Kumbukumbu la Sheria 1:41-46
Kumbukumbu la Sheria 1:41-46 Biblia Habari Njema (BHN)
“Kisha mkanijibu, ‘Sisi tumemtendea dhambi Mwenyezi-Mungu, lakini sasa tutakwenda na kupigana kama Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, alivyotuamuru’. Hivyo, kila mmoja wenu akajitayarisha kupigana vita; maana mlifikiri kwamba lingekuwa jambo rahisi kuivamia nchi hiyo ya milima. Naye Mwenyezi-Mungu akaniambia, ‘Waambie hao watu wasiende kupigana kwa sababu sipo pamoja nao; wasiende, wasije wakashindwa na adui zao’. Basi, mimi niliwaambieni hivyo, lakini nyinyi hamkusikia. Badala yake mlikataa kufuata agizo la Mwenyezi-Mungu, bila kujali mkaingia katika nchi hiyo ya milima. Hapo, Waamori waliokuwa wanaishi katika eneo hilo la milimani wakateremka kuwashambulia na kama wafanyavyo nyuki wakawapiga huko Seiri mpaka Horma. Ndipo mliporudi, mkamlilia Mwenyezi-Mungu, lakini Mwenyezi-Mungu hakuwasikiliza wala hakuwajali. Basi, mkabaki huko Kadeshi kwa muda mrefu ambao mlikaa huko.
Kumbukumbu la Sheria 1:41-46 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ndipo mkanijibu, mkaniambia, Sisi tumefanya dhambi juu ya BWANA, tutakwea kupigana kwa mfano wa yote tuliyoamriwa na BWANA. Mkajihami kila mtu silaha zake za vita, mkafanya wepesi kukwea mlimani. BWANA akaniambia, Waambie, Msiende, wala msipigane; kwani mimi siko kati yenu; msije mkapigwa mbele ya adui zenu. Hata ingawa niliwaambia, hamkunisikiza, bali mliasi amri ya Bwana, makajiamini na kulewa mlimani. Na Waamori waliokuwa wakikaa katika mlima huo, waliwatokea juu yenu, wakawafukuza, kama wafukuzwao na nyuki, wakawapigia Seiri mpaka Horma. Mkarudi mkalia mbele za BWANA; BWANA asiisikize sauti yenu, wala hakuelekeza masikio yake kwenu. Ndipo mkakaa Kadeshi siku nyingi, kwa kadiri ya hizo siku mlizokaa.
Kumbukumbu la Sheria 1:41-46 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ndipo mkanijibu, mkaniambia, Sisi tumefanya dhambi juu ya BWANA, tutakwea kupigana kwa mfano wa yote tuliyoamriwa na BWANA. Mkajifunga kila mtu silaha zake za vita, mkafanya wepesi kukwea mlimani. BWANA akaniambia, Uwaambie, Msiende, wala msipigane; kwani mimi si kati yenu; msije mkapigwa mbele ya adui zenu. Basi niliwaambia, msinisikize, bali mliasi amri ya BWANA, mkajikinai, na kukwea mlimani. Na Waamori waliokuwa wakikaa katika mlima huo, waliwatokea juu yenu, wakawafukuza, kama wafukuzwao na nyuki, wakawapomoshea Seiri mpaka Horma. Mkarudi mkalia mbele za BWANA; BWANA asiisikize sauti yenu, wala hakuelekeza masikio yake kwenu. Ndipo mkakaa Kadeshi siku nyingi, kwa kadiri ya hizo siku mlizokaa.
Kumbukumbu la Sheria 1:41-46 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)
Ndipo mkanijibu, “Tumemtenda Mwenyezi Mungu dhambi. Tutaenda kupigana, kama Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, alivyotuamuru.” Hivyo kila mmoja wenu akachukua silaha zake, huku mkifikiri kuwa ni rahisi kukwea katika nchi ya vilima. Lakini Mwenyezi Mungu aliniambia, “Waambie, ‘Msipande kupigana, kwa sababu sitakuwa pamoja nanyi. Mtashindwa na adui zenu.’ ” Hivyo niliwaambia, lakini hamkutaka kusikia. Mliasi dhidi ya amri ya Mwenyezi Mungu, na katika kiburi chenu mlienda katika nchi ya vilima. Waamori ambao waliishi katika vilima hivyo waliinuka dhidi yenu, wakawafukuza kama kundi la nyuki wakiwapiga njia yote ya Seiri hadi Horma. Mlirudi na kulia mbele za Mwenyezi Mungu, lakini Mungu hakusikiliza kilio chenu, wala hakuwajali. Hivyo mlikaa Kadeshi kwa siku nyingi, kwa muda ule wote mliokaa huko.