Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Danieli 2:1-28

Danieli 2:1-28 Biblia Habari Njema (BHN)

Mnamo mwaka wa pili wa utawala wake, mfalme Nebukadneza aliota ndoto, akawa na wasiwasi sana rohoni hata usingizi ukamtoweka. Basi, mfalme akaamuru waganga, walozi na wachawi wa Wakaldayo waletwe ili wamfasirie ndoto yake. Wote wakaja na kusimama mbele yake. Mfalme Nebukadneza akawaambia, “Niliota ndoto, nayo inanipa wasiwasi, nami nataka nijulishwe tafsiri yake.” Wale Wakaldayo wakamwambia mfalme kwa Kiaramu, “Uishi, ee mfalme! Tusimulie ndoto yako nasi watumishi wako tutakufasiria.” Mfalme akawaambia, “Nimetoa kauli yangu kamili: Ikiwa hamtanijulisha ndoto yenyewe na maana yake, mtangolewa viungo vyenu kimojakimoja, na nyumba zenu zitabomolewa. Lakini mkiniambia hiyo ndoto na maana yake, nitawapa zawadi, tuzo na heshima kubwa. Basi, nijulisheni ndoto hiyo na maana yake!” Wao wakamjibu mara ya pili, “Mfalme, tusimulie ndoto hiyo, nasi watumishi wako tutakufasiria.” Hapo mfalme akawakatiza kwa kusema, “Najua kweli kwamba mnajaribu kupoteza wakati kwa kuwa mnaona kwamba nilikwisha toa kauli yangu kamili, kwamba msiponijulisha ndoto hiyo, adhabu yenu ni moja. Mmepatana kunidanganyadanganya na kunilaghailaghai huku muda unapita. Niambieni ndoto hiyo, nami nitajua kuwa mnaweza kunijulisha maana yake.” Wale Wakaldayo wakamjibu: “Mfalme, hakuna mtu yeyote duniani awezaye kutimiza matakwa yako. Hakuna mfalme yeyote, hata awe mkuu na mwenye nguvu kiasi gani aliyepata kuwauliza waganga au walozi au Wakaldayo jambo kama hilo. Jambo unalouliza, ee mfalme, ni gumu. Hakuna mtu anayeweza kukufunulia isipokuwa miungu peke yake ambayo haikai miongoni mwa wanaadamu.” Kusikia hivyo, mfalme Nebukadneza alikasirika na kughadhibika sana, akaamuru wenye hekima wote wa Babuloni waangamizwe. Basi, tangazo likaenea kuwa wenye hekima wote wauawe; Danieli na wenzake, nao pia wakatafutwa ili wauawe. Basi, Danieli, kwa tahadhari na busara, alimwendea Arioko, mkuu wa kikosi cha walinzi wa mfalme na ambaye alipewa jukumu la kuwaua wenye hekima wa Babuloni, akamwuliza, “Kwa nini amri ya mfalme ni kali hivyo?” Hapo Arioko akamsimulia Danieli kisa chote. Ndipo Danieli alipomwendea mfalme na kumwomba ampe muda ili aweze kumjulisha mfalme maana ya ndoto yake. Kisha, Danieli akarudi nyumbani, akawajulisha wenzake Hanania, Mishaeli na Azaria jambo hilo. Aliwaambia wamwombe Mungu wa mbinguni awaonee huruma kuhusu fumbo hilo, ili wao wasiangamie pamoja na wenye hekima wengine wa Babuloni. Ndipo Danieli alipofunuliwa fumbo hilo usiku katika maono. Naye Danieli akamshukuru Mungu wa mbinguni, akasema, “Na litukuzwe milele na milele jina lake Mungu. Hekima na nguvu ni vyake. Hubadilisha nyakati na majira, huwaondoa na kuwatawaza wafalme. Wenye busara huwapa hekima, wenye maarifa huwaongezea ufahamu. Hufunua siri na mafumbo, ajua kilichoko gizani, mwanga wakaa kwake. Kwako, ee Mungu wa wazee wangu, natoa shukrani na kukusifu, maana umenipa hekima na nguvu, umetujulisha kile tulichokuomba, umetujulisha kile kisa cha mfalme.” Basi, Danieli akamwendea Arioko aliyekuwa ameteuliwa kuwaangamiza wenye hekima wa Babuloni, akamwambia, “Usiwaue wenye hekima wa Babuloni, ila nipeleke mimi mbele ya mfalme, nami nitamweleza maana ya ndoto yake.” Basi, Arioko akampeleka Danieli mbele ya mfalme kwa haraka na kumwambia, “Nimempata mtu fulani miongoni mwa mateka wa Yuda anayeweza kukufasiria ndoto yako, ee mfalme.” Mfalme akamwuliza Danieli, ambaye pia aliitwa Belteshaza, “Je, unaweza kunijulisha ndoto niliyoota na maana yake?” Danieli akamjibu mfalme, “Hakuna wenye hekima, wachawi, waganga wala wanajimu wanaoweza kukujulisha fumbo hilo lako. Lakini, yuko Mungu mbinguni ambaye hufumbua mafumbo, naye amekujulisha, ee mfalme Nebukadneza, mambo yatakayotukia siku zijazo. Ndoto yako na maono yaliyokujia kichwani mwako ulipokuwa umelala ni haya

Shirikisha
Soma Danieli 2

Danieli 2:1-28 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Hata katika mwaka wa pili wa kumiliki kwake Nebukadneza, Nebukadneza aliota ndoto; na roho yake ikafadhaika, akatokwa na usingizi. Ndipo mfalme akatoa amri kuwaita waganga, na wachawi, na walozi, na Wakaldayo, wapate kumweleza mfalme ndoto zake. Basi wakaingia, wakasimama mbele ya mfalme. Mfalme akawaambia, Nimeota ndoto, na roho yangu imefadhaika hata niijue tafsiri yake. Ndipo hao Wakaldayo wakamwambia mfalme, kwa lugha ya Kiaramu, Ee Mfalme, uishi milele; tuambie sisi watumishi wako ile ndoto, nasi tutakuonesha tafsiri yake. Mfalme akajibu, akawaambia Wakaldayo, Neno lenyewe limeniondoka; msiponijulisha ile ndoto na tafsiri yake, mtakatwa vipande vipande, na nyumba zenu zitafanywa jaa. Bali kama mkinionesha ile ndoto na tafsiri yake, nitawapa zawadi na thawabu na heshima nyingi; basi nionesheni ile ndoto na tafsiri yake. Wakajibu mara ya pili, wakasema, Mfalme na atuambie sisi watumishi wake ile ndoto, nasi tutamwonesha tafsiri yake. Mfalme akajibu, akasema, Najua hakika ya kuwa mnataka kupata nafasi, kwa sababu mmeona ya kuwa lile neno lenyewe limeniondoka. Lakini msiponijulisha ile ndoto, iko amri moja tu iwapasayo; maana mmepatana kusema maneno ya uongo, na maneno maovu, mbele yangu, hata zamani zitakapobadilika; basi niambieni ile ndoto, nami nitajua ya kuwa mwaweza kunionesha tafsiri yake. Wakaldayo wakajibu mbele ya mfalme, wakasema, Hapana mtu duniani awezaye kulionesha neno hili la mfalme; kwa maana hapana mfalme, wala bwana, wala mtawala, aliyetaka neno kama hili kwa mganga, wala kwa mchawi, wala kwa Mkaldayo. Ni neno la ajabu, hili analolitaka mfalme, wala hapana mwingine awezaye kumwonesha mfalme neno hilo, ila miungu, wasio na kikao pamoja na wenye mwili. Basi kwa hiyo mfalme akaghadhibika sana, akaona hasira nyingi, akatoa amri kuwaangamiza wenye hekima wote wa Babeli. Basi ile amri ikatangazwa, na hao wenye hekima walikuwa karibu na kuuawa; watu wakamtafuta Danieli na wenzake ili wauawe. Ndipo Danieli kwa busara na hadhari akamjibu Arioko, mkuu wa walinzi wa mfalme, aliyekuwa ametoka ili kuwaua wenye hekima wa Babeli; alijibu, akamwambia Arioko, mkuu wa walinzi wa mfalme, Mbona amri hii ya mfalme ina ukali namna hii? Ndipo Arioko akamwarifu Danieli habari ile. Basi Danieli akaingia, akamwomba mfalme ampe muda, kisha yeye atamwonesha mfalme tafsiri ile. Ndipo Danieli akaenda nyumbani kwake, akawapasha habari kina Hanania, na Mishaeli, na Azaria wenzake; ili waombe rehema kwa Mungu wa mbinguni kuhusu siri hiyo, ili kwamba Danieli na wenzake wasiangamizwe pamoja na wenye hekima wa Babeli. Ndipo Danieli alipofunuliwa siri hiyo katika njozi ya usiku. Basi Danieli akamhimidi Mungu wa mbinguni. Danieli akajibu, akasema, Na lihimidiwe jina la Mungu milele na milele; kwa kuwa hekima na uweza ni wake. Yeye hubadili majira na nyakati; hutengua na kuteua wafalme; huwapa hekima wenye hekima; huwapa wenye ufahamu maarifa; yeye hufunua mambo ya fumbo na ya siri; huyajua yaliyo gizani, na nuru hukaa kwake. Nakushukuru, nakuhimidi, Ee Mungu wa baba zangu, uliyenipa hekima na uwezo, ukanijulisha hayo tuliyotaka kwako; maana umetujulisha neno lile la mfalme. Basi Danieli akaenda kwa Arioko, aliyewekwa na mfalme kuwaangamiza wenye hekima wa Babeli; alikwenda akamwambia hivi, Usiwaangamize wenye hekima wa Babeli; niingize mimi mbele ya mfalme, nami nitamwonesha mfalme ile tafsiri. Ndipo Arioko akamwingiza Danieli mbele ya mfalme kwa haraka, akamwambia hivi, Nimemwona mtu wa hao wana wa Yuda waliohamishwa, atakayemjulisha mfalme ile tafsiri. Mfalme akajibu, akamwambia Danieli, aliyekuwa akiitwa Belteshaza, Je! Waweza kunijulisha ile ndoto niliyoiona, na tafsiri yake? Danieli akajibu mbele ya mfalme, akasema, Ile siri aliyoiuliza mfalme, wenye hekima hawawezi kumfunulia mfalme; wala wachawi, wala waganga, wala wanajimu; lakini yuko Mungu mbinguni afunuaye siri, naye amemjulisha mfalme Nebukadneza mambo yatakayokuwa siku za mwisho. Ndoto yako, na njozi za kichwa chako ulizoziona kitandani pako, ni hizi

Shirikisha
Soma Danieli 2

Danieli 2:1-28 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Hata katika mwaka wa pili wa kumiliki kwake Nebukadreza, Nebukadreza aliota ndoto; na roho yake ikafadhaika, usingizi wake ukamwacha. Ndipo mfalme akatoa amri kuwaita waganga, na wachawi, na wasihiri, na Wakaldayo, wapate kumweleza mfalme ndoto zake. Basi wakaingia, wakasimama mbele ya mfalme. Mfalme akawaambia, Nimeota ndoto, na roho yangu imefadhaika hata niijue tafsiri yake. Ndipo hao Wakaldayo wakamwambia mfalme, kwa lugha ya Kiaramu, Ee Mfalme, uishi milele; tuambie sisi watumishi wako ile ndoto, nasi tutakuonyesha tafsiri yake. Mfalme akajibu, akawaambia Wakaldayo, Neno lenyewe limeniondoka; msiponijulisha ile ndoto na tafsiri yake, mtakatwa vipande vipande, na nyumba zenu zitafanywa jaa. Bali kama mkinionyesha ile ndoto na tafsiri yake, nitawapa zawadi na thawabu na heshima nyingi; basi nionyesheni ile ndoto na tafsiri yake. Wakajibu mara ya pili, wakasema, Mfalme na atuambie sisi watumishi wake ile ndoto, nasi tutamwonyesha tafsiri yake. Mfalme akajibu, akasema, Najua hakika ya kuwa mnataka kupata nafasi, kwa sababu mmeona ya kuwa lile neno lenyewe limeniondoka. Lakini msiponijulisha ile ndoto, iko amri moja tu iwapasayo; maana mmepatana kusema maneno ya uongo, na maneno maovu, mbele yangu, hata zamani zitakapobadilika; basi niambieni ile ndoto, nami nitajua ya kuwa mwaweza kunionyesha tafsiri yake. Wakaldayo wakajibu mbele ya mfalme, wakasema, Hapana mtu duniani awezaye kulionyesha neno hili la mfalme; kwa maana hapana mfalme, wala bwana, wala liwali, aliyetaka neno kama hili kwa mganga, wala kwa mchawi, wala kwa Mkaldayo. Ni neno la ajabu, hili analolitaka mfalme, wala hapana mwingine awezaye kumwonyesha mfalme neno hilo, ila miungu, wasio na kikao pamoja na wenye mwili. Basi kwa hiyo mfalme akaghadhibika sana, akaona hasira nyingi, akatoa amri kuwaangamiza wenye hekima wote wa Babeli. Basi ile amri ikatangazwa, na hao wenye hekima walikuwa karibu na kuuawa; watu wakamtafuta Danieli na wenzake ili wauawe. Ndipo Danieli kwa busara na hadhari akamjibu Arioko, akida wa walinzi wa mfalme, aliyekuwa ametoka ili kuwaua wenye hekima wa Babeli; alijibu, akamwambia Arioko, akida wa walinzi wa mfalme, Mbona amri hii ya mfalme ina ukali namna hii? Ndipo Arioko akamwarifu Danieli habari ile. Basi Danieli akaingia, akamwomba mfalme ampe muda, kisha yeye atamwonyesha mfalme tafsiri ile. Ndipo Danieli akaenda nyumbani kwake, akawapasha habari kina Hanania, na Mishaeli, na Azaria wenzake; ili waombe rehema kwa Mungu wa mbinguni kwa habari ya siri hiyo, ili kwamba Danieli na wenzake wasiangamizwe pamoja na wenye hekima wa Babeli. Ndipo Danieli alipofunuliwa siri hiyo katika njozi ya usiku. Basi Danieli akamhimidi Mungu wa mbinguni. Danieli akajibu, akasema, Na lihimidiwe jina la Mungu milele na milele; kwa kuwa hekima na uweza ni wake. Yeye hubadili majira na nyakati; huuzulu wafalme na kuwamilikisha wafalme; huwapa hekima wenye hekima; huwapa wenye ufahamu maarifa; yeye hufunua mambo ya fumbo na ya siri; huyajua yaliyo gizani, na nuru hukaa kwake. Nakushukuru, nakuhimidi, Ee Mungu wa baba zangu, uliyenipa hekima na uwezo, ukanijulisha hayo tuliyotaka kwako; maana umetujulisha neno lile la mfalme. Basi Danieli akaenda kwa Arioko, aliyewekwa na mfalme kuwaangamiza wenye hekima wa Babeli; alikwenda akamwambia hivi, Usiwaangamize wenye hekima wa Babeli; niingize mimi mbele ya mfalme, nami nitamwonyesha mfalme ile tafsiri. Ndipo Arioko akamwingiza Danieli mbele ya mfalme kwa haraka, akamwambia hivi, Nimemwona mtu wa hao wana wa Yuda waliohamishwa, atakayemjulisha mfalme ile tafsiri. Mfalme akajibu, akamwambia Danieli, aliyekuwa akiitwa Belteshaza, Je! Waweza kunijulisha ile ndoto niliyoiona, na tafsiri yake. Danieli akajibu mbele ya mfalme, akasema, Ile siri aliyoiuliza mfalme, wenye hekima hawawezi kumfunulia mfalme; wala wachawi, wala waganga, wala wanajimu; lakini yuko Mungu mbinguni afunuaye siri, naye amemjulisha mfalme Nebukadreza mambo yatakayokuwa siku za mwisho. Ndoto yako, na njozi za kichwa chako ulizoziona kitandani pako, ni hizi

Shirikisha
Soma Danieli 2

Danieli 2:1-28 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Katika mwaka wa pili wa utawala wake, Nebukadneza aliota ndoto. Mawazo yake yakasumbuka na hakuweza kulala. Hivyo mfalme akawaita waganga, wasihiri, wachawi na wanajimu ili wamwambie ndoto yake aliyokuwa ameota. Walipoingia ndani na kusimama mbele ya mfalme, akawaambia, “Niliota ndoto inayonisumbua, nami nataka nijue maana yake.” Ndipo wanajimu wakamjibu mfalme kwa lugha ya Kiaramu, “Ee mfalme, uishi milele! Waambie watumishi wako hiyo ndoto, nasi tutaifasiri.” Mfalme akawajibu wanajimu, “Nimeamua hivi kwa uthabiti: Ikiwa hamtaniambia ndoto yangu ilikuwa ipi na kuifasiri, mtakatwa vipande vipande na nyumba zenu zitafanywa kuwa vifusi. Lakini mkiniambia ndoto yangu na kuielezea, mtapokea kwangu zawadi, tuzo na heshima kubwa. Basi niambieni ndoto yangu na mnifasirie.” Wakajibu kwa mara nyingine, “Mfalme na awaambie watumishi wake ndoto yake, nasi tutaifasiri.” Ndipo mfalme akajibu, “Nina hakika kuwa mnajaribu kupata muda zaidi, kwa sababu mnatambua kuwa nimeamua hivi kwa uthabiti: Ikiwa hamtaniambia ndoto yangu, ipo adhabu moja tu kwenu. Mmefanya shauri kuniambia habari za kunipotosha na mambo maovu, mkitumaini kwamba hali itabadilika. Hivyo basi, niambieni hiyo ndoto, nami nitajua kuwa mwaweza kunifasiria.” Wanajimu wakamjibu mfalme, “Hakuna mtu duniani ambaye anaweza kufanya analotaka mfalme! Vilevile hakuna mfalme hata awe mkuu na mwenye uweza namna gani, aliyeuliza kitu kama hicho kwa mganga au kwa msihiri, wala kwa mnajimu yeyote. Anachouliza mfalme ni kigumu mno. Hakuna yeyote awezaye kumfunulia mfalme isipokuwa miungu, nao hawaishi miongoni mwa wanadamu.” Jambo hili lilimkasirisha na kumghadhibisha mfalme mno hata kuagiza kuuawa kwa wenye hekima wote wa Babeli. Hivyo amri ikatolewa ya kuwaua wenye hekima, nao watu wakatumwa kuwatafuta Danieli na rafiki zake ili wawaue. Wakati Arioko, mkuu wa askari wa walinzi wa mfalme, alikuwa amekwenda kuwaua watu wenye hekima wa Babeli, Danieli akazungumza naye kwa hekima na busara. Akamuuliza huyo afisa wa mfalme, “Kwa nini mfalme ametoa amri kali hivyo?” Ndipo Arioko akamweleza Danieli jambo hilo. Aliposikia jambo hili, Danieli akamwendea mfalme, akamwomba ampe muda ili aweze kumfasiria ile ndoto. Ndipo Danieli akarudi nyumbani kwake na kuwaeleza rafiki zake Hanania, Mishaeli na Azaria jambo hilo. Aliwasihi waombe rehema kutoka kwa Mungu wa mbinguni kuhusu siri hii, ili yeye na rafiki zake wasije wakauawa pamoja na wenye hekima wengine wa Babeli. Wakati wa usiku lile fumbo lilifunuliwa kwa Danieli katika maono. Ndipo Danieli akamhimidi Mungu wa mbinguni, na akasema: “Lihimidiwe jina la Mungu milele na milele; hekima na uweza ni vyake. Yeye hubadili nyakati na majira; huwaweka wafalme na kuwaondoa. Huwapa hekima wenye hekima, na maarifa wenye ufahamu. Hufunua siri na mambo yaliyofichika; anajua yale yaliyo gizani, nayo nuru hukaa kwake. Ninakushukuru na kukuhimidi, Ee Mungu wa baba zangu: Umenipa hekima na uwezo, umenijulisha kile tulichokuomba, umetujulisha ndoto ya mfalme.” Ndipo Danieli akamwendea Arioko, ambaye mfalme alikuwa amemteua kuwaua wenye hekima wa Babeli, akamwambia, “Usiwaue wenye hekima wa Babeli. Nipeleke kwa mfalme, nami nitamfasiria ndoto yake.” Arioko akampeleka Danieli kwa mfalme mara moja na kumwambia, “Nimempata mtu miongoni mwa watu wa uhamisho kutoka Yuda ambaye anaweza kumwambia mfalme maana ya ndoto yake.” Mfalme akamuuliza Danieli (aliyeitwa pia Belteshaza), “Je, unaweza kuniambia nilichoona katika ndoto yangu na kuifasiri?” Danieli akajibu, “Hakuna mwenye hekima, msihiri, mganga au mwaguzi anayeweza kumweleza mfalme siri aliyouliza, lakini yuko Mungu mbinguni afunuaye siri. Amemwonyesha Mfalme Nebukadneza kitakachotokea siku zijazo. Ndoto yako na maono yaliyopita mawazoni mwako ulipokuwa umelala kitandani mwako ni haya

Shirikisha
Soma Danieli 2