Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Danieli 3:1-18

Danieli 3:1-18 BHN

Mfalme Nebukadneza alitengeneza sanamu ya dhahabu, yenye kimo mita ishirini na nane na upana mita tatu. Aliisimamisha katika sehemu tambarare ya Dura, mkoani Babuloni. Kisha mfalme akaamuru maliwali, wasimamizi, wakuu wa mikoa, washauri, watunza hazina, majaji, mahakimu na maofisa wote wa mikoa wahudhurie sherehe ya kuzindua rasmi sanamu aliyoisimamisha. Basi, maliwali, wasimamizi, wakuu wa mikoa, washauri, watunza hazina, majaji, mahakimu na maofisa wote wa mikoa wakakusanyika tayari kwa uzinduzi wa sanamu aliyosimamisha mfalme Nebukadneza. Mpiga mbiu akatangaza kwa sauti kubwa, “Enyi watu wa makabila yote, mataifa yote na lugha zote, mnaamriwa kwamba mkisikia sauti ya baragumu, filimbi, kinubi, zeze, santuri, zumari na sauti za ala nyingine za muziki, lazima mwiname chini na kuiabudu sanamu ya dhahabu aliyosimamisha mfalme Nebukadneza. Na yeyote ambaye hatainama chini na kuiabudu, atatupwa mara moja katika tanuri ya moto mkali.” Kwa hiyo, watu wote, mara waliposikia sauti za baragumu, filimbi, kinubi, zeze, santuri, zumari na sauti za ala nyingine za muziki, walianguka kifudifudi na kuiabudu ile sanamu ya dhahabu ambayo mfalme Nebukadneza aliisimamisha. Wakati huo, baadhi ya Wakaldayo wakajitokeza na kuwashtaki Wayahudi. Walimwambia mfalme Nebukadneza, “Uishi, ee mfalme! Wewe, ee mfalme, ulitoa amri kuwa kila mtu anaposikia sauti ya baragumu, filimbi, kinubi, zeze, santuri, zumari na kila aina ya muziki, ainame chini na kuiabudu ile sanamu ya dhahabu. Na kwamba mtu yeyote asiyeinama chini na kuiabudu sanamu hiyo, atupwe ndani ya tanuri ya moto mkali. Sasa, kuna Wayahudi fulani uliowateua kushughulikia mambo ya utawala wa mkoa wa Babuloni, yaani Shadraki, Meshaki na Abednego; watu hawa, ee mfalme, hawakuitii amri yako. Wanakataa kuitumikia miungu yako na kuiabudu ile sanamu ya dhahabu uliyoisimamisha.” Hapo mfalme Nebukadneza, huku akiwaka hasira, akaamuru Shadraki, Meshaki na Abednego waletwe mbele yake. Nao wakawaleta mbele ya mfalme. Mfalme Nebukadneza akawauliza, “Je, ni kweli kwamba wewe Shadraki, wewe Meshaki na wewe Abednego, hamuitumikii miungu yangu wala kuiabudu ile sanamu ya dhahabu niliyoisimamisha? Basi, mtakaposikia tena sauti ya baragumu, filimbi, kinubi, zeze, santuri, zumari na sauti za ala nyingine za muziki, je, mko tayari kuinama chini na kuiabudu sanamu niliyotengeneza? Kama mkikataa, mtatupwa mara moja katika tanuri ya moto mkali. Je, ni mungu gani anayeweza kuwaokoa mikononi mwangu?” Shadraki, Meshaki na Abednego wakamjibu mfalme, “Ee Nebukadneza, sisi hatuhitaji kukujibu kuhusu jambo hilo. Ikiwa ndivyo, Mungu wetu ambaye tunamtumikia aweza kutuokoa katika tanuri ya moto mkali; tena atatuokoa mikononi mwako, ee mfalme. Lakini, hata kama haitafanyika hivyo, ujue wazi, ee mfalme, kwamba sisi hatutaitumikia miungu yako wala kuiabudu sanamu ya dhahabu uliyosimamisha.”

Soma Danieli 3