka 5:1-23 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Baadaye Mose na Aroni wakaenda kwa Farao, wakamwambia, “Hili ndilo asemalo BWANA, Mungu wa Israeli: ‘Waruhusu watu wangu waende, ili waweze kunifanyia sikukuu huko jangwani.’ ” Farao akasema, “Huyo BWANA ni nani, hata nimtii na kuruhusu Israeli uende? Simjui huyo BWANA wala sitawaruhusu Israeli waende.” Ndipo Mose na Aroni wakasema, “Mungu wa Waebrania amekutana nasi. Sasa turuhusu tuwe na safari ya siku tatu ya jangwani ili tukamtolee BWANA Mungu wetu dhabihu, la sivyo aweza kutupiga sisi kwa tauni au kwa upanga.” Lakini mfalme wa Misri akasema, “Mbona ninyi Mose na Aroni mnawachukua watu waache kazi zao? Rudini kwenye kazi zenu!” Kisha Farao akasema, “Tazama, sasa watu hawa ni wengi, nanyi mnawazuia kufanya kazi.” Siku iyo hiyo Farao akatoa amri hii kwa viongozi wa watumwa na wasimamizi wa watu akawaambia: “Tangu sasa msiwape hawa watu nyasi za kutengenezea matofali. Wao wakusanye nyasi zao wenyewe. Lakini watakeni kutengeneza matofali kiasi kile kile cha mwanzo, kiwango kisipunguzwe. Wao ni wavivu, ndiyo sababu wanalia, wakisema, ‘Turuhusiwe twende kumtolea Mungu wetu dhabihu.’ Fanyeni kazi kuwa ngumu zaidi kwa watu hao ili kwamba wakazane na kazi na kuacha kusikiliza uongo.” Basi viongozi wa watumwa na wasimamizi wakaenda kuwaambia watu, “Hivi ndivyo Farao asemavyo: ‘Sitawapa tena nyasi. Nendeni mkatafute nyasi wenyewe popote mnapoweza kuzipata, lakini kazi yenu haitapunguzwa hata kidogo.’ ” Basi watu wakatawanyika kote nchini Misri kukusanya mabua ya kutumia badala ya nyasi. Viongozi wa watumwa wakasisitiza, wakisema, “Timizeni kazi mnayotakiwa kwa kila siku, kama wakati ule mlipokuwa mkipewa nyasi.” Wasimamizi wa Kiisraeli waliochaguliwa na viongozi wa watumwa wa Farao walipigwa na kuulizwa, “Kwa nini hamkutimiza kiwango chenu cha kutengeneza matofali jana na leo, kama mwanzoni?” Ndipo wasimamizi wa Kiisraeli wakaenda kumlilia Farao, wakisema: “Mbona umewatendea watumishi wako hivi? Watumishi wako hawapewi nyasi, hata hivyo tumeambiwa, ‘Tengenezeni matofali!’ Watumishi wako wanapigwa, lakini kosa ni la watu wako wenyewe.” Farao akasema, “Ninyi ni wavivu ndiyo sababu mnasema, ‘Turuhusu twende tukamtolee BWANA dhabihu.’ Sasa nendeni kazini. Hamtapewa nyasi zozote, nanyi ni lazima mtengeneze matofali.” Wasimamizi wa Kiisraeli walitambua kuwa wako taabani walipoambiwa, “Hamtakiwi kupunguza idadi ya matofali mliotakiwa kutengeneza kila siku.” Walipoondoka kwa Farao, wakawakuta Mose na Aroni wakingojea kukutana nao, wakawaambia Mose na Aroni, “BWANA na awaangalie awahukumu ninyi! Mmetufanya tunuke kwa Farao na maafisa wake, nanyi mmeweka upanga mikononi mwao ili kutuua sisi.” Mose akarudi kwa BWANA na kumwambia, “Ee Bwana, mbona umewaletea watu hawa taabu? Kwa nini basi ukanituma mimi? Tangu nilipomwendea Farao kuzungumza naye kwa jina lako, amewaletea taabu watu hawa, nawe kamwe hujawakomboa watu wako.”
Kutoka 5:1-23 Biblia Habari Njema (BHN)
Baadaye, Mose na Aroni walimwendea Farao, wakamwambia, “Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli anasema hivi, ‘Waache watu wangu waondoke, wakanifanyie sikukuu jangwani.’” Lakini Farao akawauliza, “Ni nani huyo Mwenyezi-Mungu, hata nimsikilize na kuwaacha Waisraeli waondoke? Mimi simtambui huyo Mwenyezi-Mungu, wala sitawaruhusu Waisraeli waondoke.” Mose na Aroni wakamwambia, “Mungu wa Waebrania amekutana nasi. Tunakusihi utuache twende zetu jangwani mwendo wa siku tatu tukamtambikie Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu. La sivyo, yeye atatuua kwa maradhi mabaya au vita.” Lakini mfalme wa Misri akawajibu, “Enyi Mose na Aroni, kwa nini mnajaribu kuwatoa watu kazini mwao? Rudini kazini mwenu.” Tena Farao akasema, “Hawa watu wenu ni wengi kuliko wananchi; mnataka waache kufanya kazi!” Siku hiyohiyo Farao aliwaamuru wanyapara pamoja na wasimamizi, akasema, “Tangu leo msiwape watu hawa nyasi za kutengenezea matofali kama ilivyo kawaida. Wao wenyewe watakwenda kujitafutia. Lakini idadi ya matofali yanayotengenezwa kila siku iwe ileile, wala lisipungue hata tofali moja, kwa kuwa watu hawa ni wavivu ndio maana wanapiga kelele: ‘Tuache twende tukamtambikie Mungu wetu.’ Wazidishieni watu hawa kazi ngumu ili waitolee jasho na kuacha kusema maneno ya uongo.” Basi, wanyapara na wasimamizi wa watu wakatoka na kuwaambia watu, “Farao anasema hivi, ‘Sitawapeni nyasi. Nendeni nyinyi wenyewe mkatafute popote mtakapoweza kuzipata, na wala kazi yenu haitapunguzwa hata kidogo.’” Basi, watu wote wakatawanyika kila mahali nchini Misri wakitafuta nyasi za kutengenezea matofali. Nao Wanyapara wakakazana wakisema, “Timizeni kazi yenu ya kila siku kama hapo awali mlipoletewa nyasi.” Wanyapara Wamisri wakawapiga wasimamizi wa Waisraeli waliochaguliwa kusimamia kazi wakisema, “Kwa nini hamtimizi kazi yenu na kufikisha idadi ileile ya matofali kama awali?” Ndipo wasimamizi wa Waisraeli walipomwendea Farao, wakamlilia wakisema, “Kwa nini unatutenda hivi sisi watumishi wako? Hatupewi tena nyasi zozote na huku tunalazimishwa kufyatua matofali. Tena sisi watumishi wako tunapigwa, hali kosa ni la watu wako.” Lakini Farao akasema, “Wavivu nyinyi; nyinyi ni wavivu, ndio maana mnasema, ‘Tuache twende tukamtambikie Mwenyezi-Mungu’. Nendeni sasa mkafanye kazi; maana hamtapewa nyasi zozote na mtafyatua idadi ileile ya matofali.” Basi, hao wasimamizi wa Waisraeli sasa walijiona kuwa wako taabuni, kwani waliambiwa, “Hamtaipunguza kamwe idadi ya matofali ya kila siku.” Walipoondoka kwa Farao, walikutana na Mose na Aroni ambao walikuwa wanawangojea. Basi, wakawaambia Mose na Aroni, “Mwenyezi-Mungu na aone jambo hili na kuwahukumu nyinyi kwa sababu mmetufanya sisi kuwa chukizo kwa Farao na maofisa wake; nyinyi mmewapa sababu ya kutuua.” Kisha Mose akamgeukia tena Mwenyezi-Mungu, akasema, “Ee Mwenyezi-Mungu, kwa nini unawatendea watu hawa uovu? Kwa nini hata ulinituma? Tangu nilipokwenda na kuongea na Farao kwa jina lako, yeye amewatendea uovu watu hawa. Wewe hujafanya lolote kuwakomboa watu wako.”
Kutoka 5:1-23 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Hata baadaye, Musa na Haruni wakaenda wakamwambia Farao, wakasema, BWANA, Mungu wa Israeli, asema hivi, Wape watu wangu ruhusa waende, ili kunifanyia sikukuu jangwani. Farao akasema, BWANA ni nani, hata niisikilize sauti yake, na kuwapa Israeli ruhusa waende zao? Mimi simjui BWANA, wala sitawapa Israeli ruhusa waende zao. Wakasema, Mungu wa Waebrania amekutana nasi; twakuomba, tupe ruhusa twende safari ya siku tatu jangwani, tumtolee dhabihu BWANA, Mungu wetu; asije akatupiga kwa tauni, au kwa upanga. Mfalme wa Misri akawaambia Enyi Musa na Haruni, mbona mnawaachisha watu kazi zao? Nendeni zenu kwa mizigo yenu. Kisha Farao akasema, Tazameni, watu wa nchi sasa ni wengi, nanyi mnawapumzisha, wasichukue mizigo yao. Na siku ile ile Farao akawaamuru wasimamizi wa watu, na wanyapara wao, akisema, Msiwape watu tena majani ya kufanyia matofali, kama mlivyofanya tangu hapo; na waende wakatafute majani wenyewe. Lakini hesabu ya matofali waliyokuwa wakifanya tokea hapo, wawekeeni iyo hiyo, msiipunguze hata kidogo, kwa maana ni wavivu hao; kwa hiyo wanapiga kelele, wakisema, Tupe ruhusa twende kumtolea Mungu wetu dhabihu. Wapeni watu hao kazi nzito zaidi, waitaabikie; wala wasiangalie maneno ya uongo. Hao wasimamizi wa watu na wanyapara wao wakatoka, wakasema na watu, wakanena, Farao asema hivi, Mimi siwapi majani. Nendeni wenyewe, jipatieni majani hapo mtakapoyaona; kwa maana kazi yenu haitapunguzwa hata kidogo. Basi hao watu wakatawanyika katika nchi yote ya Misri ili wapate kukusanya takataka ya mashamba badala ya majani. Wasimamizi wao wakawahimiza, wakisema, Timizeni kazi zenu, shughuli zenu za kila siku, kama wakati ule majani yalipokuwapo. Na wanyapara wa wana wa Israeli, ambao wasimamizi wa Farao wamewaweka juu yao, wakapigwa, wakiambiwa, Kwa nini hamkutimiza kazi yenu jana na leo; kwa kufanya matofali kama hapo kwanza? Basi wanyapara wa wana wa Israeli wakaenda, wakamlilia Farao, wakisema, Mbona umetutenda hivi, sisi watumwa wako? Watumwa wako hawapewi majani, nao wanatuambia, Fanyeni matofali; na tazama, watumwa wako wapigwa; lakini kosa hilo ni la watu wako mwenyewe. Akasema, Wavivu ninyi; wavivu; kwa ajili hii mwasema, Tupe ruhusa twende kumtolea BWANA dhabihu. Basi, nendeni sasa, mkafanye kazi; kwa maana hamtapewa majani, na pamoja na hayo mtaleta hesabu ile ile ya matofali. Basi wanyapara wa wana wa Israeli wakaona ya kwamba wako katika hali mbaya, walipoambiwa, Hamtapunguza idadi ya matofali yenu hata kidogo; ndizo shughuli zenu za kila siku. Wakakutana na Musa na Haruni, waliokuwa wanasimama njiani, hapo walipotoka kwa Farao; wakawaambia, BWANA awaangalie na kuamua; kwa kuwa mmefanya harufu yetu kuwa chukizo mbele ya Farao, na mbele ya watumishi wake, mkatia upanga mikononi mwao, watuue. Musa akarudi kwa BWANA, akasema, BWANA, mbona umewatenda mabaya watu hawa? Kwani kunituma mimi? Kwa maana tangu nilipokwenda kwa Farao, kusema naye kwa jina lako, amewatenda mabaya watu hawa; wala hukuwaokoa watu wako hata kidogo.