Wakolosai 4:12-18
Wakolosai 4:12-18 Biblia Habari Njema (BHN)
Epafra, mwananchi mwenzenu na mtumishi wa Kristo Yesu, anawasalimuni. Daima anawaombeeni nyinyi kwa bidii ili mpate kusimama imara, mkomae na kuwa thabiti kabisa katika mambo yote anayotaka Mungu. Naweza kushuhudia kwamba anafanya kazi kwa bidii kwa ajili yenu na kwa ajili ya watu wa Laodikea na Hierapoli. Luka, daktari wetu mpenzi, na Dema, wanawasalimuni. Salamu zetu kwa ndugu wa Laodikea. Msalimuni dada Nimfa pamoja na jumuiya yote ya waumini inayokutana nyumbani kwake. Mkisha soma barua hii, hakikisheni kwamba inasomwa na Wakristo wa Laodikea; na nyinyi fanyeni mpango mpate kuisoma barua waliyoipata wao. Mwambieni Arkipo aitekeleze vizuri ile huduma aliyokabidhiwa na Bwana. Naandika haya kwa mkono wangu mwenyewe: Salamu kutoka kwangu, mimi Paulo. Kumbukeni kwamba niko kifungoni. Neema ya Mungu iwe nanyi.
Wakolosai 4:12-18 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Epafra, aliye mtu wa kwenu, mtumwa wa Yesu Kristo, awasalimu, akifanya bidii siku zote kwa ajili yenu katika maombi yake, ili msimame mkiwa wakamilifu na kuthibitika kabisa katika mapenzi yote ya Mungu. Maana namshuhudia kwamba ana juhudi nyingi kwa ajili yenu, na kwa ajili ya hao walioko Laodikia, na kwa ajili ya hao walioko Hierapoli. Luka, yule tabibu mpendwa, na Dema, wanawasalimu. Wasalimuni ndugu walioko Laodikia, na Nimfa, na kanisa lililo katika nyumba yake. Waraka huu ukiisha kusomwa kwenu hakikisheni kwamba unasomwa katika kanisa la Walaodikia pia; na ule wa Laodikia usomwe na ninyi. Mwambieni Arkipo, Iangalie sana huduma ile uliyopewa katika Bwana, ili uitimize. Naandika salamu yangu mimi Paulo, kwa mkono wangu mwenyewe. Kumbukeni kufungwa kwangu. Neema na iwe pamoja nanyi.
Wakolosai 4:12-18 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Epafra, aliye mtu wa kwenu, mtumwa wa Yesu Kristo, awasalimu, akifanya bidii siku zote kwa ajili yenu katika maombi yake, ili kwamba msimame wakamilifu na kuthibitika sana katika mapenzi yote ya Mungu. Maana namshuhudia kwamba ana juhudi nyingi kwa ajili yenu, na kwa ajili ya hao walioko Laodikia, na kwa ajili ya hao walioko Hierapoli. Luka, yule tabibu mpendwa, na Dema, wanawasalimu. Wasalimuni ndugu walioko Laodikia, na Nimfa, na kanisa lililo katika nyumba yake. Waraka huu ukiisha kusomwa kwenu fanyeni kwamba usomwe katika kanisa la Walaodikia pia; na ule wa Laodikia usomwe na ninyi. Mwambieni Arkipo, Iangalie sana huduma ile uliyopewa katika Bwana, ili uitimize. Salamu yangu mimi Paulo, kwa mkono wangu mwenyewe. Kumbukeni kufungwa kwangu. Neema na iwe pamoja nanyi.
Wakolosai 4:12-18 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)
Epafra, ambaye ni mmoja wenu na mtumishi wa Al-Masihi Isa, anawasalimu. Yeye siku zote anawaombea kwa bidii kwamba msimame imara katika mapenzi yote ya Mungu, mkiwa wakamilifu na thabiti. Ninashuhudia kumhusu kwamba anafanya kazi kwa bidii kwa ajili yenu, na kwa ajili ya ndugu wa Laodikia na wale wa Hierapoli. Rafiki yetu mpendwa, Luka yule tabibu, pamoja na Dema, wanawasalimu. Wasalimuni ndugu wote wa Laodikia, na pia Nimfa, pamoja na kundi la waumini wanaokutana katika nyumba yake. Baada ya barua hii kusomwa kwenu, hakikisheni kwamba inasomwa pia katika kundi la waumini wa Walaodikia. Nanyi pia msome barua inayotoka Laodikia. Mwambieni Arkipo hivi: “Hakikisha kuwa unakamilisha ile huduma uliyopokea katika Bwana Isa.” Mimi Paulo naandika salamu hizi kwa mkono wangu mwenyewe. Kumbukeni minyororo yangu. Neema iwe nanyi.