Kutoka 5:1-23
Kutoka 5:1-23 SRUV
Hata baadaye, Musa na Haruni wakaenda wakamwambia Farao, wakasema, BWANA, Mungu wa Israeli, asema hivi, Wape watu wangu ruhusa waende, ili kunifanyia sikukuu jangwani. Farao akasema, BWANA ni nani, hata niisikilize sauti yake, na kuwapa Israeli ruhusa waende zao? Mimi simjui BWANA, wala sitawapa Israeli ruhusa waende zao. Wakasema, Mungu wa Waebrania amekutana nasi; twakuomba, tupe ruhusa twende safari ya siku tatu jangwani, tumtolee dhabihu BWANA, Mungu wetu; asije akatupiga kwa tauni, au kwa upanga. Mfalme wa Misri akawaambia Enyi Musa na Haruni, mbona mnawaachisha watu kazi zao? Nendeni zenu kwa mizigo yenu. Kisha Farao akasema, Tazameni, watu wa nchi sasa ni wengi, nanyi mnawapumzisha, wasichukue mizigo yao. Na siku ile ile Farao akawaamuru wasimamizi wa watu, na wanyapara wao, akisema, Msiwape watu tena majani ya kufanyia matofali, kama mlivyofanya tangu hapo; na waende wakatafute majani wenyewe. Lakini hesabu ya matofali waliyokuwa wakifanya tokea hapo, wawekeeni iyo hiyo, msiipunguze hata kidogo, kwa maana ni wavivu hao; kwa hiyo wanapiga kelele, wakisema, Tupe ruhusa twende kumtolea Mungu wetu dhabihu. Wapeni watu hao kazi nzito zaidi, waitaabikie; wala wasiangalie maneno ya uongo. Hao wasimamizi wa watu na wanyapara wao wakatoka, wakasema na watu, wakanena, Farao asema hivi, Mimi siwapi majani. Nendeni wenyewe, jipatieni majani hapo mtakapoyaona; kwa maana kazi yenu haitapunguzwa hata kidogo. Basi hao watu wakatawanyika katika nchi yote ya Misri ili wapate kukusanya takataka ya mashamba badala ya majani. Wasimamizi wao wakawahimiza, wakisema, Timizeni kazi zenu, shughuli zenu za kila siku, kama wakati ule majani yalipokuwapo. Na wanyapara wa wana wa Israeli, ambao wasimamizi wa Farao wamewaweka juu yao, wakapigwa, wakiambiwa, Kwa nini hamkutimiza kazi yenu jana na leo; kwa kufanya matofali kama hapo kwanza? Basi wanyapara wa wana wa Israeli wakaenda, wakamlilia Farao, wakisema, Mbona umetutenda hivi, sisi watumwa wako? Watumwa wako hawapewi majani, nao wanatuambia, Fanyeni matofali; na tazama, watumwa wako wapigwa; lakini kosa hilo ni la watu wako mwenyewe. Akasema, Wavivu ninyi; wavivu; kwa ajili hii mwasema, Tupe ruhusa twende kumtolea BWANA dhabihu. Basi, nendeni sasa, mkafanye kazi; kwa maana hamtapewa majani, na pamoja na hayo mtaleta hesabu ile ile ya matofali. Basi wanyapara wa wana wa Israeli wakaona ya kwamba wako katika hali mbaya, walipoambiwa, Hamtapunguza idadi ya matofali yenu hata kidogo; ndizo shughuli zenu za kila siku. Wakakutana na Musa na Haruni, waliokuwa wanasimama njiani, hapo walipotoka kwa Farao; wakawaambia, BWANA awaangalie na kuamua; kwa kuwa mmefanya harufu yetu kuwa chukizo mbele ya Farao, na mbele ya watumishi wake, mkatia upanga mikononi mwao, watuue. Musa akarudi kwa BWANA, akasema, BWANA, mbona umewatenda mabaya watu hawa? Kwani kunituma mimi? Kwa maana tangu nilipokwenda kwa Farao, kusema naye kwa jina lako, amewatenda mabaya watu hawa; wala hukuwaokoa watu wako hata kidogo.