Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Kutoka 28:1-14

Kutoka 28:1-14 Biblia Habari Njema (BHN)

“Nawe Mose umlete kwangu Aroni ndugu yako, pamoja na wanawe: Nadabu, Abihu, Eleazari na Ithamari utawateua miongoni mwa Waisraeli, ili wanitumikie kama makuhani. Utamshonea ndugu yako Aroni mavazi matakatifu ili apate kuonekana mwenye utukufu na mzuri. Waagize mafundi wote ambao nimewapa maarifa wamtengenezee Aroni mavazi ili awekwe wakfu kwa ajili ya kazi ya ukuhani. Waambie wamtengenezee vitu vifuatavyo: Kifuko cha kifuani, kizibao, kanzu, joho iliyonakshiwa, kilemba na mshipi. Aroni nduguyo na wanawe watayavaa ili wanitumikie kama makuhani. Hao mafundi watatumia sufu ya rangi ya buluu, zambarau na nyekundu, na nyuzi za dhahabu na kitani safi iliyosokotwa. “Watakitengeneza kizibao cha kuhani kwa nyuzi za dhahabu na sufu ya rangi ya buluu, zambarau na nyekundu, na kitani safi iliyosokotwa, na kukitarizi vizuri. Kitakuwa na kamba mbili za kukifungia mabegani zilizoshonewa kwenye ncha zake mbili. Mkanda wa kukishikia utatengenezwa kwa vifaa hivyohivyo: Kwa nyuzi za dhahabu, sufu ya buluu, zambarau na nyekundu, na kitani safi iliyosokotwa na kuwa kitu kimoja na kizibao hicho. “Kisha utachukua mawe mawili ya sardoniki ambayo utachora juu yake majina ya wana wa Israeli. Majina sita katika jiwe la kwanza, na majina sita yaliyobakia katika jiwe la pili; majina yafuatane kadiri ya kuzaliwa kwao. Utayachora majina hayo juu ya hayo mawe kama vile sonara achoravyo mhuri, kisha uyatie nakshi na kuyaingiza katika vijalizo vya dhahabu. Mawe hayo mawili yatawekwa juu ya kanda za kizibao kama kumbukumbu ya makabila kumi na mawili ya Israeli. Hivyo Aroni atavaa majina hayo mabegani mwake mbele yangu mimi Mwenyezi-Mungu kama ukumbusho. Utayatengenezea vijalizo viwili vya dhahabu, na mikufu miwili ya dhahabu safi iliyosokotwa kama kamba. Utaifunga mikufu hiyo kwenye hivyo vijalizo.

Shirikisha
Soma Kutoka 28

Kutoka 28:1-14 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Nawe umlete Haruni ndugu yako karibu nami, na wanawe pamoja naye, miongoni mwa wana wa Israeli, ili anitumikie katika kazi ya ukuhani. Haruni, na Nadabu, na Abihu, na Eleazari, na Ithamari, wana wa Haruni. Nawe utamfanyia Haruni ndugu yako mavazi matakatifu, kwa utukufu na kwa uzuri. Nawe utawaambia watu wote wenye uwezo wa hali ya juu, niliowapa ubingwa wamfanyie Haruni mavazi ili awekwe wakfu anitumikie katika kazi ya ukuhani. Na mavazi watakayoyafanya ni haya; kifuko cha kifuani, na naivera, na joho, na kanzu ya kazi ya urembo; na kilemba, na mshipi; nao watawafanyia Haruni nduguyo, na wanawe, mavazi matakatifu ili anitumikie katika kazi ya ukuhani. Nao wataitwaa dhahabu, na nguo ya rangi ya buluu, zambarau, na nyekundu na nguo ya kitani nzuri. Nao waifanye naivera kwa nyuzi za dhahabu, buluu, zambarau na nyekundu, na kitani nzuri yenye kusokotwa kwa ustadi. Itakuwa na vipande viwili vya mabegani, vilivyoungana kwenye ncha zake mbili; ili ipate kuunganishwa. Na mshipi stadi ulio juu yake, ili kuifunga mahali pake; utakuwa wa kazi kama ile ya naivera, ya vitu vile vile ya nyuzi za dhahabu, za buluu, zambarau na nyekundu, na kitani nzuri yenye kusokotwa. Nawe utatwaa vito viwili vya shohamu rangi ya chanikiwiti, nawe utachora juu yake majina ya wana wa Israeli; majina yao sita katika kito kimoja, na majina sita yaliyosalia katika kile kito cha pili, kwa utaratibu wa kuzaliwa kwao. Kwa kazi mtu mwenye kuchora mawe kama vile mihuri ichorwavyo, utavichora hivi vito viwili, sawasawa na majina ya wana wa Israeli, nawe utavitia katika vijalizo vya dhahabu. Nawe utavitia vile vito viwili juu ya vipande vya mabegani vya hiyo naivera, viwe vito vya ukumbusho kwa ajili ya wana wa Israeli; naye Haruni atayachukua majina yao mbele za BWANA juu ya mabega yake mawili ili kuwa ukumbusho. Nawe fanya vijalizo viwili vya dhahabu; na mikufu miwili ya dhahabu safi; utaifanya iwe mfano wa kamba, ya kazi ya kusokotwa; nawe uitie ile mikufu ya kazi ya kusokotwa katika vile vijalizo.

Shirikisha
Soma Kutoka 28

Kutoka 28:1-14 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Nawe umlete Haruni ndugu yako karibu nami, na wanawe pamoja naye, miongoni mwa wana wa Israeli, ili anitumikie katika kazi ya ukuhani. Haruni, na Nadabu, na Abihu, na Eleazari, na Ithamari, wana wa Haruni. Nawe utamfanyia Haruni ndugu yako mavazi matakatifu, kwa utukufu na kwa uzuri. Nawe utawaambia watu wote wenye moyo wa hekima, niliowajaza na roho ya hekima wamfanyie Haruni mavazi ili kumtakasa anitumikie katika kazi ya ukuhani. Na mavazi watakayoyafanya ni haya; kifuko cha kifuani, na naivera, na joho, na kanzu ya kazi ya urembo; na kilemba, na mshipi; nao watawafanyia Haruni nduguyo, na wanawe, mavazi matakatifu ili anitumikie katika kazi ya ukuhani. Nao wataitwaa dhahabu, na nguo ya rangi ya samawi, na ya rangi ya zambarau, na ya rangi nyekundu, na nguo ya kitani nzuri. Nao waifanye naivera kwa nyuzi za dhahabu, na za samawi, na za zambarau, na nyekundu, na kitani nzuri yenye kusokotwa kwa kazi ya mstadi. Itakuwa na vipande viwili vya mabegani, vilivyoungana kwenye ncha zake mbili; ili ipate kuunganywa. Na mshipi wa kazi ya ustadi ulio juu yake, ili kuifunga mahali pake; utakuwa wa kazi kama ile ya naivera, ya vitu vile vile ya nyuzi za dhahabu, na za rangi ya samawi, na ya zambarau, na nyekundu, na kitani nzuri yenye kusokotwa. Nawe utatwaa vito viwili vya shohamu, ya rangi ya chani-kiwiti, nawe utachora juu yake majina ya wana wa Israeli; majina yao sita katika kito kimoja, na majina sita yaliyosalia katika kile kito cha pili, kwa utaratibu wa kuzaliwa kwao. Kwa kazi mtu mwenye kuchora mawe kama vile muhuri ichorwavyo, utavichora hivi vito viwili, sawasawa na majina ya wana wa Israeli, nawe utavitia katika vijalizo vya dhahabu. Nawe utavitia vile vito viwili juu ya vipande vya mabegani vya hiyo naivera, viwe vito vya ukumbusho kwa ajili ya wana wa Israeli; naye Haruni atayachukua majina yao mbele za BWANA juu ya mabega yake mawili ili kuwa ukumbusho. Nawe fanya vijalizo viwili vya dhahabu; na mikufu miwili ya dhahabu safi; utaifanya iwe mfano wa kamba, ya kazi ya kusokotwa; nawe uitie ile mikufu ya kazi ya kusokotwa katika vile vijalizo.

Shirikisha
Soma Kutoka 28

Kutoka 28:1-14 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)

“Mtwae Haruni ndugu yako aliyeletwa kwako kutoka miongoni mwa Waisraeli, pamoja na wanawe Nadabu, Abihu, Eleazari na Ithamari, ili wanitumikie katika kazi ya ukuhani. Mshonee Haruni ndugu yako mavazi matakatifu ili yampe ukuu na heshima. Waambie mafundi stadi wote niliowapa hekima katika shughuli hiyo wamtengenezee Haruni mavazi hayo, ili awekwe wakfu, anitumikie katika kazi ya ukuhani. Haya ndio mavazi watakayoshona: kifuko cha kifuani, kizibau, kanzu, joho lililofumwa, kilemba na mshipi. Mavazi haya yatashonwa kwa ajili ya ndugu yako Haruni na wanawe ili wanitumikie katika kazi ya ukuhani. Waambie watumie dhahabu na nyuzi za rangi ya buluu, za zambarau, na za rangi nyekundu pamoja na kitani safi. “Tengeneza kizibau cha dhahabu, na nyuzi za rangi ya buluu, za zambarau, za rangi nyekundu na kitani safi iliyosokotwa, kazi ya fundi stadi. Kitakuwa na vipande viwili vya mabegani vilivyoshikizwa kwenye pembe zake mbili ili kufungia kizibau. Mshipi wa kiunoni uliofumwa kwa ustadi utafanana nacho: utakuwa kitu kimoja na hicho kizibau, nao utengenezwe kwa dhahabu na nyuzi za rangi ya buluu, za zambarau, na nyekundu na kwa kitani iliyosokotwa vizuri. “Chukua vito viwili vya shohamu, na uchore juu yake majina ya wana wa Israeli kufuatana na walivyozaliwa: majina sita katika kito kimoja, na mengine sita katika kito kingine. Yachore majina ya wana wa Israeli juu ya vito hivyo viwili kama vile sonara anavyochonga muhuri. Kisha uvitie vito hivyo katika vijalizo vya dhahabu, na uvifungie juu ya vipande vya mabega ya kizibau yawe kama vito vya ukumbusho kwa wana wa Israeli. Haruni atavaa majina hayo mabegani mwake kama kumbukumbu mbele za Mwenyezi Mungu. Tengeneza vijalizo vya dhahabu na mikufu miwili ya dhahabu safi iliyosokotwa kama kamba, na uifunge mikufu hiyo kwenye vijalizo.

Shirikisha
Soma Kutoka 28