2 Samueli 9:3-13
2 Samueli 9:3-13 Biblia Habari Njema (BHN)
Mfalme akamwuliza, “Je, hakuna mtu yeyote aliyesalia katika jamaa ya Shauli? Kama yuko, ningependa kumtendea wema wa Mungu.” Siba akamjibu, “Yuko mwana wa Yonathani, lakini yeye amelemaa miguu.” Mfalme akamwuliza, “Yuko wapi?” Siba akamjibu, “Yuko nyumbani kwa Makiri mwana wa Amieli huko Lo-debari.” Basi, mfalme Daudi akatuma watu, naye akaletwa kutoka nyumbani kwa Makiri mwana wa Amieli huko Lo-debari. Basi, Mefiboshethi mwana wa Yonathani, na mjukuu wa Shauli akaenda kwa mfalme Daudi, akaanguka kifudifudi mbele ya mfalme Daudi, akasujudu. Daudi akamwita, “Mefiboshethi.” Naye akamjibu, “Naam! Mimi hapa mtumishi wako.” Daudi akamwambia, “Usiogope. Mimi nitakutendea wema kwa ajili ya baba yako Yonathani. Ile ardhi yote iliyokuwa ya babu yako Shauli nitakurudishia. Nawe, daima utakula mezani pangu.” Mefiboshethi akasujudu, na kusema, “Mimi ni sawa na mbwa mfu; kwa nini unishughulikie hivyo?” Kisha, mfalme Daudi akamwita Siba mtumishi wa Shauli, akamwambia, “Ile mali yote iliyokuwa ya Shauli na jamaa yake nimempa mjukuu wa bwana wako. Wewe, watoto wako na watumishi wako mtakuwa mnamlimia Mefiboshethi na mtamletea mavuno ili mjukuu wa bwana wako awe daima na chakula. Lakini yeye atakula mezani pangu.” Wakati huo, Siba alikuwa na watoto wa kiume kumi na watano na watumishi ishirini. Kisha, Siba akamwambia mfalme, “Mimi mtumishi wako, nitafanya yote kulingana na amri yako.” Basi, Mefiboshethi akawa anapata chakula chake mezani pa Daudi, kama mmojawapo wa watoto wa mfalme. Mefiboshethi alikuwa na mtoto mdogo wa kiume aliyeitwa Mika. Watu wote wa jamaa ya Siba wakawa watumishi wa Mefiboshethi. Hivyo, Mefiboshethi aliyekuwa amelemaa miguu yake yote akawa anaishi mjini Yerusalemu, na kupata chakula chake mezani pa mfalme daima.
2 Samueli 9:3-13 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Mfalme akasema, Je! Hakuna hata sasa mtu yeyote wa nyumba ya Sauli, nipate kumtendea mema ya Mungu? Siba akamwambia mfalme, Yonathani anaye mwana hata sasa, aliye na kilema cha mguu. Mfalme akamwambia, Yuko wapi? Siba akamwambia mfalme, Tazama, yumo katika nyumba ya Makiri, mwana wa Amieli, katika Lo-debari. Basi mfalme Daudi akatuma watu, na kumwondoa katika nyumba ya Makiri, mwana wa Amieli, katika Lo-debari. Basi Mefiboshethi, mwana wa Yonathani, mwana wa Sauli akaenda kwa Daudi, akaanguka kifudifudi, akasujudu. Daudi akasema, Mefiboshethi! Naye akaitika, Mimi hapa, mtumishi wako! Daudi akamwambia, Usiogope, maana bila shaka nitakutendea mema; kwa ajili ya Yonathani, baba yako, nami nitakurudishia mashamba yote ya Sauli, babu yako; nawe utakula chakula mezani pangu daima. Akasujudu, akasema, Mimi mtumishi wako ni nini, hata ukamwangalia mbwa mfu kama mimi? Ndipo mfalme akamwita Siba, mtumishi wa Sauli, akamwambia, Mali yote yaliyokuwa ya Sauli na ya nyumba yake nimempa mjukuu wa bwana wako. Nawe utamlimia nchi hiyo, wewe, na wanao, na watumishi wako; nawe utamletea mjukuu wa bwana wako matunda yake, apate chakula ale; lakini Mefiboshethi, mjukuu wa bwana wako, atakula chakula mezani pangu siku zote. Basi huyo Siba alikuwa na wana kumi na watano na watumishi ishirini. Ndipo Siba akamwambia mfalme, Mimi, mtumishi wako, nitatenda hayo yote kama bwana wangu, mfalme, alivyoniamuru. Na kuhusu Mefiboshethi, mfalme alisema, Atakula mezani pangu, kama mmojawapo wa wana wa mfalme. Huyo Mefiboshethi alikuwa na mwana mdogo, jina lake akiitwa Mika. Na watu wote waliokaa nyumbani mwa Siba walikuwa watumishi wa Mefiboshethi. Basi Mefiboshethi akakaa Yerusalemu; maana alikuwa akila chakula siku zote mezani pa mfalme; naye alikuwa na kilema cha miguu yote miwili.
2 Samueli 9:3-13 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Mfalme akasema, Je! Hakuna hata sasa mtu ye yote wa nyumba ya Sauli, nipate kumtendea mema ya Mungu? Siba akamwambia mfalme, Yonathani anaye mwana hata sasa, aliye na kilema cha mguu. Mfalme akamwambia, Yuko wapi? Siba akamwambia mfalme, Tazama, yumo katika nyumba ya Makiri, mwana wa Amieli, katika Lo-debari. Basi mfalme Daudi akatuma watu, akamwondoa katika nyumba ya Makiri, mwana wa Amieli, katika Lo-debari. Basi Mefiboshethi, mwana wa Yonathani, mwana wa Sauli akaenda kwa Daudi, akaanguka kifudifudi, akasujudu. Daudi akasema, Mefiboshethi! Naye akaitika, Mimi hapa, mtumwa wako! Daudi akamwambia, Usiogope, maana bila shaka nitakutendea mema; kwa ajili ya Yonathani, baba yako, nami nitakurudishia mashamba yote ya Sauli, baba yako; nawe utakula chakula mezani pangu daima. Akasujudu, akasema, Mimi mtumwa wako ni nini, hata ukamwangalia mbwa mfu kama mimi? Ndipo mfalme akamwita Siba, mtumwa wa Sauli, akamwambia, Mali yote yaliyokuwa ya Sauli na ya nyumba yake nimempa mwana wa bwana wako. Nawe utamlimia nchi hiyo, wewe, na wanao, na watumwa wako; nawe utamletea mwana wa bwana wako matunda yake, apate chakula ale; lakini Mefiboshethi, mwana wa bwana wako, atakula chakula mezani pangu sikuzote. Basi huyo Siba alikuwa na wana kumi na watano na watumwa ishirini. Ndipo Siba akamwambia mfalme, Mimi, mtumwa wako, nitatenda hayo yote kama bwana wangu, mfalme, alivyoniamuru. Na kwa habari za Mefiboshethi, mfalme alisema, Atakula mezani pangu, kama mmojawapo wa wana wa mfalme. Huyo Mefiboshethi alikuwa na mwana mdogo, jina lake akiitwa Mika. Na watu wote waliokaa nyumbani mwa Siba walikuwa watumwa wa Mefiboshethi. Basi Mefiboshethi akakaa Yerusalemu; maana alikuwa akila chakula sikuzote mezani pa mfalme; naye alikuwa na kilema cha miguu yote miwili.
2 Samueli 9:3-13 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Mfalme akauliza, “Je, hakuna yeyote ambaye amebaki wa nyumba ya Sauli ninayeweza kumwonyesha wema wa Mungu?” Siba akamjibu mfalme, “Bado yupo mwana wa Yonathani, yeye ni kiwete miguu yote.” Mfalme akauliza, “Yuko wapi?” Siba akajibu, “Yuko nyumbani kwa Makiri mwana wa Amieli huko Lo-Debari.” Basi Mfalme Daudi akamtaka aletwe kutoka Lo-Debari, kutoka nyumbani kwa Makiri mwana wa Amieli. Mefiboshethi mwana wa Yonathani, mwana wa Sauli, alipofika kwa Daudi, akainama kumpa mfalme heshima. Daudi akamwita, “Mefiboshethi!” Mefiboshethi akajibu, “Ndimi mtumishi wako.” Daudi akamwambia, “Usiogope, kwa maana hakika nitakutendea wema kwa ajili ya baba yako Yonathani. Nitakurudishia ardhi yote iliyokuwa mali ya Sauli baba yako, nawe daima utakula chakula mezani pangu.” Mefiboshethi akasujudu akasema, “Mimi mtumishi wako ni nini hata uangalie mbwa mfu kama mimi?” Ndipo mfalme akamwita Siba mtumishi wa Sauli na kumwambia, “Nimempa mwana wa bwana wako kila kitu kilichokuwa mali ya Sauli na jamaa yake. Wewe, wanao na watumishi wako mtamlimia mashamba Mefiboshethi na kumletea mavuno, ili kwamba mwana wa bwana wako apate mahitaji yake. Naye Mefiboshethi mwana wa bwana wako atakula chakula mezani pangu daima.” (Siba alikuwa na wana kumi na watano, na watumishi ishirini.) Ndipo Siba akamwambia mfalme, “Mtumishi wako atafanya chochote bwana wangu mfalme atakachoagiza mtumishi wake kufanya.” Basi Mefiboshethi akala chakula mezani pa Daudi kama mmoja wa wana wa mfalme. Mefiboshethi alikuwa na mwanawe mdogo aliyeitwa Mika, nao watu wote wa nyumba ya Siba walikuwa watumishi wa Mefiboshethi. Naye Mefiboshethi akaishi huko Yerusalemu, kwa sababu daima alikula mezani pa mfalme, naye alikuwa kiwete miguu yote.