Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Waefeso 5

5
Kuenenda katika nuru
1Kwa hiyo, mfuateni Mungu kama watoto wanaopendwa, 2mkiishi maisha ya upendo, kama vile Al-Masihi alivyotupenda sisi akajitoa kwa ajili yetu kuwa sadaka yenye harufu nzuri na dhabihu kwa Mungu.
3Lakini uasherati usitajwe miongoni mwenu kamwe, wala uchafu wa aina yoyote, wala tamaa, kwa sababu mambo haya hayastahili miongoni mwa watakatifu wa Mungu. 4Wala pasiwepo mazungumzo machafu ya aibu, au maneno ya upuzi au mzaha, ambayo hayafai, badala yake mshukuruni Mungu. 5Kwa habari ya mambo haya mjue hakika kwamba: Mwasherati, wala mtu mwovu, wala mwenye tamaa mbaya (mtu kama huyo ni mwabudu sanamu) kamwe hataurithi ufalme wa Al-Masihi na wa Mungu. 6Mtu yeyote na asiwadanganye kwa maneno matupu, kwa kuwa hasira ya Mungu huwaka kwa sababu ya mambo kama hayo juu ya wale wasiomtii. 7Kwa hiyo, msishirikiane nao.
8Kwa maana zamani ninyi mlikuwa giza, lakini sasa ninyi ni nuru katika Bwana Isa. Nendeni kama watoto wa nuru 9(kwa kuwa tunda la nuru hupatikana katika wema wote, haki na kweli), 10nanyi tafuteni yale yanayompendeza Bwana Isa. 11Msishiriki matendo ya giza yasiyofaa, bali yafichueni. 12Kwa maana ni aibu hata kutaja mambo yale ambayo wasiotii wanayafanya sirini. 13Lakini kila kitu kilichowekwa nuruni, huonekana, 14kwa kuwa nuru ndiyo hufanya kila kitu kionekane. Hii ndiyo sababu imesemekana:
“Amka, wewe uliyelala,
ufufuke kutoka kwa wafu,
naye Al-Masihi atakuangazia.”
15Kwa hiyo angalieni sana jinsi mnavyoenenda, si kama watu wasio na hekima, bali kama wenye hekima, 16mkiukomboa wakati, kwa sababu nyakati hizi ni za uovu. 17Kwa hiyo msiwe wajinga, bali mpate kujua nini mapenzi ya Bwana Isa. 18Pia msilewe kwa mvinyo, ambamo mna upotovu, bali mjazwe Roho wa Mungu. 19Msemezane ninyi kwa ninyi kwa zaburi, nyimbo na tenzi za rohoni, mkimwimbia na kumsifu Bwana Isa mioyoni mwenu, 20siku zote mkimshukuru Mungu Baba#5:20 Kwa mwanadamu, Mwenyezi Mungu ni Baba kupitia uhusiano unaopatikana katika kumtumaini Isa Al-Masihi. Mwenyezi kwa kila jambo katika Jina la Bwana wetu Isa Al-Masihi.
21Nyenyekeaneni ninyi kwa ninyi kutokana na kumcha Al-Masihi.
Mafundisho kuhusu wake na waume
22Ninyi wake, watiini waume zenu kama vile mnavyomtii Bwana Isa. 23Kwa maana mume ni kichwa cha mkewe kama vile Al-Masihi alivyo kichwa cha jumuiya ya waumini, ambayo ni mwili wake, naye Al-Masihi ni Mwokozi wake. 24Basi, kama vile jumuiya ya waumini wanavyomtii Al-Masihi, vivyo hivyo na wake nao imewapasa kuwatii waume zao kwa kila jambo.
25Ninyi waume, wapendeni wake zenu, kama vile Al-Masihi alivyoipenda jumuiya ya waumini na akajitoa kwa ajili yake, 26kusudi aifanye takatifu, akiitakasa kwa kuiosha kwa maji katika neno lake, 27apate kujiletea jumuiya tukufu isiyo na doa wala kunyanzi au waa lolote, bali takatifu na isiyo na hatia. 28Vivyo hivyo imewapasa waume kuwapenda wake zao kama miili yao wenyewe. Ampendaye mkewe hujipenda mwenyewe. 29Hakuna mtu anayeuchukia mwili wake mwenyewe, bali huulisha na kuutunza vizuri, kama Al-Masihi anavyoitunza jumuiya yake ya waumini. 30Sisi tu viungo vya mwili wake. 31“Kwa sababu hii, mwanaume atamwacha baba yake na mama yake, naye ataambatana na mkewe, na hao wawili watakuwa mwili mmoja.”#5:31 Mwanzo 2:24 32Siri hii ni kubwa, bali mimi nanena kuhusu Al-Masihi na jumuiya ya waumini wake. 33Hata hivyo, kila mmoja wenu ampende mkewe kama anavyoipenda nafsi yake mwenyewe, naye mke lazima amheshimu mumewe.

Iliyochaguliwa sasa

Waefeso 5: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia