Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Danieli 3:1-18

Danieli 3:1-18 Biblia Habari Njema (BHN)

Mfalme Nebukadneza alitengeneza sanamu ya dhahabu, yenye kimo mita ishirini na nane na upana mita tatu. Aliisimamisha katika sehemu tambarare ya Dura, mkoani Babuloni. Kisha mfalme akaamuru maliwali, wasimamizi, wakuu wa mikoa, washauri, watunza hazina, majaji, mahakimu na maofisa wote wa mikoa wahudhurie sherehe ya kuzindua rasmi sanamu aliyoisimamisha. Basi, maliwali, wasimamizi, wakuu wa mikoa, washauri, watunza hazina, majaji, mahakimu na maofisa wote wa mikoa wakakusanyika tayari kwa uzinduzi wa sanamu aliyosimamisha mfalme Nebukadneza. Mpiga mbiu akatangaza kwa sauti kubwa, “Enyi watu wa makabila yote, mataifa yote na lugha zote, mnaamriwa kwamba mkisikia sauti ya baragumu, filimbi, kinubi, zeze, santuri, zumari na sauti za ala nyingine za muziki, lazima mwiname chini na kuiabudu sanamu ya dhahabu aliyosimamisha mfalme Nebukadneza. Na yeyote ambaye hatainama chini na kuiabudu, atatupwa mara moja katika tanuri ya moto mkali.” Kwa hiyo, watu wote, mara waliposikia sauti za baragumu, filimbi, kinubi, zeze, santuri, zumari na sauti za ala nyingine za muziki, walianguka kifudifudi na kuiabudu ile sanamu ya dhahabu ambayo mfalme Nebukadneza aliisimamisha. Wakati huo, baadhi ya Wakaldayo wakajitokeza na kuwashtaki Wayahudi. Walimwambia mfalme Nebukadneza, “Uishi, ee mfalme! Wewe, ee mfalme, ulitoa amri kuwa kila mtu anaposikia sauti ya baragumu, filimbi, kinubi, zeze, santuri, zumari na kila aina ya muziki, ainame chini na kuiabudu ile sanamu ya dhahabu. Na kwamba mtu yeyote asiyeinama chini na kuiabudu sanamu hiyo, atupwe ndani ya tanuri ya moto mkali. Sasa, kuna Wayahudi fulani uliowateua kushughulikia mambo ya utawala wa mkoa wa Babuloni, yaani Shadraki, Meshaki na Abednego; watu hawa, ee mfalme, hawakuitii amri yako. Wanakataa kuitumikia miungu yako na kuiabudu ile sanamu ya dhahabu uliyoisimamisha.” Hapo mfalme Nebukadneza, huku akiwaka hasira, akaamuru Shadraki, Meshaki na Abednego waletwe mbele yake. Nao wakawaleta mbele ya mfalme. Mfalme Nebukadneza akawauliza, “Je, ni kweli kwamba wewe Shadraki, wewe Meshaki na wewe Abednego, hamuitumikii miungu yangu wala kuiabudu ile sanamu ya dhahabu niliyoisimamisha? Basi, mtakaposikia tena sauti ya baragumu, filimbi, kinubi, zeze, santuri, zumari na sauti za ala nyingine za muziki, je, mko tayari kuinama chini na kuiabudu sanamu niliyotengeneza? Kama mkikataa, mtatupwa mara moja katika tanuri ya moto mkali. Je, ni mungu gani anayeweza kuwaokoa mikononi mwangu?” Shadraki, Meshaki na Abednego wakamjibu mfalme, “Ee Nebukadneza, sisi hatuhitaji kukujibu kuhusu jambo hilo. Ikiwa ndivyo, Mungu wetu ambaye tunamtumikia aweza kutuokoa katika tanuri ya moto mkali; tena atatuokoa mikononi mwako, ee mfalme. Lakini, hata kama haitafanyika hivyo, ujue wazi, ee mfalme, kwamba sisi hatutaitumikia miungu yako wala kuiabudu sanamu ya dhahabu uliyosimamisha.”

Shirikisha
Soma Danieli 3

Danieli 3:1-18 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Nebukadneza, mfalme, alifanya sanamu ya dhahabu, ambayo urefu wake ulikuwa ni dhiraa sitini, na upana wake dhiraa sita; akaisimamisha katika uwanda wa Dura, katika wilaya ya Babeli. Ndipo Nebukadneza akatuma watu kuwakusanya maamiri, wasimamizi, watawala, washauri, watunza hazina, majaji, mahakimu na wakuu wa wilaya zote, ili wahudhurie wakati wa kuizindua ile sanamu, mfalme Nebukadneza aliyoisimamisha. Ndipo maamiri, wasimamizi, watawala, washauri, watunza hazina, majaji, mahakimu na wakuu wa wilaya zote, wakakusanyika ili kuizindua ile sanamu, mfalme Nebukadneza aliyoisimamisha; wakasimama mbele ya ile sanamu, mfalme Nebukadneza aliyoisimamisha. Ndipo mpiga mbiu akapiga kelele akisema, Enyi watu wa kabila zote, na taifa, na lugha, mmeamriwa hivi, wakati mtakapoisikia sauti ya panda, na filimbi, na kinubi, na zeze, na santuri, na zumari, na namna zote za ngoma, lazima kuanguka na kuiabudu sanamu ya dhahabu, mfalme Nebukadneza aliyoisimamisha. Na kila mtu asiyeanguka na kuabudu atatupwa saa iyo hiyo katika tanuri liwakalo moto. Basi wakati huo, watu wa kabila zote walipoisikia sauti ya panda, na filimbi, na kinubi, na zeze, na santuri, na zumari, na namna zote za ngoma, watu wote na mataifa na lugha wakaanguka, wakaiabudu ile sanamu, mfalme Nebukadneza aliyoisimamisha. Basi baadhi ya Wakaldayo wakakaribia, wakaleta mashitaka juu ya Wayahudi. Wakajibu, wakamwambia mfalme Nebukadneza, Ee mfalme, uishi milele. Wewe, Ee mfalme, ulitoa amri ya kwamba kila mtu atakapoisikia sauti ya panda, na filimbi, na kinubi, na zeze, na santuri, na zumari, na namna zote za ngoma, ni lazima aanguke na kuiabudu ile sanamu ya dhahabu; na kila mtu asiyeanguka na kuabudu atatupwa katika tanuri liwakalo moto. Wako Wayahudi kadha wa kadha uliowaweka juu ya mambo ya wilaya ya Babeli, yaani, Shadraka, na Meshaki, na Abednego; watu hawa, Ee mfalme, hawakukujali wewe; hawaitumikii miungu yako, wala kuiabudu ile sanamu ya dhahabu uliyoisimamisha. Basi Nebukadneza akatoa amri kwa hasira na ghadhabu, waletwe hao Shadraka, na Meshaki, na Abednego. Basi wakawaleta watu hao mbele ya mfalme. Nebukadneza akajibu, akawaambia, Enyi Shadraka, na Meshaki, na Abednego, je! Ni kwa makusudi hata hamumtumikii mungu wangu wala kuisujudia sanamu ya dhahabu niliyoisimamisha? Basi sasa, kama mkiwa tayari wakati mtakapoisikia sauti ya panda, na filimbi, na kinubi, na zeze, na santuri, na zumari, na namna zote za ngoma, kuanguka na kuisujudia sanamu niliyoisimamisha, ni vema; bali msipoisujudia, mtatupwa saa iyo hiyo katika tanuri liwakalo moto; naye ni nani Mungu yule atakayewaokoa ninyi mikononi mwangu? Ndipo Shadraka, na Meshaki, na Abednego, wakajibu, wakamwambia mfalme, Ee Nebukadneza, hamna haja kukujibu katika neno hili. Kama ni hivyo, Mungu wetu tunayemtumikia aweza kutuokoa na tanuri liwakalo moto; naye atatuokoa mkononi mwako, Ee mfalme. Bali kama si hivyo, ujue, Ee mfalme, ya kuwa sisi hatukubali kuitumikia miungu yako, wala kuisujudia hiyo sanamu ya dhahabu uliyoisimamisha.

Shirikisha
Soma Danieli 3

Danieli 3:1-18 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Nebukadreza, mfalme, alifanya sanamu ya dhahabu, ambayo urefu wake ulikuwa ni dhiraa sitini, na upana wake dhiraa sita; akaisimamisha katika uwanda wa Dura, katika wilaya ya Babeli. Ndipo Nebukadreza akatuma watu kuwakusanya maamiri, na manaibu, na maliwali, na makadhi, na watunza hazina, na mawaziri, na mawakili, na wakuu wa wilaya zote, ili wahudhurie wakati wa kuizindua ile sanamu, mfalme Nebukadneza aliyoisimamisha. Ndipo maamiri, na manaibu, na maliwali, na makadhi, na watunza hazina, na mawaziri, na mawakili, na wakuu wa wilaya zote, wakakusanyika ili kuizindua ile sanamu, mfalme Nebukadreza aliyoisimamisha; wakasimama mbele ya ile sanamu, mfalme Nebukadreza aliyoisimamisha. Ndipo mpiga mbiu akapiga kelele akisema, Enyi watu wa kabila zote, na taifa, na lugha, mmeamriwa hivi, wakati mtakapoisikia sauti ya panda, na filimbi, na kinubi, na zeze, na santuri, na zomari, na namna zote za ngoma, lazima kuanguka na kuiabudu sanamu ya dhahabu, mfalme Nebukadreza aliyoisimamisha. Na kila mtu asiyeanguka na kuabudu atatupwa saa iyo hiyo katika tanuru ya moto uwakao. Basi wakati huo, watu wa kabila zote walipoisikia sauti ya panda, na filimbi, na kinubi, na zeze, na santuri, na zomari, na namna zote za ngoma, watu wote na mataifa na lugha wakaanguka, wakaiabudu ile sanamu, mfalme Nebukadreza aliyoisimamisha. Basi baadhi ya Wakaldayo wakakaribia, wakaleta mashitaka juu ya Wayahudi. Wakajibu, wakamwambia mfalme Nebukadreza, Ee mfalme, uishi milele. Wewe, Ee mfalme, ulitoa amri ya kwamba kila mtu atakapoisikia sauti ya panda, na filimbi, na kinubi, na zeze, na santuri, na zomari, na namna zote za ngoma, ni lazima aanguke na kuiabudu ile sanamu ya dhahabu; na kila mtu asiyeanguka na kuabudu atatupwa katika tanuru ya moto uwakao. Wako Wayahudi kadha wa kadha uliowaweka juu ya mambo ya wilaya ya Babeli, yaani, Shadraka, na Meshaki, na Abednego; watu hawa, Ee mfalme, hawakukujali wewe; hawaitumikii miungu yako, wala kuiabudu ile sanamu ya dhahabu uliyoisimamisha. Basi Nebukadreza akatoa amri kwa hasira na ghadhabu, waletwe hao Shadraka, na Meshaki, na Abednego. Basi wakawaleta watu hao mbele ya mfalme. Nebukadreza akajibu, akawaambia, Enyi Shadraka, na Meshaki, na Abednego, je! Ni kwa makusudi hata hammtumikii mungu wangu wala kuisujudia sanamu ya dhahabu niliyoisimamisha? Basi sasa, kama mkiwa tayari wakati mtakapoisikia sauti ya panda, na filimbi, na kinubi, na zeze, na santuri, na zomari, na namna zote za ngoma, kuanguka na kuisujudia sanamu niliyoisimamisha, ni vema; bali msipoisujudia, mtatupwa saa iyo hiyo katika tanuru iwakayo moto; naye ni nani Mungu yule atakayewaokoa ninyi na mikono yangu? Ndipo Shadraka, na Meshaki, na Abednego, wakajibu, wakamwambia mfalme, Ee Nebukadreza, hamna haja kukujibu katika neno hili. Kama ni hivyo, Mungu wetu tunayemtumikia aweza kutuokoa na tanuru ile iwakayo moto; naye atatuokoa na mkono wako, Ee mfalme. Bali kama si hivyo, ujue, Ee mfalme, ya kuwa sisi hatukubali kuitumikia miungu yako, wala kuisujudia hiyo sanamu ya dhahabu uliyoisimamisha.

Shirikisha
Soma Danieli 3

Danieli 3:1-18 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Mfalme Nebukadneza alitengeneza sanamu ya dhahabu, yenye kimo cha dhiraa sitini, na upana wa dhiraa sita, akaisimamisha kwenye tambarare ya Dura katika jimbo la nchi ya Babeli. Kisha mfalme akaita wakuu, wasimamizi, watawala, washauri, watunza hazina, waamuzi, mahakimu na maafisa wengine wote wa jimbo kuja kuizindua sanamu ambayo Mfalme Nebukadneza alikuwa ameisimamisha. Basi wakuu, wasimamizi, watawala, washauri, watunza hazina, waamuzi, mahakimu na maafisa wengine wa jimbo walikusanyika ili kuizindua sanamu ile Mfalme Nebukadneza alikuwa ameisimamisha, nao wakasimama mbele ya hiyo sanamu. Ndipo mpiga mbiu akatangaza kwa sauti kubwa, “Enyi watu wa kabila zote, mataifa na watu wa kila lugha, hili ndilo mnaloamriwa kulifanya: Mara mtakaposikia sauti ya baragumu, filimbi, marimba, zeze, kinubi, zumari na aina zote za sauti za ala za uimbaji, lazima mwanguke chini na kuabudu sanamu ya dhahabu ambayo Mfalme Nebukadneza ameisimamisha. Mtu yeyote ambaye hataanguka chini na kuiabudu sanamu hiyo, atatupwa saa iyo hiyo ndani ya tanuru iwakayo moto.” Kwa hiyo, mara waliposikia sauti ya baragumu, filimbi, kinubi, zeze, kinanda na aina zote za ala za uimbaji, watu wa kabila zote, mataifa na watu wa kila lugha wakaanguka chini na kuiabudu ile sanamu ya dhahabu ambayo Mfalme Nebukadneza alikuwa ameisimamisha. Wakati huo baadhi ya Wakaldayo walijitokeza na kuwashtaki Wayahudi. Wakamwambia Mfalme Nebukadneza, “Ee mfalme, uishi milele! Ee mfalme, umetoa amri kwamba kila mmoja atakayesikia sauti ya baragumu, filimbi, kinubi, zeze, kinanda, zumari na aina zote za ala za uimbaji lazima aanguke chini na kuiabudu ile sanamu ya dhahabu, na kwamba yeyote ambaye hataanguka chini na kuiabudu atatupwa saa iyo hiyo ndani ya tanuru iwakayo moto. Lakini wako baadhi ya Wayahudi ambao umewaweka juu ya mambo ya jimbo la Babeli: yaani, Shadraki, Meshaki na Abednego, ambao hawakujali wewe, ee mfalme. Hawaitumikii miungu yako wala kuiabudu ile sanamu ya dhahabu uliyoisimamisha.” Mfalme Nebukadneza, akiwa amekasirika na mwenye ghadhabu kali, akawaita Shadraki, Meshaki na Abednego. Hivyo watu hawa wakaletwa mbele ya mfalme, naye Nebukadneza akawauliza, “Je, ni kweli kwamba ninyi Shadraki, Meshaki na Abednego hamuitumikii miungu yangu wala kuiabudu sanamu ya dhahabu niliyoisimamisha? Basi wakati mtakaposikia sauti ya baragumu, filimbi, marimba, zeze, kinubi, zumari na aina zote za ala za uimbaji, kama mtakuwa tayari kusujudu na kuiabudu hiyo sanamu niliyoitengeneza, vyema sana. Lakini kama hamtaiabudu, mtatupwa saa iyo hiyo ndani ya tanuru iwakayo moto. Naye ni mungu yupi atakayeweza kuwaokoa ninyi, kutoka mkono wangu?” Shadraki, Meshaki na Abednego wakamjibu mfalme, “Ee Nebukadneza, hatuhitaji kujitetea mbele zako kuhusu jambo hili. Ikiwa tutatupwa ndani ya tanuru iwakayo moto, Mungu tunayemtumikia anaweza kutuokoa na moto, naye atatuokoa kutoka mkononi mwako, ee mfalme. Lakini hata ikiwa hatatuokoa, ee mfalme, tunataka ufahamu kwamba, hatutaitumikia miungu yako wala kuiabudu sanamu ya dhahabu uliyoisimamisha.”

Shirikisha
Soma Danieli 3