Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Danieli 3:19-30

Danieli 3:19-30 Biblia Habari Njema (BHN)

Hapo, mfalme Nebukadneza akawaka hasira, sura yake ikabadilika kwa chuki dhidi ya Shadraki, Meshaki na Abednego. Akaamuru mwako wa moto wa tanuri uongezwe mara saba kuliko kawaida yake. Akaamuru watu fulani wenye nguvu kabisa katika jeshi lake wawafunge Shadraki, Meshaki na Abednego na kuwatupa katika ile tanuri ya moto mkali. Basi, vijana hao wakafungwa hali wamevaa makoti yao, kanzu zao, kofia na mavazi yao mengine, wakatupwa katikati ya ile tanuri ya moto mkali. Kwa vile amri ya mfalme ilikuwa kali, ule moto ulikuwa umewashwa ukawa mkali sana, hata ndimi za moto zikawateketeza wale watu waliowapeleka Shadraki, Meshaki na Abednego. Ndipo Shadraki, Meshaki na Abednego, wakiwa wamefungwa, wakatumbukia katika ile tanuri ya moto mkali. Basi, mfalme Nebukadneza akashangaa, akainuka kwa haraka na kuwauliza washauri wake, “Je, hatukuwafunga watu watatu na kuwatupa motoni?” Nao wakamjibu mfalme, “Naam, mfalme! Ndivyo!” Kisha akauliza, “Lakini sasa mbona ninaona watu wanne wakitembeatembea humo motoni bila kufungwa na wala hawadhuriki, na mtu wa nne anaonekana kama mwana wa miungu?” Basi, mfalme Nebukadneza akaukaribia mlango wa tanuri ya moto mkali, akaita, “Shadraki, Meshaki na Abednego, watumishi wa Mungu Mkuu, tokeni mje hapa!” Shadraki, Meshaki na Abednego wakatoka motoni. Maliwali, wasimamizi, wakuu wa mikoa na washauri wa mfalme, wote wakakusanyika pamoja, wakaona ya kuwa ule moto haukuweza kuwaunguza hao watatu. Nywele zao hazikuungua, mavazi yao hayakuungua, wala hawakuwa na harufu yoyote ya moto. Basi, mfalme Nebukadneza akasema, “Na asifiwe Mungu wa Shadraki, Meshaki na Abednego kwa kuwa alimtuma malaika wake na kuwaokoa watumishi wake ambao wanamtegemea. Wao walikataa kutii amri yangu ya kifalme, wakaitoa mhanga miili yao badala ya kuabudu mungu mwingine, ila Mungu wao peke yake. Kwa hiyo, naamuru kwamba watu wa kabila lolote, taifa lolote au lugha yoyote, watakaosema kitu chochote dhidi ya Mungu wa Shadraki, Meshaki na Abednego, watangolewa viungo vyao kimojakimoja na nyumba zao zitabomolewa. Maana hakuna mungu mwingine awezaye kuokoa namna hii.” Basi, mfalme Nebukadneza akawapandisha vyeo Shadraki, Meshaki na Abednego katika mkoa wa Babuloni.

Shirikisha
Soma Danieli 3

Danieli 3:19-30 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Ndipo Nebukadneza akajaa ghadhabu, na sura ya uso wake ikabadilika juu ya Shadraka, na Meshaki, na Abednego, basi akatoa amri watie moto ile tanuri mara saba kuliko desturi yake ya kutiwa moto. Kisha akawaamuru baadhi ya watu mashujaa wa jeshi lake kuwafunga Shadraka, na Meshaki, na Abednego, na kuwatupa katika lile tanuri lililokuwa likiwaka moto. Basi watu hao wakafungwa, wakiwa wamevaa suruali zao, na kanzu zao, na majoho yao, na mavazi yao mengine, wakatupwa katikati ya lile tanuri lililokuwa likiwaka moto. Basi kwa sababu amri ya mfalme ilikuwa ni kali, na lile tanuri lilikuwa lina moto sana, mwako wa ule moto ukawaua wale watu waliowashika Shadraka, na Meshaki, na Abednego. Na watu hao watatu, Shadraka, na Meshaki, na Abednego, wakaanguka, wakiwa wamefungwa, katikati ya lile tanuri lililokuwa linawaka moto. Ndipo Nebukadneza akastaajabu, akainuka kwa haraka; akanena, akawaambia mawaziri wake, Je! Hatukutupa watu watatu, wakiwa wamefungwa, katikati ya moto? Wakajibu, wakamwambia mfalme, Kweli, Ee mfalme. Akajibu, akasema, Tazama, mimi naona watu wanne, nao wamefunguliwa, wanatembea katikati ya moto hali hawana dhara; na sura yake yule wa nne ni mfano wa mwana wa miungu. Kisha Nebukadneza akaukaribia mlango wa lile tanuri lililokuwa linawaka moto. Akanena, akasema, Enyi Shadraka, na Meshaki, na Abednego, watumishi wa Mungu Aliye Juu, tokeni, mje huku. Ndipo Shadraka, na Meshaki, na Abednego, wakatoka katika ule moto. Na maamiri, wasimamizi, watawala, na mahakimu, waliokuwa wamekusanyika pamoja, wakawaona watu hao, ya kuwa ule moto ulikuwa hauna nguvu juu ya miili yao, wala nywele za vichwa vyao hazikuteketea, wala suruali zao hazikubadilika, wala harufu ya moto haikuwapata hata kidogo. Nebukadneza akanena, akasema, Na ahimidiwe Mungu wa Shadraka, na Meshaki, na Abednego; aliyemtuma malaika wake, akawaokoa watumishi wake waliomtumaini, wakaligeuza neno la mfalme, na kujitoa miili yao ili wasimtumikie mungu mwingine, wala kumwabudu, ila Mungu wao wenyewe. Basi mimi naweka amri ya kuwa kila kabila la watu, na kila taifa, na kila lugha, watakaonena neno lolote lisilopasa juu ya huyo Mungu wa Shadraka, na Meshaki, na Abednego, watakatwa vipande vipande, na nyumba zao zitafanywa jaa; kwa kuwa hakuna Mungu mwingine awezaye kuokoa namna hii. Kisha mfalme akawakuza Shadraka, na Meshaki, na Abednego, katika wilaya ya Babeli.

Shirikisha
Soma Danieli 3

Danieli 3:19-30 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Ndipo Nebukadreza akajaa ghadhabu, na sura ya uso wake ikabadilika juu ya Shadraka, na Meshaki, na Abednego, basi akatoa amri watie moto ile tanuru mara saba kuliko desturi yake ya kutiwa moto. Kisha akawaamuru baadhi ya watu mashujaa wa jeshi lake kuwafunga Shadraka, na Meshaki, na Abednego, na kuwatupa katika ile tanuru iliyokuwa ikiwaka moto. Basi watu hao wakafungwa, hali wamevaa suruali zao, na kanzu zao, na joho zao, na mavazi yao mengine, wakatupwa katikati ya ile tanuru iliyokuwa ikiwaka moto. Basi kwa sababu amri ya mfalme ilikuwa ni kali, na ile tanuru ilikuwa ina moto sana, mwako wa ule moto ukawaua wale watu waliowashika Shadraka, na Meshaki, na Abednego. Na watu hao watatu, Shadraka, na Meshaki, na Abednego, wakaanguka, hali wamefungwa, katikati ya ile tanuru iliyokuwa inawaka moto. Ndipo Nebukadreza akastaajabu, akainuka kwa haraka; akanena, akawaambia mawaziri wake, Je! Hatukutupa watu watatu, hali wamefungwa, katikati ya moto? Wakajibu, wakamwambia mfalme, Kweli, Ee mfalme. Akajibu, akasema, Tazama, mimi naona watu wanne, nao wamefunguliwa, wanatembea katikati ya moto hali hawana dhara; na sura yake yule wa nne ni mfano wa mwana wa miungu. Kisha Nebukadreza akaukaribia mdomo wa ile tanuru iliyokuwa inawaka moto. Akanena, akasema, Enyi Shadraka, na Meshaki, na Abednego, watumishi wa Mungu Aliye juu, tokeni, mje huku. Ndipo Shadraka, na Meshaki, na Abednego, wakatoka katika ule moto. Na maamiri, na manaibu, na maliwali, na mawaziri, waliokuwa wamekusanyika pamoja, wakawaona watu hao, ya kuwa ule moto ulikuwa hauna nguvu juu ya miili yao, wala nywele za vichwa vyao hazikuteketea, wala suruali zao hazikubadilika, wala harufu ya moto haikuwapata hata kidogo. Nebukadreza akanena, akasema, Na ahimidiwe Mungu wa Shadraka, na Meshaki, na Abednego; aliyemtuma malaika wake, akawaokoa watumishi wake waliomtumaini, wakaligeuza neno la mfalme, na kujitoa miili yao ili wasimtumikie mungu mwingine, wala kumwabudu, ila Mungu wao wenyewe. Basi mimi naweka amri ya kuwa kila kabila ya watu, na kila taifa, na kila lugha, watakaonena neno lo lote lisilopasa juu ya huyo Mungu wa Shadraka, na Meshaki, na Abednego, watakatwa vipande vipande, na nyumba zao zitafanywa jaa; kwa kuwa hakuna Mungu mwingine awezaye kuokoa namna hii. Kisha mfalme akawakuza Shadraka, na Meshaki, na Abednego, katika wilaya ya Babeli.

Shirikisha
Soma Danieli 3

Danieli 3:19-30 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)

Ndipo Nebukadneza akawa na ghadhabu kali sana kwa Shadraki, Meshaki na Abednego, nayo nia yake ikabadilika kwao. Akaagiza tanuru lichochewe moto mara saba kuliko kawaida yake, na akawaamuru baadhi ya askari wake wenye nguvu zaidi katika jeshi lake kuwafunga Shadraki, Meshaki na Abednego, na kuwatupa ndani ya tanuru lililowaka moto. Hivyo watu hawa walifungwa na kutupwa ndani ya tanuru hilo wakiwa wamevaa majoho yao, suruali, vilemba, na nguo zao nyingine. Amri ya mfalme ilikuwa ya haraka sana na tanuru lilikuwa na moto mkali kiasi kwamba miali ya moto iliwaua wale askari waliowapeleka Shadraki, Meshaki na Abednego. Watu hawa watatu walianguka ndani ya tanuru hilo la moto wakiwa wamefungwa kwa uthabiti sana. Ndipo Mfalme Nebukadneza akashangaa, akainuka kwa haraka na kuwauliza washauri wake, “Je, hawakuwa watu watatu ambao tuliwafunga na kuwatupa ndani ya moto?” Washauri wakajibu, “Hakika, ee mfalme.” Mfalme akasema, “Tazama! Naona watu wanne wakitembeatembea ndani ya moto; hawajafungwa wala kudhurika, naye mtu yule wa nne anaonekana kama mwana wa miungu.” Ndipo Nebukadneza akaukaribia mdomo wa lile tanuru lililowaka moto na kuita kwa sauti kuu, “Shadraki, Meshaki na Abednego, watumishi wa Mungu Aliye Juu Sana, tokeni! Njooni hapa!” Ndipo Shadraki, Meshaki na Abednego wakatoka ndani ya moto. Nao maliwali, wasimamizi, watawala na washauri wa mfalme wakakusanyika kuwazunguka. Waliona kwamba moto haukudhuru miili yao, wala unywele wa vichwa vyao haukuungua, majoho yao hayakuungua, wala hawakuwa na harufu ya moto. Ndipo Nebukadneza akasema, “Ahimidiwe Mungu wa Shadraki, Meshaki na Abednego, ambaye amemtuma malaika wake na kuwaokoa watumishi wake. Walimtumaini na kukaidi amri ya mfalme, nao wakawa tayari kufa kuliko kutumikia au kuabudu mungu mwingine yeyote isipokuwa Mungu wao. Kwa hiyo ninaamuru kwamba watu wa taifa lolote au lugha yoyote watakaosema kitu chochote dhidi ya Mungu wa Shadraki, Meshaki na Abednego wakatwe vipande vipande, na nyumba zao zifanywe kuwa malundo ya kokoto, kwa maana hakuna mungu mwingine awezaye kuokoa namna hii.” Kisha mfalme akawapandisha vyeo Shadraki, Meshaki na Abednego katika jimbo la Babeli.

Shirikisha
Soma Danieli 3