Waefeso 5:1-7
Waefeso 5:1-7 Biblia Habari Njema (BHN)
Kwa hiyo, mwigeni Mungu, maana nyinyi ni watoto wake wapenzi. Upendo uongoze maisha yenu kama vile Kristo alivyotupenda, na kwa ajili yetu akajitoa mwenyewe kama tambiko yenye harufu nzuri na sadaka impendezayo Mungu. Kwa vile nyinyi ni watu wa Mungu, basi uasherati, uchafu wowote ule au choyo visitajwe kamwe miongoni mwenu. Tena maneno ya aibu, ya upuuzi au ubishi, yote hayo hayafai kwenu; maneno ya kumshukuru Mungu ndiyo yanayofaa. Jueni wazi kwamba mwasherati yeyote au mchafu au mchoyo, (ambao ni sawa na kuabudu sanamu), au mtu yeyote wa aina hiyo hataambulia chochote katika ufalme wa Kristo na wa Mungu. Msikubali kudanganywa na mtu kwa maneno matupu; maana, kwa sababu ya mambo kama hayo ghadhabu ya Mungu huwajia wote wasiomtii. Basi, msishirikiane nao.
Waefeso 5:1-7 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Hivyo mwigeni Mungu, kama watoto wanaopendwa; mkaende katika upendo, kama Kristo naye alivyowapenda ninyi tena akajitoa kwa ajili yetu, sadaka na dhabihu kwa Mungu, kuwa harufu ya manukato. Lakini uasherati usitajwe kwenu kamwe, wala uchafu wowote wa kutamani, kama iwastahilivyo watakatifu; wala aibu wala maneno ya upuzi wala ubishi; hayo hayapendezi; bali kuwepo kushukuru. Maana neno hili mnalijua hakika, ya kwamba hakuna mwasherati wala mchafu wala mwenye tamaa, (ndiye mwabudu sanamu), aliye na urithi katika ufalme wa Kristo na Mungu. Mtu asiwadanganye kwa maneno yasiyo na maana; kwa kuwa kwa sababu ya hayo hasira ya Mungu huwajia wana wa uasi. Basi msishirikiane nao.
Waefeso 5:1-7 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Hivyo mfuateni Mungu, kama watoto wanaopendwa; mkaenende katika upendo, kama Kristo naye alivyowapenda ninyi tena akajitoa kwa ajili yetu, sadaka na dhabihu kwa Mungu, kuwa harufu ya manukato. Lakini uasherati usitajwe kwenu kamwe, wala uchafu wo wote wa kutamani, kama iwastahilivyo watakatifu; wala aibu wala maneno ya upuzi wala ubishi; hayo hayapendezi; bali afadhali kushukuru. Maana neno hili mnalijua hakika, ya kwamba hakuna mwasherati wala mchafu wala mwenye tamaa, ndiye mwabudu sanamu, aliye na urithi katika ufalme wa Kristo na Mungu. Mtu asiwadanganye kwa maneno yasiyo na maana; kwa kuwa kwa sababu ya hayo hasira ya Mungu huwajia wana wa uasi. Basi msishirikiane nao.
Waefeso 5:1-7 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)
Kwa hiyo, mfuateni Mungu kama watoto wanaopendwa, mkiishi maisha ya upendo, kama vile Al-Masihi alivyotupenda sisi akajitoa kwa ajili yetu kuwa sadaka yenye harufu nzuri na dhabihu kwa Mungu. Lakini uasherati usitajwe miongoni mwenu kamwe, wala uchafu wa aina yoyote, wala tamaa, kwa sababu mambo haya hayastahili miongoni mwa watakatifu wa Mungu. Wala pasiwepo mazungumzo machafu ya aibu, au maneno ya upuzi au mzaha, ambayo hayafai, badala yake mshukuruni Mungu. Kwa habari ya mambo haya mjue hakika kwamba: Mwasherati, wala mtu mwovu, wala mwenye tamaa mbaya (mtu kama huyo ni mwabudu sanamu) kamwe hataurithi ufalme wa Al-Masihi na wa Mungu. Mtu yeyote na asiwadanganye kwa maneno matupu, kwa kuwa hasira ya Mungu huwaka kwa sababu ya mambo kama hayo juu ya wale wasiomtii. Kwa hiyo, msishirikiane nao.