Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Kutoka 28:1-14

Kutoka 28:1-14 SRUV

Nawe umlete Haruni ndugu yako karibu nami, na wanawe pamoja naye, miongoni mwa wana wa Israeli, ili anitumikie katika kazi ya ukuhani. Haruni, na Nadabu, na Abihu, na Eleazari, na Ithamari, wana wa Haruni. Nawe utamfanyia Haruni ndugu yako mavazi matakatifu, kwa utukufu na kwa uzuri. Nawe utawaambia watu wote wenye uwezo wa hali ya juu, niliowapa ubingwa wamfanyie Haruni mavazi ili awekwe wakfu anitumikie katika kazi ya ukuhani. Na mavazi watakayoyafanya ni haya; kifuko cha kifuani, na naivera, na joho, na kanzu ya kazi ya urembo; na kilemba, na mshipi; nao watawafanyia Haruni nduguyo, na wanawe, mavazi matakatifu ili anitumikie katika kazi ya ukuhani. Nao wataitwaa dhahabu, na nguo ya rangi ya buluu, zambarau, na nyekundu na nguo ya kitani nzuri. Nao waifanye naivera kwa nyuzi za dhahabu, buluu, zambarau na nyekundu, na kitani nzuri yenye kusokotwa kwa ustadi. Itakuwa na vipande viwili vya mabegani, vilivyoungana kwenye ncha zake mbili; ili ipate kuunganishwa. Na mshipi stadi ulio juu yake, ili kuifunga mahali pake; utakuwa wa kazi kama ile ya naivera, ya vitu vile vile ya nyuzi za dhahabu, za buluu, zambarau na nyekundu, na kitani nzuri yenye kusokotwa. Nawe utatwaa vito viwili vya shohamu rangi ya chanikiwiti, nawe utachora juu yake majina ya wana wa Israeli; majina yao sita katika kito kimoja, na majina sita yaliyosalia katika kile kito cha pili, kwa utaratibu wa kuzaliwa kwao. Kwa kazi mtu mwenye kuchora mawe kama vile mihuri ichorwavyo, utavichora hivi vito viwili, sawasawa na majina ya wana wa Israeli, nawe utavitia katika vijalizo vya dhahabu. Nawe utavitia vile vito viwili juu ya vipande vya mabegani vya hiyo naivera, viwe vito vya ukumbusho kwa ajili ya wana wa Israeli; naye Haruni atayachukua majina yao mbele za BWANA juu ya mabega yake mawili ili kuwa ukumbusho. Nawe fanya vijalizo viwili vya dhahabu; na mikufu miwili ya dhahabu safi; utaifanya iwe mfano wa kamba, ya kazi ya kusokotwa; nawe uitie ile mikufu ya kazi ya kusokotwa katika vile vijalizo.

Soma Kutoka 28