Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Danieli 2

2
Ndoto ya Nebukadneza
1 # Mwa 41:8; Est 6:1 Hata katika mwaka wa pili wa kumiliki kwake Nebukadneza, Nebukadneza aliota ndoto; na roho yake ikafadhaika, akatokwa na usingizi. 2#Kut 7:11 Ndipo mfalme akatoa amri kuwaita waganga, na wachawi, na walozi, na Wakaldayo, wapate kumweleza mfalme ndoto zake. Basi wakaingia, wakasimama mbele ya mfalme. 3Mfalme akawaambia, Nimeota ndoto, na roho yangu imefadhaika hata niijue tafsiri yake. 4Ndipo hao Wakaldayo wakamwambia mfalme, kwa lugha ya Kiaramu, Ee Mfalme, uishi milele; tuambie sisi watumishi wako ile ndoto, nasi tutakuonesha tafsiri yake. 5Mfalme akajibu, akawaambia Wakaldayo, Neno lenyewe limeniondoka; msiponijulisha ile ndoto na tafsiri yake, mtakatwa vipande vipande, na nyumba zenu zitafanywa jaa. 6Bali kama mkinionesha ile ndoto na tafsiri yake, nitawapa zawadi na thawabu na heshima nyingi; basi nionesheni ile ndoto na tafsiri yake. 7Wakajibu mara ya pili, wakasema, Mfalme na atuambie sisi watumishi wake ile ndoto, nasi tutamwonesha tafsiri yake. 8Mfalme akajibu, akasema, Najua hakika ya kuwa mnataka kupata nafasi, kwa sababu mmeona ya kuwa lile neno lenyewe limeniondoka. 9#Est 4:11 Lakini msiponijulisha ile ndoto, iko amri moja tu iwapasayo; maana mmepatana kusema maneno ya uongo, na maneno maovu, mbele yangu, hata zamani zitakapobadilika; basi niambieni ile ndoto, nami nitajua ya kuwa mwaweza kunionesha tafsiri yake. 10Wakaldayo wakajibu mbele ya mfalme, wakasema, Hapana mtu duniani awezaye kulionesha neno hili la mfalme; kwa maana hapana mfalme, wala bwana, wala mtawala, aliyetaka neno kama hili kwa mganga, wala kwa mchawi, wala kwa Mkaldayo. 11#Kut 8:10; Dan 5:11; Mt 19:26 Ni neno la ajabu, hili analolitaka mfalme, wala hapana mwingine awezaye kumwonesha mfalme neno hilo, ila miungu, wasio na kikao pamoja na wenye mwili. 12#Zab 76:10; 94:20; Mit 16:14; 19:12; 20:2; 28:15; Mt 2:16 Basi kwa hiyo mfalme akaghadhibika sana, akaona hasira nyingi, akatoa amri kuwaangamiza wenye hekima wote wa Babeli. 13Basi ile amri ikatangazwa, na hao wenye hekima walikuwa karibu na kuuawa; watu wakamtafuta Danieli na wenzake ili wauawe. 14Ndipo Danieli kwa busara na hadhari akamjibu Arioko, mkuu wa walinzi wa mfalme, aliyekuwa ametoka ili kuwaua wenye hekima wa Babeli; 15alijibu, akamwambia Arioko, mkuu wa walinzi wa mfalme, Mbona amri hii ya mfalme ina ukali namna hii? Ndipo Arioko akamwarifu Danieli habari ile. 16Basi Danieli akaingia, akamwomba mfalme ampe muda, kisha yeye atamwonesha mfalme tafsiri ile.
Mungu afumbua ndoto ya mfalme Nebukadneza
17Ndipo Danieli akaenda nyumbani kwake, akawapasha habari kina Hanania, na Mishaeli, na Azaria wenzake; 18ili waombe rehema kwa Mungu wa mbinguni kuhusu siri hiyo, ili kwamba Danieli na wenzake wasiangamizwe pamoja na wenye hekima wa Babeli. 19#Hes 12:6; Ayu 33:15,16 Ndipo Danieli alipofunuliwa siri hiyo katika njozi ya usiku. Basi Danieli akamhimidi Mungu wa mbinguni. 20#Zab 113:2; 147:5; Ayu 12:13; Yer 32:19; Mt 6:13 Danieli akajibu, akasema, Na lihimidiwe jina la Mungu milele na milele; kwa kuwa hekima na uweza ni wake. 21#1 Nya 29:30; Est 1:13; Dan 7:25; 4:17; Ayu 12:18; Zab 75:6,7; Yer 27:5; Yak 1:5 Yeye hubadili majira na nyakati; hutengua na kuteua wafalme; huwapa hekima wenye hekima; huwapa wenye ufahamu maarifa; 22#Ayu 12:22; Ebr 4:13; Zab 25:14; 139:11,12; Dan 5:11 yeye hufunua mambo ya fumbo na ya siri; huyajua yaliyo gizani, na nuru hukaa kwake. 23#Amo 3:7 Nakushukuru, nakuhimidi, Ee Mungu wa baba zangu, uliyenipa hekima na uwezo, ukanijulisha hayo tuliyotaka kwako; maana umetujulisha neno lile la mfalme.
Danieli afasiri ndoto
24Basi Danieli akaenda kwa Arioko, aliyewekwa na mfalme kuwaangamiza wenye hekima wa Babeli; alikwenda akamwambia hivi, Usiwaangamize wenye hekima wa Babeli; niingize mimi mbele ya mfalme, nami nitamwonesha mfalme ile tafsiri.
25Ndipo Arioko akamwingiza Danieli mbele ya mfalme kwa haraka, akamwambia hivi, Nimemwona mtu wa hao wana wa Yuda waliohamishwa, atakayemjulisha mfalme ile tafsiri. 26Mfalme akajibu, akamwambia Danieli, aliyekuwa akiitwa Belteshaza, Je! Waweza kunijulisha ile ndoto niliyoiona, na tafsiri yake? 27Danieli akajibu mbele ya mfalme, akasema, Ile siri aliyoiuliza mfalme, wenye hekima hawawezi kumfunulia mfalme; wala wachawi, wala waganga, wala wanajimu; 28#Mwa 40:8; Zab 115:2,3; Amo 4:13 lakini yuko Mungu mbinguni afunuaye siri, naye amemjulisha mfalme Nebukadneza mambo yatakayokuwa siku za mwisho.
Ndoto yako, na njozi za kichwa chako ulizoziona kitandani pako, ni hizi; 29Wewe, Ee mfalme, mawazo yako yaliingia moyoni mwako kitandani pako ya mambo yatakayokuwa halafu; na yeye afunuaye siri amekujulisha mambo yatakayokuwa. 30#Mwa 41:16; Mdo 3:12 Lakini mimi, sikufunuliwa siri hii kwa sababu ya hekima iwayo yote niliyo nayo zaidi ya watu wengine walio hai, bali kusudi mfalme afunuliwe ile tafsiri, nawe upate kujua mawazo ya moyo wako. 31Wewe, Ee Mfalme, uliona, na tazama, sanamu kubwa sana. Sanamu hii, iliyokuwa kubwa sana, na mwangaza wake mwingi sana, ilisimama mbele yako; na umbo lake lilikuwa la kutisha. 32Na sanamu hii kichwa chake kilikuwa ni cha dhahabu safi; kifua chake na mikono yake ni ya fedha; tumbo lake na viuno vyake ni vya shaba; 33miguu yake ni ya chuma; na nyayo za miguu yake nusu ya chuma na nusu ya udongo. 34Nawe ukatazama hata jiwe likachongwa bila kazi ya mikono, nalo jiwe hilo likaipiga sanamu miguu yake, iliyokuwa ya chuma na udongo, likaivunja vipande vipande. 35#Isa 2:2,3; Mik 4:1,2; Zab 22:27; 67:1,2; Isa 11:9; Zek 14:8,9; Ufu 11:15 Ndipo kile chuma, na ule udongo, na ile shaba, na ile fedha, na ile dhahabu, vilivunjwa vipande vipande pamoja vikawa kama makapi ya viwanja vya kupepetea wakati wa joto; upepo ukavipeperusha hata pasionekane mahali pake; na lile jiwe lililoipiga hiyo sanamu likawa milima mikubwa, likaijaza dunia yote.
36Hii ndiyo ile ndoto, nasi tutaihubiri tafsiri yake mbele ya mfalme. 37#Ezr 7:12; 1:2; Isa 47:5 Wewe, Ee mfalme, u mfalme wa wafalme, na Mungu wa mbinguni amekupa ufalme, na uwezo, na nguvu, na utukufu; 38#Dan 4:21; Yer 27:6 na kila mahali wakaapo wanadamu, wanyama wa kondeni na ndege wa angani amewatia mkononi mwako, naye amekumilikisha juu ya hao wote; wewe u kichwa kile cha dhahabu. 39#Dan 5:28 Na baada yako utainuka ufalme mwingine mdogo kuliko wewe; na ufalme mwingine wa tatu wa shaba, utakaoitawala dunia yote. 40#Dan 7:7,23; Yn 11:48 Na ufalme wa nne utakuwa na nguvu mfano wa chuma; kwa maana chuma huvunja vitu vyote na kuviponda; na kama chuma kipondavyo vitu hivi vyote, ndivyo utakavyovunjavunja na kuponda. 41Na kama vile ulivyoziona hizo nyayo za miguu na vidole vyake, kuwa nusu udongo wa mfinyanzi, na nusu chuma, ufalme ule utakuwa ufalme uliogawanyika; lakini ndani yake zitakuwako nguvu za chuma, kama vile ulivyoona kile chuma kimechanganyika na udongo wa matope. 42Na kama vidole vya zile nyayo vilikuwa nusu chuma na nusu udongo, kadhalika ufalme ule utakuwa nusu yake una nguvu, na nusu yake umevunjika. 43Na kama vile ulivyokiona kile chuma kimechanganyika na udongo wa matope, watajichanganya nafsi zao kwa mbegu za wanadamu; lakini hawatashikamana, kama vile chuma kisivyoshikamana na udongo. 44#Mwa 49:10; Zab 2:6,9; Dan 4:3,34; Mik 4:7; Lk 1:32; Isa 60:12; 1 Kor 15:24,25 Na katika siku za wafalme hao Mungu wa mbinguni atausimamisha ufalme ambao hautaangamizwa milele, wala watu wengine hawataachiwa enzi yake; bali utavunja falme hizi zote vipande vipande na kuziharibu, nao utasimama milele na milele. 45#Isa 28:16 Na kama vile ulivyoona ya kuwa jiwe lilichongwa mlimani bila kazi ya mikono, na ya kuwa lilivunjavunja kile chuma, na ile shaba na ule udongo, na ile fedha, na ile dhahabu; basi Mungu aliye mkuu amemjulisha mfalme mambo yatakayokuwa baadaye; na ndoto hii ni ya hakika, na tafsiri yake ni thabiti.
Danieli na wenzake wapewa nyadhifa
46 # Mdo 10:25; 14:13; Ufu 19:10; Ezr 6:10 Ndipo Nebukadneza, mfalme, akaanguka kifudifudi, akamsujudia Danieli, akatoa amri wamtolee Danieli sadaka na uvumba. 47Mfalme akajibu, akamwambia Danieli, Hakika Mungu wenu ndiye Mungu wa miungu, na Bwana wa wafalme, awezaye kufumbua siri, kwa kuwa wewe uliweza kuifumbua siri hii. 48#Mwa 41:40; Dan 4:9 Basi mfalme akamtukuza Danieli, akampa zawadi kubwa nyingi sana, akamfanya kuwa mkubwa juu ya utawala wote wa Babeli, na kuwa mtawala mkuu juu ya wote wenye hekima wa Babeli. 49#Mit 28:12; Dan 1:17; Est 2:19; Yer 39:3; Amo 5:15 Tena, Danieli akamwomba mfalme, naye akawaweka Shadraka, na Meshaki, na Abednego, wawe juu ya mambo yote ya utawala wa Babeli; lakini huyo Danieli alikuwa akikaa katika lango la mfalme.

Iliyochaguliwa sasa

Danieli 2: SRUV

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia