Kutoka 24:3-11
Kutoka 24:3-11 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Musa akaenda akawaambia watu maneno yote ya BWANA, na hukumu zake zote; watu wote wakajibu kwa sauti moja, wakasema, Maneno yote aliyoyanena BWANA tutayatenda. Basi Musa akayaandika maneno yote ya BWANA, akaondoka asubuhi na mapema, akajenga madhabahu chini ya mlima, na nguzo kumi na mbili, kwa hesabu ya kabila kumi na mbili za Israeli, akapeleka vijana wa wana wa Israeli, waliotoa sadaka za kuteketezwa, wakamchinjia BWANA sadaka za amani za ng’ombe. Musa akatwaa nusu ya ile damu, akaitia katika mabakuli; na nusu ya ile damu akainyunyiza juu ya madhabahu. Kisha akakitwaa kitabu cha agano akakisoma masikioni mwa watu; wakasema, Hayo yote aliyoyanena BWANA tutayatenda, nasi tutatii. Musa akaitwaa ile damu, akawanyunyizia watu, akasema, Hii ndiyo damu ya agano alilolifanya BWANA pamoja nanyi katika maneno haya yote. Ndipo akakwea juu, Musa, na haruni, na Nadabu, na Abihu, na watu sabini miongoni mwa wazee wa Israeli; wakamwona Mungu wa Israeli; chini ya miguu yake palikuwa na kama sakafu iliyofanyizwa kwa yakuti samawi, kama zile mbingu zenyewe kwa usafi wake. Naye hakuweka mkono wake juu ya hao wakuu wa wana wa Israeli; nao wakamwona Mungu, wakala na kunywa.
Kutoka 24:3-11 Biblia Habari Njema (BHN)
Basi, Mose akaenda na kuwaambia watu wote maneno na maagizo yote Mwenyezi-Mungu aliyomwambia. Watu wote wakajibu kwa sauti moja, “Mambo yote aliyoyasema Mwenyezi-Mungu, tutayafanya.” Mose akayaandika maagizo yote ambayo Mwenyezi-Mungu alimpa. Kisha akaamka asubuhi na mapema, akajenga madhabahu chini ya mlima na kusimamisha nguzo kumi na mbili kulingana na idadi ya makabila kumi na mbili ya Israeli. Kisha akawatuma vijana wa Waisraeli wamtolee Mwenyezi-Mungu sadaka za kuteketezwa na kumchinjia sadaka za amani za ng'ombe. Mose akachota nusu ya damu ya wanyama hao na kuiweka katika mabirika, na nusu nyingine akairashia ile madhabahu. Kisha akachukua kitabu cha agano la Mwenyezi-Mungu, akakisoma mbele ya watu, nao wakasema, “Hayo yote aliyoyasema Mwenyezi-Mungu, tutayafanya, nasi tutakuwa watiifu.” Mose akaichukua ile damu na kuwanyunyizia watu, akisema, “Hii ndiyo damu ya agano ambalo Mwenyezi-Mungu amelifanya nanyi kufuatana na maneno haya yote.” Kisha Mose, Aroni, Nadabu na Abihu na wazee sabini wa Israeli wakapanda mlimani, wakamwona Mungu wa Israeli. Chini ya miguu yake kulikuwa na kitu kama sakafu ya mawe ya johari ya rangi ya samawati, kikiwa safi kama mbingu angavu. Na Mungu hakuwadhuru hao viongozi wa watu wa Israeli. Walimwona Mungu, wakala na kunywa.
Kutoka 24:3-11 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Musa akaenda akawaambia watu maneno yote ya BWANA, na hukumu zake zote; watu wote wakajibu kwa sauti moja, wakasema, Maneno yote aliyoyanena BWANA tutayatenda. Basi Musa akayaandika maneno yote ya BWANA, akaondoka asubuhi na mapema, akajenga madhabahu chini ya mlima, na nguzo kumi na mbili, kwa hesabu ya makabila kumi na mawili ya Israeli, akapeleka vijana wa wana wa Israeli, waliotoa sadaka za kuteketezwa, wakamchinjia BWANA sadaka za amani za ng'ombe. Musa akatwaa nusu ya ile damu, akaitia katika mabakuli; na nusu ya ile damu akainyunyiza juu ya madhabahu. Kisha akakitwaa Kitabu cha Agano akakisoma masikioni mwa watu; wakasema, Hayo yote aliyoyanena BWANA tutayatenda, nasi tutatii. Musa akaitwaa ile damu, akawanyunyizia watu, akasema, Hii ndiyo damu ya agano alilolifanya BWANA pamoja nanyi katika maneno haya yote. Ndipo akakwea juu, Musa, na Haruni, na Nadabu, na Abihu, na watu sabini miongoni mwa wazee wa Israeli; wakamwona Mungu wa Israeli; chini ya miguu yake palikuwa na kama sakafu iliyofanyizwa kwa yakuti samawi, kama zile mbingu zenyewe kwa usafi wake. Naye hakuweka mkono wake juu ya hao wakuu wa wana wa Israeli; nao wakamwona Mungu, wakala na kunywa.
Kutoka 24:3-11 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Mose alipokwenda na kuwaambia watu maneno yote na sheria zote za BWANA, wakaitikia kwa sauti moja, “Kila kitu alichosema BWANA tutakifanya.” Ndipo Mose akaandika kila kitu BWANA alichokuwa amesema. Akaamka kesho yake asubuhi na mapema na kujenga madhabahu chini ya mlima na kusimamisha nguzo kumi na mbili za mawe kuwakilisha makabila kumi na mawili ya Israeli. Kisha akawatuma vijana wanaume wa Kiisraeli, nao wakatoa sadaka za kuteketezwa na dhabihu za mafahali wachanga kuwa sadaka za amani kwa BWANA. Mose akachukua nusu ya damu ya wale wanyama na kuiweka kwenye mabakuli na nusu nyingine akainyunyiza juu ya madhabahu. Kisha akachukua kile Kitabu cha Agano na kuwasomea watu. Nao wakajibu, “Tutafanya kila kitu alichosema BWANA, nasi tutatii.” Ndipo Mose akachukua ile damu, akawanyunyizia wale watu, akasema, “Hii ni damu ya agano ambalo BWANA amelifanya nanyi kufuatana na maneno haya yote.” Mose na Aroni, Nadabu na Abihu, pamoja na wazee sabini wa Israeli wakapanda mlimani, nao wakamwona Mungu wa Israeli. Chini ya miguu yake kulikuwa na kitu kama sakafu ya mawe ya yakuti samawi, iliyo safi kama anga angavu. Lakini Mungu hakuinua mkono wake dhidi ya hawa viongozi wa Waisraeli; walimwona Mungu, nao wakala na kunywa.