Matendo 28:11-22
Matendo 28:11-22 Biblia Habari Njema (BHN)
Baada ya miezi mitatu tulianza tena safari yetu kwa meli moja ya Aleksandria iitwayo “Miungu Pacha”. Meli hiyo ilikuwa imetia nanga kisiwani wakati wote wa baridi. Tulifika katika mji wa Sirakusa, tukakaa hapo kwa siku tatu. Toka huko tulingoa nanga, tukazunguka na kufika Regio. Baada ya siku moja, upepo ulianza kuvuma kutoka kusini, na baada ya siku mbili tulifika bandari ya Potioli. Huko tuliwakuta ndugu kadhaa ambao walituomba tukae nao kwa juma moja. Hivi ndivyo tulivyopata kufika Roma. Ndugu wa kule Roma walipopata habari zetu, wakaja kutulaki kwenye soko la Apio na Mikahawa Mitatu. Paulo alipowaona alimshukuru Mungu, akapata moyo. Tulipofika Roma, Paulo aliruhusiwa kukaa peke yake pamoja na askari mmoja wa kumlinda. Baada ya siku tatu, Paulo aliwaita pamoja viongozi wa Kiyahudi wa mahali hapo. Walipokusanyika, Paulo aliwaambia, “Wananchi wenzangu, mimi, ingawa sikufanya chochote kibaya wala kupinga desturi za wazee wetu, nilitiwa nguvuni kule Yerusalemu na kutiwa mikononi mwa Waroma. Waliponihoji na kuona kwamba sikuwa na hatia yoyote, walitaka kuniachia. Lakini Wayahudi wengine walipinga jambo hilo, nami nikalazimika kukata rufani kwa Kaisari, ingawa sikuwa na chochote cha kuwashtaki wananchi wenzangu. Ni kwa sababu hiyo nimeomba kuonana na kuongea nanyi, maana nimefungwa minyororo hii kwa sababu ya tumaini lile la Israeli.” Wao wakamwambia, “Sisi hatujapokea barua yoyote kutoka Yudea, wala hakuna ndugu yeyote aliyefika hapa na kutoa habari rasmi au kusema chochote kibaya juu yako. Lakini tunafikiri inafaa tusikie kutoka kwako mwenyewe mambo yaliyo kichwani mwako. Kwa maana tujualo sisi kuhusu hicho kikundi ni kwamba kinapingwa kila mahali.”
Matendo 28:11-22 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Baada ya miezi mitatu tukasafiri katika merikebu ya Aleksandria iliyokuwa imekaa pale kisiwani wakati wa baridi; na alama yake ni Ndugu Pacha. Tukafika Sirakusa, tukakaa siku tatu. Kutoka huko tukazunguka tukafikia Regio; baada ya siku moja upepo wa kusi ukavuma, na siku ya pili tukawasili Puteoli. Huko tukakuta ndugu, wakatusihi tukae nao siku saba; na hivi ndivyo tulifika Rumi. Na kutoka huko ndugu, waliposikia habari zetu, wakaja kutulaki mpaka Soko la Apio na Mikahawa Mitatu. Paulo alipowaona alimshukuru Mungu, akachangamka. Tulipoingia Rumi Paulo alipewa ruhusa kukaa kwake mwenyewe pamoja na askari aliyemlinda. Ikawa baada ya siku tatu akawaita wakuu wa Wayahudi wakutane, na walipokutanika akawaambia, Ndugu zangu, ningawa sikufanya neno kinyume cha watu wetu wala neno lililopingamana na desturi za baba zetu, nilitiwa katika mikono ya Warumi, nikiwa nimefungwa, tokea Yerusalemu. Na hao walipokwisha kunihoji walitaka kunifungua, kwa maana hapakuwa na sababu yoyote kwangu ya kuuawa. Lakini Wayahudi walipotoa hoja juu ya shauri hili nilishurutishwa kutaka rufani kwa Kaisari. Si kwamba nilikuwa na neno la kuwashitaki watu wa taifa langu. Basi kwa ajili ya hayo, nimewaita mje kunitazama na kusema nami; kwa maana nimefungwa kwa mnyororo huu kwa ajili ya tumaini la Israeli. Wale wakamwambia, Sisi hatukupata nyaraka zenye habari zako kutoka Yudea, wala hapana ndugu hata mmoja aliyefika hapa na kutupasha habari, au kunena neno baya juu yako. Lakini tunataka kusikia kwako uonavyo wewe; kwa maana kuhusu madhehebu hiyo imejulikana kwetu kwamba inanenwa vibaya kila mahali.
Matendo 28:11-22 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Baada ya miezi mitatu tukasafiri katika merikebu ya Iskanderia iliyokuwa imekaa pale kisiwani wakati wa baridi; na alama yake ni Ndugu Pacha. Tukafika Sirakusa, tukakaa siku tatu. Kutoka huko tukazunguka tukafikia Regio; baada ya siku moja upepo wa kusi ukavuma, na siku ya pili tukawasili Puteoli. Huko tukakuta ndugu, wakatusihi tukae nao siku saba; na hivi tukafika Rumi. Na kutoka huko ndugu, waliposikia habari zetu, wakaja kutulaki mpaka Soko la Apio na Mikahawa Mitatu. Paulo alipowaona alimshukuru Mungu, akachangamka. Tulipoingia Rumi Paulo alipewa ruhusa kukaa kwake mwenyewe pamoja na askari aliyemlinda. Ikawa baada ya siku tatu akawaita wakuu wa Wayahudi wakutane, hata walipokutanika akawaambia, Ndugu zangu, ningawa sikufanya neno kinyume cha watu wetu wala neno lililopingamana na desturi za baba zetu, nalitiwa katika mikono ya Warumi, hali nimefungwa, tokea Yerusalemu. Na hao walipokwisha kuniuliza-uliza walitaka kunifungua, kwa maana hapakuwa na sababu yo yote kwangu ya kuuawa. Lakini Wayahudi walipotoa hoja juu ya shauri hili nalishurutishwa kutaka rufani kwa Kaisari. Si kwamba nalikuwa na neno la kuwashitaki watu wa taifa langu. Basi kwa ajili ya hayo, nimewaita mje kunitazama na kusema nami; kwa maana nimefungwa kwa mnyororo huu kwa ajili ya tumaini la Israeli. Wale wakamwambia, Sisi hatukupata nyaraka zenye habari zako kutoka Uyahudi, wala hapana ndugu hata mmoja aliyefika hapa na kutupasha habari, au kunena neno baya juu yako. Lakini tunataka kusikia kwako uonavyo wewe; kwa maana katika habari za madhehebu hiyo imejulikana kwetu kwamba inanenwa vibaya kila mahali.
Matendo 28:11-22 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Miezi mitatu baadaye tukaanza safari kwa meli iliyokuwa imetia nanga kwenye kisiwa hicho kwa ajili ya majira ya baridi. Hii ilikuwa meli ya Iskanderia yenye alama ya miungu pacha waitwao Kasta na Poluksi. Kituo chetu cha kwanza kilikuwa Sirakusa na tukakaa huko siku tatu. Kisha tukangʼoa nanga, tukafika Regio. Siku iliyofuata, upepo mkali wa kusi ukavuma, na siku ya pili yake tukafika Puteoli. Huko tukawakuta ndugu, nasi tukakaribishwa tukae nao kwa siku saba. Hivyo tukaendelea na safari mpaka Rumi. Ndugu wa huko Rumi waliposikia habari zetu, walikuja mpaka Soko la Apio na mahali paitwapo Mikahawa Mitatu kutulaki. Paulo alipowaona, alimshukuru Mungu akatiwa moyo. Tulipofika Rumi, Paulo aliruhusiwa kuishi peke yake akiwa na askari wa kumlinda. Siku tatu baadaye Paulo akawaita pamoja viongozi wa Kiyahudi. Walipokwisha kukusanyika akawaambia, “Ndugu zangu, ingawa sikufanya jambo lolote dhidi ya watu wetu au dhidi ya desturi za baba zetu, lakini nilikamatwa huko Yerusalemu nikakabidhiwa kwa Warumi. Wao walipokwisha kunihoji, wakataka kuniachia huru kwa sababu hawakuona kosa lolote nililolifanya linalostahili adhabu ya kifo. Lakini Wayahudi walipopinga uamuzi huo, nililazimika kukata rufaa kwa Kaisari, ingawa sikuwa na lalamiko lolote juu ya taifa langu. Basi hii ndiyo sababu nimewatumania, ili niseme nanyi. Kwa kuwa ni kwa ajili ya tumaini la Israeli nimefungwa kwa minyororo.” Wakamjibu, “Hatujapokea barua zozote kutoka Uyahudi zinazokuhusu, wala hapana ndugu yeyote aliyekuja hapa ambaye ametoa taarifa au kuzungumza jambo lolote baya juu yako. Lakini tungependa kusikia kutoka kwako unalofikiri kwa sababu tunajua kwamba kila mahali watu wanazungumza mabaya kuhusu jamii hii.”