Mdo 28:11-22
Mdo 28:11-22 SUV
Baada ya miezi mitatu tukasafiri katika merikebu ya Iskanderia iliyokuwa imekaa pale kisiwani wakati wa baridi; na alama yake ni Ndugu Pacha. Tukafika Sirakusa, tukakaa siku tatu. Kutoka huko tukazunguka tukafikia Regio; baada ya siku moja upepo wa kusi ukavuma, na siku ya pili tukawasili Puteoli. Huko tukakuta ndugu, wakatusihi tukae nao siku saba; na hivi tukafika Rumi. Na kutoka huko ndugu, waliposikia habari zetu, wakaja kutulaki mpaka Soko la Apio na Mikahawa Mitatu. Paulo alipowaona alimshukuru Mungu, akachangamka. Tulipoingia Rumi Paulo alipewa ruhusa kukaa kwake mwenyewe pamoja na askari aliyemlinda. Ikawa baada ya siku tatu akawaita wakuu wa Wayahudi wakutane, hata walipokutanika akawaambia, Ndugu zangu, ningawa sikufanya neno kinyume cha watu wetu wala neno lililopingamana na desturi za baba zetu, nalitiwa katika mikono ya Warumi, hali nimefungwa, tokea Yerusalemu. Na hao walipokwisha kuniuliza-uliza walitaka kunifungua, kwa maana hapakuwa na sababu yo yote kwangu ya kuuawa. Lakini Wayahudi walipotoa hoja juu ya shauri hili nalishurutishwa kutaka rufani kwa Kaisari. Si kwamba nalikuwa na neno la kuwashitaki watu wa taifa langu. Basi kwa ajili ya hayo, nimewaita mje kunitazama na kusema nami; kwa maana nimefungwa kwa mnyororo huu kwa ajili ya tumaini la Israeli. Wale wakamwambia, Sisi hatukupata nyaraka zenye habari zako kutoka Uyahudi, wala hapana ndugu hata mmoja aliyefika hapa na kutupasha habari, au kunena neno baya juu yako. Lakini tunataka kusikia kwako uonavyo wewe; kwa maana katika habari za madhehebu hiyo imejulikana kwetu kwamba inanenwa vibaya kila mahali.