Danieli 3:19-30
Danieli 3:19-30 SRUV
Ndipo Nebukadneza akajaa ghadhabu, na sura ya uso wake ikabadilika juu ya Shadraka, na Meshaki, na Abednego, basi akatoa amri watie moto ile tanuri mara saba kuliko desturi yake ya kutiwa moto. Kisha akawaamuru baadhi ya watu mashujaa wa jeshi lake kuwafunga Shadraka, na Meshaki, na Abednego, na kuwatupa katika lile tanuri lililokuwa likiwaka moto. Basi watu hao wakafungwa, wakiwa wamevaa suruali zao, na kanzu zao, na majoho yao, na mavazi yao mengine, wakatupwa katikati ya lile tanuri lililokuwa likiwaka moto. Basi kwa sababu amri ya mfalme ilikuwa ni kali, na lile tanuri lilikuwa lina moto sana, mwako wa ule moto ukawaua wale watu waliowashika Shadraka, na Meshaki, na Abednego. Na watu hao watatu, Shadraka, na Meshaki, na Abednego, wakaanguka, wakiwa wamefungwa, katikati ya lile tanuri lililokuwa linawaka moto. Ndipo Nebukadneza akastaajabu, akainuka kwa haraka; akanena, akawaambia mawaziri wake, Je! Hatukutupa watu watatu, wakiwa wamefungwa, katikati ya moto? Wakajibu, wakamwambia mfalme, Kweli, Ee mfalme. Akajibu, akasema, Tazama, mimi naona watu wanne, nao wamefunguliwa, wanatembea katikati ya moto hali hawana dhara; na sura yake yule wa nne ni mfano wa mwana wa miungu. Kisha Nebukadneza akaukaribia mlango wa lile tanuri lililokuwa linawaka moto. Akanena, akasema, Enyi Shadraka, na Meshaki, na Abednego, watumishi wa Mungu Aliye Juu, tokeni, mje huku. Ndipo Shadraka, na Meshaki, na Abednego, wakatoka katika ule moto. Na maamiri, wasimamizi, watawala, na mahakimu, waliokuwa wamekusanyika pamoja, wakawaona watu hao, ya kuwa ule moto ulikuwa hauna nguvu juu ya miili yao, wala nywele za vichwa vyao hazikuteketea, wala suruali zao hazikubadilika, wala harufu ya moto haikuwapata hata kidogo. Nebukadneza akanena, akasema, Na ahimidiwe Mungu wa Shadraka, na Meshaki, na Abednego; aliyemtuma malaika wake, akawaokoa watumishi wake waliomtumaini, wakaligeuza neno la mfalme, na kujitoa miili yao ili wasimtumikie mungu mwingine, wala kumwabudu, ila Mungu wao wenyewe. Basi mimi naweka amri ya kuwa kila kabila la watu, na kila taifa, na kila lugha, watakaonena neno lolote lisilopasa juu ya huyo Mungu wa Shadraka, na Meshaki, na Abednego, watakatwa vipande vipande, na nyumba zao zitafanywa jaa; kwa kuwa hakuna Mungu mwingine awezaye kuokoa namna hii. Kisha mfalme akawakuza Shadraka, na Meshaki, na Abednego, katika wilaya ya Babeli.